Ugonjwa wa kuanguka na kupiga kelele unaowakumba baadhi
ya wasichana katika shule mbalimbali nchini,
umetajwa kusababishwa na maambukizi ya hofu inayosababisha mwili
kupata dalili za magonjwa yasiyokuwepo.
Mtaalamu wa saikolojia na theolojia, Mchungaji John Rowse
kutoka taasisi ya The Uhakika Christian Education Trust Fund kutoka
Mbeya, alisema hayo hivi karibuni baada ya kutembelea shule zinazopata tatizo hilo mara kwa mara na
kuzungumza na wazazi, wanafunzi na walimu wa shule hiyo.
Alisema kuna mambo kadhaa yanayochangia kujenga hofu hiyo
ambayo mwili hujitayarisha kuambukizwa, ikiwemo vitisho vya maisha kwa
wanafunzi vinavyotokana na mambo mbalimbali kama vile ugomvi na mabadiliko
ambapo miili yao inahangaika kujihami.
Kwa mujibu wa Mchungaji huyo
, upo uwezekano kuwa baadhi
ya wanaoanguka, ni wasichana
wanaonyanyaswa nyumbani, wengine wanafundishwa kujidharau na wengine
wanabaguliwa na kufanyiwa unyanyapaa shuleni.
Sababu nyingine ya kuanguka kwa wasichana shuleni kwa mujibu
wa Mchungaji Rowse, ni hofu wanayopewa
wasichana hao na waganga wa kienyeji
wanaotabiri au kupiga ramli, pamoja na wachungaji au wainjilisti
wanaokemea mapepo huku wakiwashika
kichwani, begani au kwenye shingo na kuwatetemesha wasichana hao.
Mchungaji Rowse alisisitiza kuwa dawa pekee ya
kutibu ugonjwa huo, ni utulivu
kwani wanafunzi hao hususani
wasichana huambukizana kwa hofu
hivyo matibabu yake ni kupunguza hofu na
mawazo.
“Hofu hiyo kwa wasichana
hao husababishwa kwa imani potofu, waganga wa kienyeji wanaotabiri au kupiga ramli ... waganga hawa
wanapenda kujenga hofu ya uchawi, ili baadaye wajidai kwamba ni wao
waliondoa laana na kuleta uponyaji.
“Dawa ya kusaidia kuzuia matukio hayo ni kuwa na mipango ya
kupunguza msongo wa mawazo shuleni, hasa miongoni mwa
wasichana,” alisema.
Mchungaji Rowse
alipendekeza machifu na waganga wa
jadi wasikaribishwe shuleni kuwaombea
wasichana hao kwa kuwa watawaongezea hofu.
Pia alipendekeza wachungaji au wainjilisti wanaopenda
kushika mtu kichwani, begani au kwenye shingo na kumtetemesha, wasikaribishwe
shuleni kwa kuwa nao pia ni hatari.
“Hata wale wanaokemea mapepo kwa sauti kubwa na wakati
wakifanya hivyo hupenda kumwangalia msichana kwa ukali jicho kwa jicho.
”Katika mazingira hayo,
watoto watapata tena
hofu na wakianguka tena watasema
ni pepo, lakini sivyo. Afadhali mchungaji wa amani, amwombee kila mwanafunzi
aliyekumbwa na ugonjwa huo kwa sauti ndogo tu na kwa upole na upendo na
kumfariji na utulivu. Asitamke wazi neno lo lote juu ya mapepo,”
alisisitiza.
Alishauri kuwa kila shule iwe na mwalimu au mshauri wa kike
ambaye hatoi adhabu kwa wasichana, atakayepaswa kujenga urafiki nao na kuwa
karibu nao, ili wamwamini na kumwelezea mateso yao ya maisha, nyumbani na
shuleni.
Alisisitiza kuwa
wanafunzi wa kike wapewe nafasi za kukutana katika vikundi,
ili wajadiliane pamoja kuhusu mambo yoyote, pia walimu
wajitahidi kumpa kila msichana nafasi ya kusikilizwa.
Alitoa mfano wa Shule ya Msingi Inyonga wilayani Mlele
katika Mkoa wa Katavi, ambayo aliitembelea na kuzungumza wazazi, wanafunzi na walimu wa shule hiyo.
Alisema baada ya shule hiyo kuanza kutekeleza ushauri
huo, Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Casto
Ismail, alimwambia kuwa kasi ya matukio imepungua.
“Mwalimu Mkuu huyo alinieleza kuwa wamekuwa na mitihani ya
darasa ya saba, ambao kwa kawaida husababisha msongo wa mawazo kwa wanafunzi, lakini hakuna mwanafunzi
wa darasa ya saba hata mmoja aliyeanguka wakati huo…katika madarasa mengine ni
wachache walioanguka.
“Niliwaambia walimu wawe na uvumulivu. Mambo yatatulia kweli
baada ya mabadiliko ya imani ya wazazi na jamii… lakini watalaamu bado
wanashindwa kuelewa kwa nini hali hiyo inakutwa sana kwa wasichana na
wanawake,” alisema Mchungaji Rowse.
Mwandishi alifika katika Shule ya Msingi Inyonga na
kuzungumza na Mwalimu Ismail, ambaye alieleza kuwa ugonjwa
huo ulidumu kwa zaidi ya miezi sita tangu ulipowakumba wasichana wanaosoma
katika shule hiyo Novemba mwaka jana.
Alifafanua kwamba kasi ya kuanguka kwa wasichana hao shuleni
hapo imepungua baada ya kuanza
kufanyia kazi ushauri wa Mchungaji Rowse, aliyefika shuleni hapo na kuzungumza na wanafunzi. Pia alitoa
semina kwa wanafunzi, walimu na wazazi.


No comments:
Post a Comment