Jaji Mkuu, Mohamed Chande Othman
Jaji Mkuu, Mohamed Chande Othman alisema jana mahakama
inajifunza kutoka kwa nchi zinazoruhusu vituo vya redio na televisheni kurekodi
na kuripoti habari wakati kesi zinaendelea.
Alisema hayo alipozungumza na waandishi wa habari jana
wakati wa mkutano baina ya Baraza la Vyombo vya Habari na Mahakama uliofanyika
jijini Dar es Salaam.
Alisema utaratibu huo utaanza kwa kuripoti kesi za madai
zenye mvuto kwa jamii na kwamba utaratibu mzima unapaswa kufanyika kwa umakini
mkubwa baada ya mahakama na vyombo vya habari kukaa pamoja na kujadiliana juu
ya maadili, uhuru na mipaka ya mhimili wa mahakama na vyombo vya habari ili
kuondoa migongano katika kuandika na kuripoti habari za mahakama kwa kutumia
teknolojia ya kisasa.
Badala yake, wanaruhusiwa kuandika habari hizo kisha
kuripoti kile walichoandika bila kuonesha mwenendo mzima wa kesi kwa kutumia
sauti na picha za video.
Jaji Othman alifafanua kuwa ni lazima mahakama na vyombo vya
habari kuweka utaratibu wa kuripoti kesi kwa kurusha sauti na picha bila
kuvuruga mwenendo wa kesi kwa kukiuka haki hasa za washitakiwa, waathirika na
mashahidi kwa kuwa wote wanahitaji haki sawa katika kupata ulinzi na hifadhi
kulinda utu wao.
“Mfano sio haki kuwaonesha hadharani waathirika wa kesi ya
ubakaji, pia mshitakiwa yeyote hawezi kuitwa mwizi au muuaji hadi mwisho wa
kesi ambapo mahakama inazingatia ushahidi na kutoa hukumu,” alisema.
Aliendelea kusema, “Ukitangaza kuwa mtu ni mwizi kabla ya
hukumu, ni kumkosea haki kisheria hivyo ni lazima tuangalie yote hayo kabla ya
kuruhusu utaratibu wa kunakili sauti na picha wakati kesi zinaendelea.”
Jaji alitoa maelezo hayo wakati wa kuzungumzia mapendekezo
yaliyotolewa na Katibu Mtendaji wa Baraza la Habari Tanzania (MCT), Kajubi
Mukajanga ambaye alisema ili kuboresha uhusiano wa vyombo vya habari na
mahakama, mahakama inapaswa kuwa na msemaji.
Mukajanga alipendekeza pia mahakama kuandaa taarifa kwa
kutumia sauti na picha za video kuhusu mwenendo wa kesi, kutoa mwongozo wa
kutumia simu za viganjani na vifaa vingine vya mawasiliano kwa njia ya
digitali.
Baraza hilo la kihistoria kati ya mhimili wa Mahakama na
vyombo vya habari, limeazimia kuimarisha ushirikiano na kufanya kazi kwa pamoja
kwa kuheshimu uhuru na mipaka ya kila mmoja na kuzingatia kuwa wote wanafanya
kazi ya kutetea haki za wananchi na wote wamekuwa kimbilio la
wanyonge.HABARILEO
No comments:
Post a Comment