BAADA YA ndoto ya kuziunganisha pande mbili za katikati ya
jiji la Dar es Salaam na Kigamboni kwa daraja lenye umbali wa mita 680, Shirika
la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF), linaangalia uwezekano wa kujenga daraja la
kihistoria zaidi, litakalounganisha Dar es Salaam na Zanzibar.
Kwa sasa, uongozi wa shirika hilo upo katika mazungumzo na
wataalamu mbalimbali ili kuangalia uwezekano wa kujenga daraja hilo kutoka
bandari ya Dar es Salaam kwa upande wa Tanzania Bara na Unguja, kwa upande wa
Zanzibar.
Umbali kati ya Dar es Salaam na Zanzibar ni kilomita
74.43
sawa na meli 45.62 hivyo kuwepo kwa mradi huo ni jambo linalowezekana, kwani
kuna madaraja marefu zaidi duniani yanayounganisha upande mmoja wa bahari na
mwingine.
Kwa sasa, daraja refu zaidi duniani ni lile la
Danyang-Kunshan, lililopo nchini China, ambalo linaumbali wa kilomita 165, sawa
na meli 102.4. Daraja hilo lilifunguliwa mwezi wa Juni, mwaka 2011.
Hayo yameelezwa na Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Dk Ramadhan Dau
wakati alipokuwa akijibu swali la Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya
Maendeleo ya Jamii, Said Mtanda ambaye alitaka kufahamu, kama kuna matarajio ya
kujenga daraja kubwa zaidi, ikiwezekana kati ya Dar es Salaam na Zanzibar.
Akijibu swali hilo alisema wapo katika mazungumzo na
wataalamu mbalimbali ambapo mazungumzo hayo yakienda sawa, ujenzi wa daraja
hilo huenda isiwe ndoto, bali ukweli.
“Hilo wazo lipo mheshimiwa na tayari tumeshaanza mazungumzo
ya awali…kwa hivyo hilo wazo lipo na sisi tulilifikiria,” alisema Dk Dau.
Kamati hiyo ilifanya ziara katika miradi mikubwa mitatu ya
shirika hilo ambayo ni daraja la Kigamboni, ujenzi wa nyumba za Mtoni Kijichi
na ‘Dege-Eco village’ ambao una nyumba zaidi ya 7,000.
Akizungumza wakati wa kuhitimisha ziara hiyo, Mtanda alisema
kamati yake imeridhishwa na miradi ya NSSF ambayo inaendelea, huku akitaka
kuongezwa kwa kasi ili watanzania waanze kunufaika na miradi hiyo.
“Muangalie na hilo la ujenzi wa daraja la kutoka Dar es
Salaam hadi Zanzibar na mradi wa makazi bora na salama ambao utaweza kubadili
taswira ya jiji la Dar es Salaam,” alisema Mtanda.
Alisema kamati yake isingependa kuona changamoto zozote
ambazo zinaweza kukwamisha miradi hiyo na kwamba serikali kupitia Wizara ya
Ujenzi, itaangalia namna ya kuunganisha miundombinu karibu na miradi hiyo.
“Lakini pia tumesikia kuwa serikali inadaiwa na mifuko ya
hifadhi…tunashauri serikali kulipa mifuko hii ili kuifanya kuwa na nguvu na
kuweza kuleta maendeleo,” alisema Mtanda..
Chanzo: HABARILEO
No comments:
Post a Comment