MAMA mjamzito aliyekuwa na mimba ya
miezi tisa, Anjela Domiano (42), mkazi wa Nanenane katika Manispaa ya Morogoro,
amefariki baada ya kunywa sumu ya panya.
Tukio hilo lilitokea juzi, saa 2.30
asubuhi, katika eneo la Kichangani katika Manispaa ya Morogoro.
Kamanda wa Polisi mkoa wa Morogoro,
Leonard Paul, alisema jana kuwa, marehemu
Angela alifia katika hospitali ya
mkoa, ambako alipelekwa kwa ajili ya kupatiwa matibabu.
Alisema siku ya tukio, Angela
alikutwa akiwa ameanguka huku akitapatapa katika eneo la Kichangani.
Alisema polisi walipata taarifa na
kufika katika eneo la tukio na kumchukua mama huyo na kumfikisha katika
hospitali hiyo, ambapo alifariki wakati akipatiwa matibabu.
“Wasamaria wema walipomwona mama
huyo kaanguka chini, walitoa taarifa polisi na walipofika eneo la tukio,
walimkuta akiwa anatapatapa na kuamua kumkimbiza hospitali ili kuokoa maisha
yake,” alisema.
Alisema Angela alikutwa na sumu ya
panya katika pochi yake na uchunguzi wa awali umeonyesha kuwa, alifariki
kutokana na kunywa sumu hiyo.
Kamanda huyo alisema hawakuweza
kumhoji Anjela kutokana na hali yake kuwa mbaya na wanaendelea na uchunguzi wa
tukio hilo.(E.L)
No comments:
Post a Comment