Musoma. Mwanamke mmoja mkazi wa Kata ya Buhare, Manispaa ya
Musoma mkoani Mara, Helena Paulo (20), amejifungua watoto pacha wa kike
walioungana eneo la kifuani hadi tumboni wakiwa na uzito wa kilo 4.6 kwa
pamoja. Tukio hilo la ajabu katika Mji wa Musoma na mkoa kwa jumla, liliwavutia
hisia za wananchi hali iliyosababisha msongamano katika Hospitali ya Rufaa ya
Mkoa kwa madhumuni
ya kutaka kushuhudia.
Akizungumza katika wodi ya wazazi hospitalini hapo, muuguzi
wa zamu, Naabu Geraruma alisema mwanamke huyo alijifungua juzi saa saba usiku
kwa njia ya upasuaji. Geraruma alisema tukio hilo ni la kwanza katika hospitali
hiyo na hali ya afya ya mzazi huyo na watoto inaendelea vizuri na muda wowote
atahamishiwa Hospitali ya Rufaa ya Bugando, Mwanza.
Kwa upande wake, Mganga wa Idara ya Magonjwa ya Wanawake, Dk
Simon Kamuli alisema baada ya jitihada za kuhakikisha mwanamke huyo anajifungua
salama kukamilika, kinachofuatia ni kupelekwa Hospitali ya Rufaa ya Bugando kwa
uangalizi zaidi.
Alisema kuwa hospitali ya mkoa haina uwezo wa kuwafanya
chochote watoto hao, ikiwamo kuwatenganisha na taratibu zingine kabla ya
uchunguzi wa kina.-MWA
No comments:
Post a Comment