Social Icons

IMETOSHA

IMETOSHA

Wednesday, July 23, 2014

Maambukizi VVU Kinondoni yazidi kitaifa



MAAMBUKIZI ya ugonjwa wa ukimwi (VVU) katika Manispaa ya Kinondoni yanaelezwa kuongezeka kutoka asilimia 5.6 na kufikia 6.8 kiwango ambacho kimezidi kile cha kitaifa.
Hayo yalisemwa na Mratibu wa Kudhibiti Ukimwi wa Manispaa hiyo, Mercy Ngekeno, wakati wa kufunga semina ya siku mbili iliyowahusisha watu wanaoishi na VVU kutoka katika manispaa hiyo.
Ngekeno alizitaja sababu zilizochangia kuongezeka kwa maambukizi hayo kuwa ni pamoja na 
 
wingi wa madanguro, kaka poa na machangudoa yanayopatikana ndani ya Manispaa ya Kinondoni.
Alisema sababu nyingine ni kuwepo kwa muingiliano mkubwa wa watu kutoka maeneo mbalimbali wanaokuja kwa ajili ya utafutaji ajira na kufanya shughuli nyingine kama ujenzi na miradi mbalimbali.
“Manispaa yetu ina mwingiliano mkubwa wa watu, lakini madanguro, baa, klabu za usiku na machangudoa wamekuwa wengi sana, vitu hatarishi ni vingi ndiyo maana maambukizi yako juu… tunachofanya sisi ni kutoa elimu ya kujitambua ili kuepuka maambukizi mapya,” alisema Ngekeno.
Katika semina hiyo Naibu Meya wa Manispaa ya Kinondoni, Songoro Mnyonge, ambaye ndiye Mwenyekiti wa Kamati ya Kudhibiti Ukimwi, alitoa sh. milioni 27 kwa vikundi vitatu vya ujasiriamali vya watu wanaoishi na VVU ili viweze kukopeshana na kupata mitaji ya kuanzisha biashara.
“Wapo wanaosema kwanini fedha zinapelekwa kwenye ukimwi na zisielekezwe kwenye vipaumbele vingine, lakini bado eneo hili inahitaji kukumbushana kwani binadamu ameumbwa kusahau, tukisema tunyamaze hali itakuwa mbaya zaidi,” alisema Songoro.

No comments:

Post a Comment