Nasra alipokuwa katika hospitali ya mkoa
wa Morogoro.
MTOTO mwenye umri wa miaka minne
aliyefungiwa ndani ya boksi kwa zaidi na miaka mitatu mkoani Morogoro,
amehamishiwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) kwa ajili ya uchunguzi
na tiba zaidi huku wataalamu wakikuna vichwa namna ya kumrudishia afya yake.
Imeelezwa jopo la madaktari bingwa wa magonjwa mbalimbali ya binadamu wakiwemo
wataalamu wa saikolojia, wanahitajika kwa ajili ya kumwezesha mtoto huyo mwenye
ulemavu kuwa katika hali ya kawaida.
Aidha, pamoja na uhitaji wa jopo la
wataalamu hao, mtoto huyo ambaye amelazwa katika wadi ya watoto, atahamishiwa
katika wadi maalumu ya watoto wenye utapiamlo awe karibu na uangalizi wa lishe
baada ya kubainika ana udhaifu mkubwa wa lishe.
Wakizungumza na gazeti hili jana
jijini Dar es Salaam kwa nyakati tofauti hospitalini hapo, Daktari Bingwa wa
Watoto wa MNH, Dk Mwajuma Ah- mada alisema mtoto huyo hajazidiwa kuumwa.
Alisema walimpokea juzi usiku na
hatua za awali zilizofanywa ni pamoja na kuchukua baadhi ya vipimo kwa ajili ya
uchunguzi.
“Mtoto aliletwa hapa jana (juzi)
usiku, baadhi ya vipimo vimechuku- liwa, vingine atafanyiwa leo (jana) ikiwa ni
pamoja na kumfanyia huduma ya kum scan (kumwingiza kwenye mashine maalumu)
mwili mzima ili tufahamu tatizo na tiba sahihi,” alisema Dk Ahmada.
Alisema huduma ya tiba kwa mtoto
huyo siyo ya daktari bingwa mmoja bali inahitaji jopo la wataalamu waki- wemo
wa mifupa, saikolojia, viungo na magonjwa mbalimbali ya binadamu kumsaidia
mtoto huyo.
“Kwa sasa hatuwezi kusema lolote
kubwa kuhusu mtoto huyo ndio kwanza kafika na ndiyo tuko kwenye hatua ya awali
ya kuchukua vipimo, na leo atafanyiwa huduma ya kumulikwa mwili mzima ili tujue
tunaanzia wapi”, alisema Dk Ahmada. Alisema pamoja na kusubiri majibu ya
vipimo, hatua wanayochukua ni ya kumhamishia kwenye wadi ya watoto wenye
utapiamlo, ili kutibu maradhi hayo ambayo ndio yameonekana awali, kwani mtoto
amekosa lishe na viru- tubisho muhimu vya awali.
Alifafanua, katika hatua hiyo ya
awali, mtoto huyo atakuwa akipewa maziwa ya lishe na kuendelea na tiba ya dawa
za kuua vijasumu kutokana na kusumbuliwa na vichomi.
Akizungumzia kwa ufupi ikiwa mtoto
huyo anaweza kurejea katika hali ya kawaida kwa viungo kunyooka na kutembea, Dk
Ahmada alisema pamoja na kusubiri majibu ya vipimo, lakini pia tiba ya mtoto
inategemea zaidi historia ya mtoto mwenyewe. Mlezi azungumza Kwa upande wake,
mlezi wa mtoto huyo , Josephina Joel akizungumza na gazeti hili wadini hapo
alisema mtoto anaendelea vizuri ingawa juzi alikuwa na homa. Hata hivyo alisema
imeshuka, na kwamba kadri siku zinavyosonga, anaona uchangamfu wa mtoto.
No comments:
Post a Comment