Jicho kama kiuongo cha mwili linaona mbali, linakufanya
kuweza kuangalia na kumulika biashara yako, uwezo kupata hali halisi na kufanya
mabadiliko. Watu wengi Tanzania hususani wafanyabiashara wanafanya biashara
kiholela bila kufuata utaratibu wa kisheria
au kufanya biashara kwenye taasisi inayokubalika na inayotambulika
kisheria, kuna umuhimu mkubwa sana wa mfanyabiashara au mtoa huduma yoyote kuwa
katika taasisi inayoeleweka kisheria na kutambulika bila kujali aina au ukubwa
wa biashara husika.
Katika makala ya leo, JICHO LA BIASHARA limemulika kwenye
usajili wa makampuni, Kampuni ni muunganiko wa watu zaidi ya mmoja walisajiliwa
kisheria wenge lengo mmoja. Kampuni kisheria inatambulika kama mtu mwingine
ambaye hausiani na wanahisa au washirika.
SHERIA
Usajili wa uendeshwaji wa kampuni unasimamiwa na sheria
nyingi, Sheria kuu ni Sheria ya Makampuni sura ya 212, pia sheria nyingine ni
sheria ya kodi,
sheria ya viwango, Sheria ya Leseni, na sheria zingine zote za
nchi ikiwa ni pamoja na katiba ya jamhuri ya muungano wa Tanzania ya mwaka
1977.
AINA ZA MAKAMPUNI,
Makampuni unaweza kuyatofautisha kulingana na mambo
mbalimbali, unaweza kuyatofautisha kwa utaifa, uwepo wa hisa, umiliki au uwepo
wa ukomo. Kisheria kuna makampuni ya aina mbalimbali, tukianza kwa kuangalia
utaifa.
Tuna makampuni ya kigeni (Foreign Companies) , haya kimsingi
yameundwa nchi za nje na hapa yamesajiliwa pia na yanamilikiwa kwa asilimia
kubwa na wageni, kuna makampuni ya wazawa (Local Companies) Haya ni makampuni
yaliyosajiliwa nchini na yanamilikiwa kwa asilimia kubwa na wazawa.
Pia kuna makampuni yenye ukomo wa hisa na yasiyo na ukomo wa
hisa, Makampuni yenye ukomo wa hisa (Companies limited by Shares) Kimsingi ni
makampuni ambayo yana malengo ya kibiashara, pia wanahisa wake wanatakiwa
kuchangia endapo kampuni ikifirisiki kiasi kile ambacho hawajalipia kwenye hisa
zao. Makampuni yasiyo na ukomo wa hisa (Companies limited by Guarantee) ni
makampuni yasiyo na mlengo wa kufanya biashara, yenyewe yanategemea fedha
kutoka kwa wa hisani, mara nyingine yana sura ya Taasisi zisizo za kiserikali
(NGO’S) washirika(Members) kama kampuni itafirisika watachangia kile walicho
ahidi kwenye katiba za makampuni husika mfano LHRC (Legal and Human Right
Center).
Makampuni mengine ni kutokana na umiliki, hapa tuna
makampuni ya umma (Public companies) haya ni makampuni ambayo wanahisa wake ni
wengi sana, na kampuni inauwezo wa kuuza hisa zake kwa umma wote wa Tanzania,
Haya ni makampuni ambayo hisa zake zinauzwa kwenye soko la hisa na haina ukomo
wa idadi ya wanahisa lakini lazima waanzie wawili. Aina nyingine ni makampuni binafsi (private companies) haya ni
makampuni ya watu wachache ambao hisa zao haziuzwi kwenye soko la hisa, na
uuzaji wake wa hisa sio rahisi sana, mara nyingi wahusika wenyewe hununua
kwanza kabla ya kumuuzia mgeni lakini pia idadi ya wanahisa ya chini ni lazima
wawe watu wawili, kwa idadi ya kwenda juu lazima wasiwe zaidi ya hamsini.
