Vatican imempa kifungo cha nyumbani aliyekuwa balozi wake
katika jamuhuri ya Dominica Jozef Wesolowski.
Inaarifiwa hatua hiyo imechukuliwa dhidi ya balozi huyo wa
zamani kwa kosa la kuwadhalilisha watoto kijinsia.
Kasisi huyo wa zamani aliondolewa wadhifa wake mwezi Juni
baada ya jopo la viongozi wa kanisa kumpata na hatia ya kuwalawiti watoto
wavulana wakati akifanya kazi katika Jamuhuri ya Dominica.
Kesi yake itasikilizwa na mahakama ya uhalifu ya Vatican.
Itakuwa kesi ya kwanza kumhusisha afisa wa ngazi ya juu kusikilizwa katika
mahakama hiyo.
Wesolowski, ambaye asili yake ni kutoka Poland, alihudumu
kama balozi wa Papa katika jamuhuri hiyo kwa kipindi cha miaka mitano.
Msemaji wa Vatican, alisema kuwa kukamatwa kwa askofu huyo
ni mapenzi ya papa kwamba kesi kama hiyo inayozua hisia isikilizwe kwa haraka
bila kuchelewa.
Papa Francis ameahidi kufanya msako dhidi ya makasisi na
wafanyakazi wa Vatican, ambao huwadhulumu watoto wadogo akifananisha vitendo
vyao kama vya kishetani.
Mwaka jana aliweka sheria kali dhidi ya watuhumiwa wa
udhalilishaji wa watoto katika Vatican.
Msemaji wa Vatican, alisema kuwa uamuzi wa kumpa kifungo cha
nyumbani askofu huyo, badala ya kumzuilia katika kituo cha polisi, ulifikiwa
kutokana na afya yake.
Kesi ya Wesolowski inatarajiwa kusikilizwa baadaye mwaka
huu.


No comments:
Post a Comment