Mtoto Merina Mathayo (15) amelazwa katika Taasisi ya Tiba ya
Mifupa (Moi) Muhimbili Dar es Salaam, baada ya kuteswa na kujeruhiwa kichwani
kwa kipigo maeneo mbalimbali ya mwili na bosi wake kwa miaka miwili..Merina
amelazwa Moi baada ya kupewa rufaa na Hospitali ya Mwananyamala alipokuwa
amelazwa awali, kutokana na majeraha hayo ambayo yanadaiwa kusababishwa
kung'atwa kwa meno na kupigwa kwa vitu mbalimbali mara kwa mara.Akizungumza kwa
shida Merina alisema amekuwa katika hali ya mateso tangu mwaka 2012, kwani bosi
wake huyo ambaye anamtaja kuwa ni mwanasheria mkazi wa Boko amekuwa na tabia ya
kumpiga na vitu mbalimbali akiwa amemvua nguo.
"Haya marejaha niliyonayo sasa, alinipiga kwa fagio la
chooni akamalizia na jagi, kisha akapiga simu nyumbani kwetu huko Ishozi Kiziba
mkoani Kagera, akawaambia wazazi kwamba amenikung'uta kichwa kwa sababu mimi ni
mjeuri," alieleza Merina na kuongeza:
"Mara kwa mara amekuwa na tabia ya kunivua nguo na
kunipiga na chochote anachojisikia, ananing'ata kisha ananipakaza chumvi kwenye
majeraha," alisema Merina.
"Mara zote anazonipiga huniambia kwamba sijafanya kazi
vizuri au sijamaliza kuzifanya, lakini mwanaye ambaye ninamlea huwa analia sana
akimwambia usimpige dada, mwachie," alisema Merina.
Alibainisha kwamba dada wa mtuhumiwa huyo anayemtaja kwa
jina la Josephine Rwechungura, baada ya kukerwa na vitendo hivyo vya kikatili
alivyotendewa ndiye alimpeleka hospitali.
Merina alisema kuwa hajawahi kupewa malipo yake na bosi huyo
ambaye walikubaliana mshahara wa Sh40,000 na Sh20,000 hutumwa kwa wazazi wake
na zilizobaki alikuwa anadai kwamba anamwekea.
Moi yajitolea kumsaidia
Ofisa Uhusiano wa Moi, Patrick Mvungi alisema wamempokea
Merina juzi saa 7.00 usiku, baada ya kuelezwa historia ya majeraha yake uongozi
umeguswa na kujitolea kugharimia matibabu yake.
"Madaktari wamesema kwamba anatakiwa kufanyiwa kipimo
kikubwa cha CTS can ambacho kitawezesha kujua majeraha aliyonayo yana ukubwa
gani, gharama zake ni Sh250,000 ambazo Moi itazitoa na kumpatia matibabu
bure," alisema Mvungi.
Awali Katibu Afya wa Hospitali ya Mwananyamala, Edwin
Bisakala alisema Merina alipelekwa hospitalini hapo Juni 11 mwaka huu na
msamaria mwema, baada ya madaktari kumwona walibaini kwamba ana majeraha
makubwa kichwani."Walimwona ana maumivu makali pia majeraha kichwani, kwa
kiwango cha hospitali yetu hatuwezi kutibu kichwa, kwa sababu anatakiwa
kuchunguzwa kwa kina kiwango cha majeraha yake kwa vifaa vya kitaalamu, hivyo
tumempa rufaa ya Muhimbili," alisema.
Polisi
Kamanda wa Mkoa wa Kipolisi Kinondoni, Camillius Wambura
alikiri kupokea taarifa ya tukio hilo, ambapo mtuhumiwa ametoweka nyumbani
kwake hivyo anasakwa, polisi wanaoshughulikia ni wa Kituo cha Wazo.
"Taarifa hiyo tunayo kwa sasa tunamsaka mtuhumiwa huyo
maana ili sheria iweze kuchukua mkondo wake, kwa sasa hatuwezi kumtaja jina
lake," alisema.
Tukio hili ni mfululizo wa matukio ya kusisimua yanayozidi
kuibuliwa ndani ya jamii katika kipindi cha mwezi sasa, likiwamo lililohusisha
mtoto Nasra Mvungi (marehemu) aliyekutwa amefichwa kwenye boksi kwa miaka
mitatu huko mkoani Morogoro.
Watu watatu akiwamo baba mzazi wa Nasra, Rashid Mvungi (47),
mkazi wa Lukobe pamoja na wanandoa Mariam Said (38) ambaye ni mama yake mkubwa
na mumewe Mtonga Omar (30), wakazi wa Mtaa wa Azimio, Kata ya Kiwanja cha
Ndege, wameshtakiwa wakidaiwa kumtesa na kumsababishia kifo mtoto huyo.
Mtoto huyo aligundulika akiwa katika hali ya mateso, kwani
alikutwa akiwa mchafu na ilithibitika kwamba kwa mara ya mwisho aliogeshwa
Julai mwaka jana, huku viungo vya mwili wake mikono na mgongo vikiwa vimepinda.
Tukio lingine linahusu mtumishi wa kazi za ndani Yusta
Kashinde, anayedaiwa kung'atwa sehemu mbalimbali za mwili na kuunguzwa na pasi
na bosi wake Amina Maige, hivyo kumsababishia majeraha makubwa. Tayari Maige
amefikishwa mahakamani kwa tukio hilo.
CHANZO mwananchi
No comments:
Post a Comment