Wakati Katiba inayopendekezwa ikikabidhiwa kesho kwa Rais
Jakaya Kikwete, Mwenyekiti wa iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji
Joseph Warioba amesema hata akialikwa katika sherehe hizo hatahudhuria kutokana
na majukumu aliyonayo kwa sasa.
Jaji Warioba alisema angependa kuhudhuria sherehe hiyo
ambayo pia itahudhuriwa na wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba, wakuu wa mikoa,
mabalozi na wageni mbalimbali, lakini kutokana na dharura aliyoipata
haitawezekana.
Sherehe hiyo itafanyika mkoani Dodoma kesho na
Mwenyekiti wa
lililokuwa Bunge Maalumu la Katiba, Samuel Sitta atakabidhi nakala ya Katiba
inayopendekezwa kwa Rais Kikwete na Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohammed Shein.
Katika hafla hiyo itakayofanyika kwenye Uwanja wa Jamhuri,
wajumbe wa Bunge hilo walioshiriki mchakato huo kuanzia mwanzo mpaka mwisho
watapewa vyeti.
Akizungumza na gazeti hili jana, Jaji Warioba alisema hadi
jana hakuwa amepata mwaliko lakini hata kama akipewa hataweza kuhudhuria.
“Siwezi kutoka nje ya Dar es Salaam kwa siku mbili tatu hizi kwa sababu nina
dharura. Kama wakinialika nitawaomba radhi kwamba sitaweza kuhudhuria,”
alisema.
Alipoulizwa iwapo Jaji Warioba ni miongoni mwa waalikwa
katika sherehe hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dk Rehema Nchimbi alisema angetoa
majibu leo kuhusu suala hilo lakini anaamini mkongwe huyo ni miongoni mwa
viongozi wastaafu, hivyo kualikwa ni lazima.
Wageni wengine walioalikwa ni pamoja na wakuu wa vyombo vya
ulinzi na usalama, viongozi wa dini na wengine wastaafu. “Hatuna uhakika na
viongozi wengine kutoka nje ya nchi maana mwaliko umetoka kwa muda mfupi,
lakini mabalozi waliopo nchini wote tumewaalika na makundi mengine yote kama
wakulima, wasanii, wavuvi, wafugaji na kila anayeguswa na Katiba mwakilishi
wake lazima atakuwapo,” alisema Dk Nchimbi.
Kuhusu orodha kamili ya waalikwa alisema: “Kesho (leo)
naweza kuwa na majibu mazuri kwa kila kitu maana tunashirikiana na vyombo
vingine katika kazi hii, kwa hiyo nitawaambia kwani vikao bado vinaendelea.”
Awali, Naibu Katibu wa lililokuwa Bunge la Katiba, Dk Thomas
Kashililah alisema maandalizi ya sherehe hiyo yamefanyika chini ya Ofisi ya
Waziri mkuu.
Mwananchi.
No comments:
Post a Comment