MHADHIRI wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk. Kitilla
Mkumbo, amefichua siri ya kwenda mahakamani kwa Mbunge wa Kigoma Kaskazini,
Zitto Kabwe (CHADEMA), kwamba ni baada ya jopo la wasomi kumshauri kufanya
hivyo.
Dk. Kitilla alisema kabla ya hapo, mbunge huyo
alikuwa
tayari kuwaachia viongozi wa chama chake wamvue uanachama kama alivyofanyiwa
yeye na aliyekuwa Mwenyekiti wa CHADEMA Mkoa wa Arusha, Samson Mwigamba.
Alitoa kauli hiyo juzi wakati akiendesha mafunzo ya siku
moja kwa viongozi wa mikoa na wajumbe wa Chama cha ACT–Tanzania juu ya
historia, misingi, itikadi na falsafa ya chama hicho.
Alisema kwamba jopo la wasomi walimuelezea Zitto umuhimu wa
kuangalia maslahi ya watu waliomchagua na njia inayotaka kutumika kufikia
uamuzi wa kumvua uanachama wake katika chama hicho.
“Sisi tuliridhia kuvuliwa uanachama kwa kuwa hakukuwa na
maslahi ya moja kwa moja yanayoweza kuathiri maisha yetu na familia zetu,
lakini kwa Zitto hilo lingetokea na kumuathiri kwa mazingira yote mawili,”
alisema.
Kuhusu kuandaa waraka unaodaiwa kuwa ni wa usaliti ndani ya
CHADEMA, Dk. Kitilla alisema katika utatu wao wakiwa wanachama wa CHADEMA
wakati huo walikuwa na nia ya mabadiliko ya muda mrefu ndani ya chama hicho
baada ya kubaini baadhi ya mambo hayaendi sawa.
“Mimi, Mwigamba na Zitto tumekuwa na nia ya muda mrefu ya
kuleta mabadiliko ndani ya CHADEMA, matamanio yetu ya mabadiliko yalihitimishwa
kwa kuandika waraka wa mabadiliko, ukiainisha sababu za mabadiliko na mikakati
yetu ya kushinda uchaguzi ndani ya chama,” alisema Dk. Kitilla.
Aliongeza baada ya Mwigamba kukutwa na waraka wa mabadiliko
uliodhaniwa kuwa ni uhaini, walifukuzwa ndani ya chama hicho na kwamba
hawakuona sababu ya kujiunga na chama kingine chochote cha siasa katika vyama
vilivyopo.
Kwamba baada ya hali hiyo, vyama mbalimbali viliwafuata na
kutaka wajiunge navyo, ikiwamo CCM, na waliwakatalia kwa kuamini kujiunga na
chama hicho ni usaliti wa dhamira zao katika kufikia mabadiliko, na kuwa nchi
ilipofika sio muda wa kukisaidia kuendelea kubaki madarakani.
Alisema matatizo yaliyopo katika vyama vya upinzani ni ya
asili na yanafanana kwa kiasi kikubwa, ikiwa ni pamoja na kukosekana kwa
umakini, kuwepo kwa hisia umiliki pamoja na kukosekana kwa demokrasia.
Dk. Kitilla ambaye kwa sasa ni mshauri wa ACT-Tanzania,
alisema iwe ni marufuku kwa mwanachama wa chama hicho kuzungumzia vyama vingine
badala ya kuwazungumzia wananchi na matatizo yao.
Chanzo:Tanzania Daima
No comments:
Post a Comment