*Awaasa wananchi wasikubali kugeuzwa mtaji na wagombea
WAZIRI MKUU Mizengo Pinda amewaonya Watanzania kuwa makini
na watu wanaotumia rushwa ili kupata nafasi za uongozi na hasa kwenye uchaguzi
mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba, 2015.Ametoa onyo hilo leo mchana (Jumapili,
Julai 27, 2014) wakati akizungumza na mamia ya waumini na viongozi mbalimbali
waliohudhuria ibada ya uzinduzi wa dayosisi mpya ya Ruvuma ya Kanisa la
Kiinjili la
Kilutheri Tanzania (KKKT) na kuwekwa wakfu Askofu Amon Mwenda
aliyeteuliwa kuongoza dayosisi hiyo.“Ninawasihi wananchi wawe makini na
viongozi wanaopenda kutoa rushwa hasa katika kipindi hiki cha kuelekea kwenye
uchaguzi mkuu. Kama mtu ana nia ya kweli ya kuongoza ni kwa nini atumie fedha
ili kupata nafasi ya uongozi?,” alihoji.“Tatizo ni kwamba hata wananchi hivi
sasa wanakubali kupokea kile kinachotolewa na wagombea. Atakuja huyu atakupa
hiki na mwingine naye atakupa kile, lakini ujue akiingia madarakani anaanza
kurudisha haraka vile alivyowagawia,” alisema.
Aliwaonya wananchi kuwa makini ili wasije wakageuzwa mtaji
wa kuwanufaisha watu binafsi. “Tukikubali kutumika ni sawa tutapata viongozi
wakati wa uchaguzi, lakini watakuwa ni wale wasio na hofu ya Mungu, wenye
kujali maslahi yao kuliko ya wananchi waliowachagua,” aliongeza.
Aliwaomba viongozi wote wa dini waliohudhuria sherehe hizo
pamoja na waumini wote waendelee kuliombea Taifa ili Mungu aliepushe na janga
hilo la watu kupenda rushwa. Alitumia fursa hiyo pia kuwaomba wazidi kuuombea
mchakato wa kupata Katiba mpya ili wabunge wote warejee ndani ya Bunge na
kuikamilisha kazi waliyoianza.
Alimuomba Askofu huyo mpya apokee jukumu hilo kwa mikono
miwili na kumuahidi kuwa kama Serikali watakuwa naye bega kwa bega kuwaongoza
Watanzania walioko kwenye dayosisi yake. Dayosisi hiyo mpya inahusisha mkoa
wote wa Ruvuma na wilaya ya Ludewa eneo ambalo lina ukubwa wa kilometa za mraba
72,630. Kati ya hizo km. za mraba 64,233 ni za mkoa wa Ruvuma na km. za mraba
8,397 ni za wilaya ya Ludewa.
Mapema, akitoa hotuba yake ya kwanza mara baada ya kusimikwa
rasmi, Askofu Mwenda alisema dayosisi mpya ya Ruvuma imezaliwa katika kipindi
chenye changamoto nyingi za kidunia na utandawazi ukiwemo mmomonyoko mkubwa wa
maadili.
Hata hivyo, akiainisha malengo ya dayosisi hiyo ambayo
anakuwa Askofu wake wa kwanza, Askofu Mwenda alisema mbali ya kufundisha neno
la Mungu, dayosisi hiyo itahimiza ufanyaji kazi ili wakazi wake wawe na akiba
ya chakula cha kutosha.
Alisema watashirikiana na Serikali na wadau wa ndani najje
katika kutoa huduma za kijamii hasa elimu na afya. Aidha alisema atakabiliana
na changamoto za sasa ambazo alizitaja kuwa ni mmomonyoko wa maadili, rushwa,
mauaji ya albino, unajisi wa watoto na ubakaji wa wanawake.
Akitoa shukrani kwa niaba ya waumini wa kanisa hilo, Askofu
Mkuu wa KKKT, Dk. Alex Malasusa alisema Kanisa lingependa kupata viongozi ambao
ni wacha Mungu. Akirejea mahubiri yake, Askofu Malasusa alisema inashangaza
kuona kuna baadhi ya watu wanagombea nafasi za uongozi lakini hawana mapenzi na
Mungu aliyewaumba watu anaotaka kuwaongoza.
“Bila kujali imani ya mtu, tunatamani tungepata kiongozi
ambaye anamcha Mungu. Awe anapenda kuhudhuria ibada. Awe anampenda Mungu ndipo
atawapenda watu anaowaongoza,” alisisitiza.
(mwisho)
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMAPILI, JULAI 27, 2014
No comments:
Post a Comment