Tumekuwa na mazungumzo na wenzetu na hili jambo ni moja ya mambo ambayo
tumekubaliana kushirikiana, maana kila upande unahitaji mwenzake katika
kuikomboa nchi hii” Freeman Mbowe,Mwenyekiti wa Chadema( katikati)
Dodoma. Mvutano katika mchakato wa Katiba umeimarisha ushirikiano wa vyama vya Chadema, CUF na NCCR-Mageuzi na sasa kuna mpango wa kuundwa upya kwa Baraza la Mawaziri Kivuli ambalo litawajumuisha wabunge wa vyama hivyo.
Baraza la Kivuli la sasa linawajumuisha wabunge
kutoka Chadema pekee, ambacho kinaunda Kambi Rasmi ya Upinzani bungeni
tangu kuanza kwa Bunge la 10, Novemba 2010.
Mwenyekiti wa Chadema ambaye pia ni Kiongozi wa
Kambi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe alithibitisha kuwapo kwa mpango
huo na kwamba atapanga upya baraza lake katika siku za mwanzo za Bunge
la Bajeti linalotarajiwa kuanza mapema mwezi ujao.
“Tumekuwa na mazungumzo na wenzetu na hili jambo
ni moja ya mambo ambayo tumekubaliana kushirikiana, maana kila upande
sasa umekubali kuwa unahitaji mwenzake katika harakati za kuikomboa nchi
hii,” alisema Mbowe.
Taarifa za kuwaingiza wabunge wa NCCR-Mageuzi na
CUF katika Baraza la Mawaziri Kivuli, imekuja wakati ambao vyama hivyo
pamoja na wajumbe wengine kadhaa wa Bunge Maalumu la Katiba wakiwa
wameunda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).
Ukawa ndiyo iliyowaongoza baadhi ya wajumbe wa
Bunge Maalumu kutoka nje juzi kususia mchakato wa Katiba Mpya kutokana
na kile ilichodai kuwa ni kutoridhishwa na jinsi mambo yanavyokwenda.
Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia
alithibitisha kuwapo kwa mpango huo: “Kweli ninafahamu kuwapo kwa mpango
huo, lakini niseme tu kwamba mazungumzo haya hayakuanza sasa,
yamekuwapo kwa muda mrefu kuona namna ya kushirikiana,” alisema Mbatia.
Naibu Katibu Mkuu wa CUF, Tanzania Bara, Julius
Mtatiro alipoulizwa hakukanusha wala kukubali kuhusu kuwapo kwa mpango
huo, badala yake alitaka atafutwe Mwenyekiti wa chama hicho, Profesa
Ibrahim Lipumba.
Profesa Lipumba hakupatikana jana kuzungumzia
suala hilo kwani simu yake ilikuwa ikiita bila majibu na hata
alipotumiwa ujumbe hakujibu.
Akizungumza kupitia simu yake ya mkononi, kiongozi
wa wabunge wa CUF, Habib Mnyaa alisema hakuwa akifahamu chochote kuhusu
mpango huo kutokana na kutokuwepo nchini kwa siku kadhaa.
Pigo kwa CCM
Kuendelea kuimarika kwa ushirikiano wa kisiasa
hasa baina ya CUF na Chadema ni pigo kwa chama tawala, CCM ambacho
kinaunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK) na CUF Tanzania Visiwani.chanzo Mwanainchi

No comments:
Post a Comment