Pia kuna makampuni yenye ukomo (Limited Companies) ambayo
haya makampuni kipindi cha kufirisika au yanapokufa mtu anapaswa kuchangia kile
ambapo hakulipia kwenye hisa ( limited
to unpaid up shares) au kile ambacho amekubali kuchangia. Makampuni mengine ni
makampuni yasiyo na ukomo (Unlimited Companies) haya ni makampuni ambayo wakati
wa kufirisika au kufa mtu anapaswa kulipa madeni yote ya kampuni, hata mali
binafsi zinaweza kuchukuliwa.
Nimeeleza aina za makampuni ili ndugu msomaji uelewe kuwa
kuna aina mbalimbali za makampuni hapa Tanzania kwa mujibu wa sheria yetu ya
makampuni sura ya 212.
Watu wengi wanafikiri kuwa na kampuni ni lazima uwe na fedha
nyingi sana au biashara yako iwe kubwa sana sio kweli, acha uoga. Hata hao
wenye makampuni makubwa hawakuanza na makampuni makubwa, walianza na wazo kama
lako baadae wakasajili kampuni, ikawa kampuni mpya ndo baadae ikaanza kukua.
Uoga ni dhambi na uoga ni umaskini thubutu na fungua kampuni yako isimamie
pambana nayo baadae hata ukifariki watoto watajua baba au mama alifanya kitu.
Mtu akifariki kampuni haifa, kampuni inadumu milele na milele labda ifirisike.
JINSI YA KUSAJILI KAMPUNI
Kuna hatua kadhaa za kupitia ili kufanya usajili wa kampuni,
hatua hizo ni zifuatazo;
Moja, Uchunguzi wa jina, hapa mtu mwenye nia ya kusajili
kampuni au kwa kupitia wakili huandika barua na kutaka majina pendekezwa
yaangaliwe kama yanafaa kwa maadili ya kitanzania na haya fanani na kampuni nyingine
yoyote. Hapo barua hupelekwa kwa msajili baada ya siku mbili au tatu utaambiwa
kama jina limepita au hapana.
Kuandaa katiba na kanuni za kampuni (memorandum and articles
of association ) hii huandaliwa kitaalamu na wanasheria, inaeleza kazi, malengo,
majukumu, mgawanyo wa hisa,mwenendo na jinsi ya kuendesha kampuni. Katiba na
kanuni zinapaswa kuandikwa kisheria ikiwa kinyume na sheria kampuni haita
sajiliwa.
Kujaza fomu namba 14A, baada ya kuandaa katiba, inajazwa
fomu namba 14A ambayo kimsingi inajazwa kitaalamu ikielezea mahali ofisi ya
kampuni itakuwa, wakurugenzi na anwani zao, tarehe zao za kuzaliwa lengo ni
kuwa mkurugenzi lazima awe na miaka zaidi ya 21, pia utaifa wao ili kujua
utaifa wa kampuni. Ikikosewa kujazwa vizuri kampuni haitasajiliwa.
Kujaza fomu namba 14B, hii ni fomu ya kiapo kwamba mtu
aliyehusika kusajili kampuni hii amefuata utaratibu wote wa kisheria, hii fomu
lazima kiapo chake kiwe mbele ya wakili au kamishina yoyote wa viapo, hii ni
kwa mujibu wa kifungu cha 14 cha Sheria ya Makampuni Sura ya 212.
Baada ya kuandaa nyaraka husika basi nyaraka hizo
huwasilishwa kwa msajili wa makampuni na
kulipa gharama kwa kulingana na mtaji wa kampuni na aina ya kampuni,
Baada ya siku kadhaa mhusika au kupitia wakili huenda
kuchukua cheti cha usajili wa kampuni yako, , basi baada ya hapo mtu huwa na
kampuni yake na kuanza taratibu zingine, kama kuchukua leseni na vibali
mbalimbali kulingana na aina ya biashara yake.
