Social Icons

IMETOSHA

IMETOSHA

Sunday, May 4, 2014

DK SHEIN ATAHADHARISHA UPENDELEO MAKAZINI


Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amewatahadharisha watendaji wakuu wa Wizara na Idara za Serikali kujiepusha na upendeleo wakati wakiendesha zoezi la kupitia Miundo ya Utumishi ya wafanyakazi wa Umma(scheme of service).Tahadhari hiyo ameitoa leo wakati alipokuwa akizungumza na wafanyakazi nchini katika kilele cha maadhimisho ya siku ya wafanyakazi huko katika hoteli ya Bwawani mjini Unguja.Amewataka watendaji wanaohusika na zoezi hilo kulifanya kwa uadilifu na kwa umakini mkubwa kwa kuwapanga watumishi kulingana na kiwango cha elimu, taaluma na uzoefu walionao huku wakiainisha na kubainisha majukumu ya kila mtumishi.Aliwaeleza mamia ya watumishi wa umma waliohudhuria mkutano huo kuwa hivi sasa Serikali imo katika mchakato wa kupitia Miundo ya Utumishi wa wafanyakzi wa umma lengo likiwa ni kuhakikisha watumishi wanapata mishahara stahiki kulingana na elimu, taaluma na uzoefu wa utumishi wao.Hata hivyo alisisitiza kuwa asingependa kuona zoezi hilo linatawaliwa na upendeleo ambapo mbali ya kuitia Serikali lawamani bali pia kuwavunja moyo baadhi ya watumishi na hata kusababisha wengine kuondoka nchini.



Dk. Shein aliwahakikishia watumishi wa umma kuwa Serikali ingependa kila mara kuongeza maslahi yao kwa lengo la kuwapunguzia makali ya maisha lakini dhamira hiyo inakwenda sambamba na kukua kwa uchumi ambako msingi wake ni kwa watumishi hao kufanyakazi kwa kujituma na kuongeza tija sehemu zao za kazi.
Alifafanua kuwa tangu Serikali ya Awamu ya Saba iingie madarakani imekuwa ikichukua hatua mbalimbali kuimarisha maslahi ya watumishi pamoja na mazingira ya kazi ikiwemo kuongeza mishahara na marurupu mara mbili mwaka 2010/2011 na mwaka 2013/2014.
Aliwataka watumishi wa umma kujivunia mafanikio waliyoyapata na kufafanua kuwa watumishi hivi ni tofauti na wakati wa ukoloni ambapo hivi sasa wanaweza kumiliki nyumba za kisasa za kuishi na kwa wasiomiliki angalau wana uwezo wa kupanga nyumba badala ya chumba kama ilivyokuwa wakati wa ukoloni.
Hata hivyo aliwataka wafanyakazi nchini kufanya kazi kwa bidii, ubunifu na kuacha ubabaishaji kwani tafiti zinaonesha kuwa bado watumishi wengi wakiwa kazini wanatumia muda mdogo kufanyakazi walizoajiriwa
Dk. Shein alisisitiza ushirikiano wa UTATU kuwa ni suala muhimu lisilokwepeka kwani ni lazima masula ya watumishi yajadiliwe na pande zote husika kwa maslahi ya watumishi, waajiri na jamii kwa ujumla.
Kwa hiyo alitoa wito kwa wizara na Idara za Serikali ambazo bado suala hilo halijapewa kipaumbele kufanya hivyo na kueleza kuwa hakuna sababu kwa kamati za uongozi za wizara kutoundwa au kwa zile zilizopo kutotimiza wajibu wake.

Mhe Rais aliueleza uongozi wa Shirikisho la Vyama Huru vya Wafanyakazi –ZATUC kuwasiliana na Serikali mara kwa mara ikiwemo Ofisi yake kujadili masuala mbalimbali pasi na kusubiri maadhimisho kama hayo kueleza matatizo yao.
Kuhusu suala la ajira Dk. Shein alisema lengo la serikali ni kupunguza ukosefu wa ajira kutoka asilimia 17 hivi sasa hadi asilimia 11 ifikapo mwaka 2015 na kwamba hatua mbalimbali zinaendelea kuchukuliwa kufikia lengo hilo.
Kwa upande wake Kaimu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Kazi na Utumishi wa Umma ambaye pia ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Idara Maalum Haji Omar Heri alitoa wito kwa uongozi wa ZATUC kushajiisha watumishi kuanzisha matawi katika Wizara na Idara za Serikali ili kuimarisha UTATU kwa faida ya pande zote.
Alisema kuwa Wizara yake imekuwa na mahusiano mazuri na ZATUC hivyo ni wajibu wa pande zote kuona kuwa mahusiano hayo yanaimarishwa kwa maslahi ya Taifa.
Katika risala yao iliyosomwa na Kaimu Katibu Mkuu wa ZATUC Maalim Mussa Omar Tafurwa wafanyakazi  hao waliiomba Serikali kuongeza kiwango cha chini cha mshahara hadi shilingi 300,000.00 na kutaka kutekelezwa kwa Sheria ya kuwepo kwa mkataba wa huduma kazini.
Risala hiyo ilitaka pia kuangaliwa upya mabadiliko ya mishahara yaliyofanywa hivi karibuni na Serikali kwa watumishi wenye uzoefu mkubwa kazini na Serikali kuangalia suala la kuvunjwa sheria ya Kamati  za Uongozi katika Wizara na Taasisi za Serikali ambazo hutoa fursa kwa watumishi kushiriki katika vikao hivyo na kutoa maoni yao.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Taifa ZATUC Dk. Zahran Mohamed Nassor aliitaka Serikali kutekeleza baadhi ya vipengele vya Sheria ya Mfuko wa Hifadhi ya Jamii ambavyo Waziri husika kwa miaka 16 tangu kuundwa sheria hiyo amezuia vipengele hivyo kutumika.

No comments:

Post a Comment