Social Icons

IMETOSHA

IMETOSHA

Saturday, August 23, 2014

YANGA YAVAMIA KAMBI YA SIMBA UNGUJA

Wachezaji wa Simba wakifanya mazoezi kwenye Uwanja wa Chuoni Chukwani mjini Unguja jana Alhamisi kujiandaa na msimu mpya wa Ligi Kuu Bara. Picha na Mpiga Picha Wetu
SIMBA ipo Unguja chini ya Kocha Mzambia, Patrick Phiri, ikijipanga upya baada ya kupepesuka kwenye Ligi Kuu Bara msimu uliopita.
Wekundu wa Msimbazi hao wamekuwa wakifanya mazoezi kwenye Uwanja wa Chuo uliopo eneo la Chukwani pembeni kidogo ya mji wa Unguja.


Lakini huenda wakashituka na kupigwa butwaa kwani Yanga ambayo inaishi kizungu zaidi hapa Pemba, itahamishia kambi yao Unguja kuanzia kesho Jumamosi na Jumapili watashuhudia 'live' mechi ya kirafiki ya Simba na timu ya daraja la pili ya Kilimani City FC kwenye Uwanja wa Amaan.

Lakini hata Yanga na wenyewe wametangaza kwamba Jumapili watacheza hapohapo Unguja na KMKM ya Ligi Kuu Zanzibar. Kazi ipo.
Timu hizo zimekuwa zikikwepana kutokana na utani wa jadi ingawa kila moja ina hamu ya kusoma mbinu za mwenzake uwanjani.
Yanga ipo Pemba tangu Jumatatu iliyopita na kocha wake Marcio Maximo amesema: "Baada ya mazoezi ya kesho (leo Ijumaa), Jumamosi tutaondoka kwenda Unguja ambako pia tutakaa kwa siku tano tutakakocheza pia mechi za kujipima nguvu.
"Huku visiwani ni kutulia na mazoezi tu, hakuna mambo mengine yoyote tofauti na kama tungekaa Dar."
Ukifika hapa Pemba kuna chimbo moja hatari sana linaitwa Misali ni kama kilomita sita hivi kutoka mjini Chakechake kuna hoteli moja ya Kifahari inaitwa Pemba Misali Sunset Beach.
Sehemu kubwa ya majengo ya hoteli hiyo, imezungukwa na bahari hindi na miti mirefu inayofanya mahali hapo kuwa tulivu na kama utasikia kelele, basi lazima watakuwa ndege wa porini au mawimbi ya bahari.
Hapo ndipo Mwanaspoti ilipoikuta Yanga ikifanya maandalizi yao ya mwisho ya Ligi Kuu Bara na Kombe la Shirikisho Afrika. Mbali na yote kuna ufukwe mzuri ambao unampa nafasi kila mchezaji anayetaka kufanya mazoezi yake binafsi kujinafasi anavyotaka.
Maximo amesema kambi hiyo ni ya ushindi kwani inawafanya wachezaji wake watambue kwamba timu yao inaendeshwa kisasa na wao kazi yao ni kudhihirisha hilo uwanjani na amepata 'First 11' mbili za hatari.
Katika mahojiano na Mwanaspoti, Maximo amesema: "Timu ipo vizuri na kiwango cha kila mchezaji kinafanana hali imesababisha nipate vikosi viwili ambavyo ukivipambanisha na timu yoyote, nategemea kupata matokeo mazuri.
"Vikosi hivyo ndivyo nitakavyovichezesha katika mechi zangu za kirafiki nitakazocheza na itakapoanza ligi nitakuwa na timu yenye uwezo wa juu kabisa."
Yanga ilitarajia kucheza mechi ya kirafiki jana na Chipukizi ya Pemba baada ya hapo itakwenda Unguja na kucheza tena Jumapili dhidi ya KMKM inayofundishwa na kocha Ally Bushiri aliyewahi kufanya kazi na Maximo enzi za Mbrazili huyo Taifa Stars.
Baada ya mechi ya Jumapili, itaendelea na mazoezi hadi Jumatano ikapocheza Shangani kabla ya kirudi Dar es Salaam na kucheza na timu mbili kali za kimataifa.
"Nimezingatia mlolongo mzima wa mazoezi ya kisasa na kisayansi hatuna hata majeruhi isipokuwa Pato Ngonyani tu aliyegongana na mwenzake kwenye mazoezi na kusababisha maumivu kwenye enka ya mguu wa kushoto," alisema Maximo.
"Yanga inategemea mashabiki na ninachowaomba katika mechi hizo za kirafiki wafike kwa wingi kuja kuiona timu yao. Kikosi chao kwa sasa kipo tayari na mambo mengine ni marekebisho madogo madogo," alifafanua.
Katika kambi ya Yanga ulinzi ni mkali kupita kiasi kwani ukionekana hauelewekieleweki jirani na uwanja ambapo timu hiyo inafanya mazoezi lazima utafukuzwa kwani bado usiri unatakiwa.

Chanzo:Mwanaspoti

No comments:

Post a Comment