SIFA ZA KAMPUNI
Kampuni ina sifa kadhaa tofauti na taasisi nyingine, sifa
hizo ni kama zifuatazo;
Moja, kampuni kisheria ni mtu tofauti kabisa na wanahisa au
washirika wake, maana yake ina sifa za mtu ndani yake (legal personallity ) ina
maana kampuni inauwezo wa kufanya shughuli zote za kibiashara kwa jina lake
yenyewe, wakurugenzi ni ubongo wa kampuni lakini wao sio kampuni.
Kampuni inaweza kuingia kwenye mkataba kwa jina lake
yenyewe, kwa kuwa ina sifa kama mtu, basi inaweza kuingia kwenye mkataba kwa
kutumia mhuri wa moto (Common seal) au kupitia wakurugenzi kwa niaba ya
kampuni.
Kampuni inaweza kushitaki au kushitakiwa, kampuni inaweza
kufungua kesi na kushitaki au kusishitakiwa kwa lolote itakayofanya katika
shughuli zake.
Kampuni ina dumu milele (perpetual succession), pia kampuni
ina sifa ya kudumu, yani wanahisa au walioifungua na kuisajili wakifariki
kampuni yenyewe haifi, inaendelea kudumu ina utaratibu wake wa kufa au
kufirisika.
Lakini sheria inazuia watu kusajili kampuni kwa nia ya kuiba
au kukwepa kodi au kudhurumu, makama haitaweza kuvumilia watu kufanya uhuni kwa
kupitia kampuni. Mahakama au Sheria inaweza kutoa kivuli cha kampuni na mtu
kushitakiwa binafsi (Lift the corporate vail).
FAIDA ZA KUWA NA KAMPUNI
Kuna faida nyingi sana za kuwa na kampuni, kisheria,
kiuchumi na kijamii, kwanza mtu mwenye kampuni yake, jamii ina mheshimu sana na
anaonekana ni mtu makini sana hata kama atakuwa hajasoma kabisa. Faida za kuwa
na kampuni ni hizi zifuatazo,
Moja utaongeza uwezo wako wa kibiashara kitaifa na
kimataifa, watu wengi sana kwa sasa wanapenda kufanyakazi na makampuni na sio
mtu binafsi, kuna kazi nyingi unaweza kukosa kwa kuwa hauna kampuni, kampuni
inaweza ikawa ya kufanya usafi, kuuza na kununua biadhaa, kampuni ya kilimo,
kampuni ya uvuvi, ulinzi, kukusanya madeni, kutoa huduma ya hospitali,
michezo,mtandao,shule, mawasaliniano n.k
Ukiwa na kampuni ni rahisi kupata zabuni za aina mbalimbali
(Tender), ukipitia magazeti mbalimbali zabuni wanataka mtu ambaye yupo na
kampuni sio mtu binafsi, watu wanaamini ni salama zaidi kufanya kazi na kampuni
na sio mtu binafsi,unapaswa kwenda na wakati.
Lakini pia kampuni inakufanya uweze kufanya biashara kwa
uhuru zaidi na kuheshimika sana, ndani na nje ya nchi.
Ukiwa na kampuni, hata kama kampuni ikiyumba sio lazima na
wewe utayumba, zitayumba mali za kampuni sio zako binafsi, kama kuna hasara
mnagawana wanahisa wote, kwa hiyo unaweza kupata hasara kidogo.
Ukiwa na kampuni ni rahisi kukopesheka kwa mabenki na
taasisi mablimbali za kifedha, kampuni inaweza kutoa na kupokea mkopo.
Ni watanzania tu, ambao bado akili haijafunguka na kutambua
fursa mbalimbali ukiwa na kampuni, ni muda muafaka wa kufikilia kuwa na kampuni
yako inayojitegemea kwa kulingana na biashara yako au huduma yako.
Mwandishi wa Makala hii ni Jebra Kambole Wakili wa
Kujitegemea kutoka Kampuni ya Law Guards Advocates wa Jijini Dar-es-salaam.
JICHO LA BIASHARA kwa maswali na maoni 0717334032 Email jebrakambole@gmail.com
No comments:
Post a Comment