Mtu mmoja ambaye hakutaka kujulikana jina lake amekumbwa na
mkasa wa kuvunjiwa na kuibiwa pesa kiasi kisichopungua shilingi za kitanzania
milioni 10 alipokuwa katika mgahawa wa Kawe Club jijini Dar es Salaam leo
jioni.
Akielezea tukio hilo, shuhuda ambaye pia hakutaka kutajwa
jina lake anasema ilikuwa majira ya saa kumi na nusu wakati majambazi wasiopungua
5 walipovunja kioo upande wa kushoto mbele cha gari aina ya Toyota Hilux yenye
usajili T163CUL (Pichani) na kuchukua hela kiasi cha shilingi milioni 10.
“Walikuja na pikipiki wakati mi naosha gari hiyo, nikiwa
upande wa pili (yaani wa dereva) naosha tairi ya mbele, nikasikia mshindo wa
kuvunjwa kioo, nikaona watu wawili kwenye pikipiki mmoja ameshika bunduki
wakichukua pesa kwenye gari na kisha wakaondoka mbio” alieleza kijana huyo
Kijana huyo anasema alipiga kelele za wezi, walinzi wakiwa
wanashangaa hawajui la kufanya. Kwa mujibu wa kijana huyo, kelele zake
zikasaidia kwani watu wanaofanya shughuli zao eneo la baharini karibu na Kawe
Club walisikia na kuanza kuwakimbiza watu hao.
Walipofika mbele kidogo wakiwa wanawakaribia, ndio jambazi
mmoja akapiga risasi hewani ndipo watu wote wakalala chini kuhofia usalama wao.
Kijana mwingine aliyekuwa anapita njia ya kuelekea Kawe
Beach anasema aliposikia kelele ya risasi kisha akaona pikipiki gari aina ya
RAV4 zikifuatana kwa mwendo mkali sana.
Imedaiwa tukio zima lilichukua si zaidi ya dakika tatu mpaka
watu hao kutokomea. Hata hiyvo meneja wa Kawe Club alifanikiwa kuita polisi
ambao walifika muda si mrefu kufuatilia tukio hilo.
Mmiliki wa gari hilo anasema alikuwa ametoka benki ya CRDB
Mlimani City kuchukua pesa hizo na ndipo alipoamua kwenda kula samaki Kawe Club
kabla ya kukumbwa na mkasa huo.
No comments:
Post a Comment