Social Icons

IMETOSHA

IMETOSHA

Tuesday, March 18, 2014

Uchaguzi Chalinze usirudie makosa ya Kalenga

kalengaa_182d8.jpg
Polisi akilinda Kituo cha Kupigia Kura cha Shule ya Chekechea ya Mchwivila katika Jimbo la Kalenga, Iringa jana . Picha na Edwin Mjwahuzi.
Uchaguzi wa ubunge katika Jimbo la Kalenga, mkoani Iringa ulimalizika mwishoni mwa wiki na Chama cha Mapinduzi (CCM), kiliibuka mshindi. Uchaguzi huo ulikuwa wa kuziba nafasi iliyoachwa wazi na Dk. William Mgimwa aliyefariki dunia Januari mwaka huu. Tunaipongeza Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kwa kuendesha uchaguzi ulio huru na haki. Pamoja na kujitokeza kasoro ndogondogo za hapa na pale, tume hiyo ilisimamia na kuendesha uchaguzi huo kikamilifu na kutoa haki kwa vyama vilivyoshiriki pasipo kupindisha sheria.
Huu ni utamaduni mpya katika nchi yetu, kwani sote ni mashahidi wa jinsi chaguzi mbalimbali zilizofanyika huko nyuma zilivyokuwa zikiendeshwa kwa mizengwe. NEC ilikuwa ikikiuka waziwazi kanuni na sheria za uchaguzi, hasa kutokana na shinikizo kutoka kwa wanasiasa na baadhi ya viongozi serikalini. Vyombo vya ulinzi na usalama navyo vilichangia kuwapo kwa kasoro nyingi katika chaguzi hizo kutokana na kuegemea upande mmoja na kukandamiza upande wa pili.
Wakati tukiipongeza Tume hiyo kwa kuendesha na kusimamia uchaguzi huo vizuri, hatuna budi kulaani vitendo vya kihuni na kiharamia vilivyofanywa na kikosi cha ulinzi cha CCM kinachojulikana kama Green Guards. Katika tukio linalopaswa kulaaniwa kwa nguvu zote na wapenda amani wote pasipo kujali misimamo yao ya kisiasa, walinzi wa kikosi hicho walimteka, kumtesa na kumdhalilisha mbunge wa Viti Maalumu, Rose Kamili wa Chadema ndani ya ofisi za CCM mkoani Iringa kwa madai ya kumkuta akitoa rushwa, huku yeye akisema alikuwa akitoa maelekezo kwa mawakala wa chama chake.

Mbunge huyo sasa amelazwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Iringa. Katika tukio hilo, polisi wanadaiwa kumgeuzia kibao na kumfungulia mashtaka badala ya kuwakamata makada hao wa CCM waliomteka na kumtesa kwa tuhuma za kutunga. Pia katika tukio la awali, walinzi hao wanadaiwa kumteka na kumtesa padre wa Kanisa la Orthodox katika Parokia ya Nyamihu, Costantino Mbilinyi kwa kumhusisha na kampeni za moja ya vyama vya siasa vilivyokuwa vikishiriki katika kinyang'anyiro hicho.
Hakuna asiyejua kwamba kujichukulia sheria mkononi ni kosa la jinai. Jukumu la kila mwananchi ni kutoa ripoti polisi au katika vyombo vingine vya ulinzi na usalama pale anapomwona mtu yeyote akitenda kosa. Kama walinzi wa kikosi cha Green Guards cha CCM walimkuta mbunge huyo akitoa rushwa walipaswa kutoa ripoti polisi na kutoa ushahidi badala ya kumteka, kumpeleka katika ofisi za chama hicho kumtesa na kumdhalilisha. Kama kweli walikuwa na nia njema, kwa nini walishindwa kutoa ripoti Takukuru ambacho ndicho hasa chombo kinachohusika na kupambana na vitendo vya rushwa?
Tumekuwa tukisema kwamba vikosi vya ulinzi vya baadhi ya vyama vya siasa vya Green Guards, Blue Guards na Red Brigades vinafanya vitendo vya jinai, hivyo vipigwe marufuku ili kuinusuru nchi yetu na vita au balaa zozote zinazoweza kuchochewa na vikosi hivyo. Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi anasema anatafuta dawa ya kukomesha vurugu zinazojitokeza mara kwa mara katika chaguzi zinazofanyika sehemu mbalimbali nchini. Hilo ni wazo jema. Tunamshauri aanze kwa kupiga marufuku vikosi hivyo vya mgambo vya vyama vya siasa ili makosa yaliyojitokeza Kalenga yasijirudie katika uchaguzi wa Jimbo la Chalinze utakaofanyika mwezi ujao.
Chanzo, mwananchi.

No comments:

Post a Comment