Sheikh Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, Alhad Mussa Salum.
Stori: Gabriel Ng’osha BAADHI
ya viongozi wa dini jijini Dar es Salaam, wametoa neno juu ya vurugu
zilizofanywa wiki iliyopita na vijana wanaosadikika kuunda kundi
linalojulikana kama Panya Road, Risasi Jumatano lina habari kamili.Sheikh Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, Alhad Mussa, aliliambia gazeti hili kuwa ukosefu wa ajira ni sehemu mojawapo inayozalisha makundi ya ajabu, hivyo serikali inapaswa kujipanga na kutengeneza mifumo ya ajira kwa vijana ili kuwaepusha kujiingiza katika makundi tishio na hatari.
“Hawa wanavamia, kupora na kuumiza watu ovyoovyo. Hata katibu mkuu wa mkoa wa Dar naye
ni mhanga, alipotelewa na simu yake katika harakati za kuwakwepa hao wahuni, ukosefu wa ajira kwa vijana ni bomu kubwa na baya sana zaidi hata ya al shabbabi.”
Mchungaji Efrahimu Mwansasu wa Kanisa la Hosana Life Mission.
Kwa upande wake, Mchungaji Ifrahimu Mwansasu wa Kanisa la Hosana Life
Mission, alisema makundi hayo yanasababishwa na malezi mabaya ya
kiimani na kitabia, kitu alichokiri hata yeye kuwahi kupitia akiwa
kijana kabla ya kuokoka na kuitaka serikali ikae nao na kujua sababu ya
wao kuwa kama walivyo.“Yawezekana vijana wameingia bila kupenda kwa msukumo wa madawa ya kulevya, ugumu wa maisha na kadhalika, ila naamini katika roho wa kweli kwa Mungu kila kitu kinawezekana.”
Kundi la Panya Road, mwishoni mwa wiki iliyopita lilizua tafrani kubwa jijini Dar es Salaam baada ya kuwavamia, kuwapora na kuwajeruhi watu katika maeneo mbalimbali, lakini Jeshi la Polisi chini ya Kamanda Suleiman Kova lilifanikiwa kuwadhibiti.
No comments:
Post a Comment