Watu
wanne wamefariki dunia na wengine kadhaa bado wamenasa kwenye kifusi
katika machimbo madogo ya Kalole kata ya Lunguya wilayani kahama mkoani
Shinyanga kufuatia kuporomoka kwa duara waliyokuwa wanachimba Dhahabu.
Diwani
wa Kata ya Lunguya Benedicto Manwari ameiambia Radio Kahama FM tukio
hilo limetokea jana jioni, na kwamba hadi kufikia jioni hii miili ya
watu wane imeopolewa na majeruhi mmoja ambaye anapatiwa matibabu katika
kituo cha Afya Lunguya.
Manuari amesema miili mitatu ni wakazi wa hapo Kalole na mmoja ni wa
kutoka Bariadi mkoani Simiyu ambapo tayari umekwishasafirishwa na kwamba
Yule majeruhi ambaye amevunjika mkono na ana jeraha usoni ni mtu wa
Morogoro.
Amesema kufuatia sensa iliyofanywa, inakisiwa watu watatu wakazi wa
kijijini hapo bado wamenasa katika kifusi hicho ingawaji juhudi za
uopoaji bado zinaendelea japokuwa hakuna msaada wowote wa zana za kisasa
ulioweza kupatikana.
Manuari amesema Serikali ngazi ya wilaya imepewa taarifa hizo na Jeshi la Polisi limekwishafika kwenye eneo la tukio.
Balaa la watu kupoteza maisha katika machimbo madogo ya madini bado
halijapata jibu la kudumu kwa wilaya ya Kahama ambayo imekuwa ikiibuka
kugunduliwa madini karibu kila sehemu ya ardhi yake.
No comments:
Post a Comment