Social Icons

IMETOSHA

IMETOSHA

Wednesday, October 1, 2014

WALIODHURIKA KWA TOGWA SONGEA SASA WAFIKIA WATU 340

Idadi ya watu waliolazwa hospitalini kwa kunywa togwa inayosadikiwa kuwa na sumu katika Kijiji cha Litapwasi, Kata ya Mpitimbi mkoani Ruvuma imeongezeka kutoka 270 hadi 340.Tukio hilo lilitokea Jumapili baada ya watu kushiriki sherehe ya Kipaimara ambako walikula, kunywa pombe na togwa na baadaye wale waliokunywa togwa walianza kuumwa matumbo, kuhara na kutapika.Hadi jana, watu 102 walikuwa bado wamelazwa katika Zahanati ya Lyangweni, Hospitali ya St. Joseph Peramiho na 


Hospitali ya Mkoa wa Ruvuma.Tayari watu watano wanashikiliwa na Polisi kwa upelelezi kuhusiana na tukio hilo, akiwamo Baba Mzazi wa mtoto Dickson aliyepata kipaimara, Enes Nungu (47).
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ruvuma, Mihayo Mskhiela aliwataja watu wengine wanaoshikiliwa katika Kituo Kikuu cha Polisi Songea kwa mahojiano kuwa ni Benedict Nungu (76), Esebius Komba (36), Sadiki Masodi (65) na John Kaulangudidi. Mtu anayedaiwa kukabidhiwa ufunguo chumba cha vinywaji kabla ya kugawiwa kwa wananchi, Ridhiwani Shawa haijulikani alipo.
Mabaki ya chakula, togwa na pombe ya kienyeji vilichukuliwa juzi na kupelekwa kwa Mkemia Mkuu wa Serikali kwa uchunguzi.
Kamanda Mskhiela alitoa wito kwa wananchi wanaoandaa sherehe kuhakikisha wanafanya hivyo katika mazingira mazuri na yenye usalama ili kuepuka athari kama hizo.
Mganga Mkuu wa Hospitali ya Peramiho, Dk Vanace Mushi alisema hadi jana, watu waliokuwa wamelazwa katika hospitali hiyo walikuwa 34 na hakukuwa na mgonjwa aliyeruhusiwa kurudi nyumbani.
Kaimu Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Mkoa wa Ruvuma, Majuto Mlawa alisema wagonjwa tisa wa rufaa walipokewa na kupatiwa matibabu huku hali zao zikiwa mbaya.
Akizungumzia tukio hilo, Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Said Mwambungu alisema: “Jambo hili limenisikitisha sana, nimeumizwa sana nawapa pole wote waliopatwa na tatizo hilo naamini Mwenyezi Mungu atawasaidia na watapona na kurejea katika hali zao za kawaida.”

Hata hivyo, Mwambungu alisema hiyo ni ajali kama nyingine, hivyo anaviachia vyombo vya usalama na wataalamu wa afya kupata ukweli. Pia aliwataka wananchi kuwa makini pindi wanapoandaa vyakula na pombe za kienyeji katika sherehe mbalimbali.

No comments:

Post a Comment