Mbunge wa Bukoba Mjini kwa tiketi ya CCM, Khamis Kagasheki
amemtuhumu Waziri Mkuu Mizengo Pinda kuwa ndiye aliyekuza mgogoro wa
Bukoba uliosababisha madiwani wa halmashauri kushindwa kufanya vikao,
akidai kuwa mtendaji huyo mkuu wa Serikali ameshindwa kuchukua hatua.
Pinda hakuweza kupatikana, lakini msemaji wake alisema Waziri Mkuu
ameshalishughulikia suala hilo kwa kiasi kikubwa.
Tuhuma hizo za Kagasheki ni za nadra kwa mbunge
huyo wa chama hicho tawala kuelekeza kwa mtendaji mkuu wa Serikali na
mmoja wa wajumbe wa vikao
vya juu vya CCM.
vya juu vya CCM.
Kagasheki, ambaye alikuwa Waziri wa Maliasili na
Utalii, alitoa tuhumu hizo wakati wa mahojiano maalumu na gazeti hili
wiki iliyopita, akisisitiza kuwa ni makosa kuutazama mgogoro huo kuwa ni
kati ya yake na meya na akataka ijulikane kuwa kinachoendelea Bukoba ni
suala la wizi.
Mgogoro huo wa kisiasa, ambao umedumu kwa takriban
miaka miwili na unaotishia kugawanyika kwa CCM, umekolezwa na
kufunguliwa kwa kesi tatu ambazo zimezuia utekelezaji wa shughuli za
maendeleo na umekuwa ukihusishwa na vita vya ubunge baina ya Kagasheki
na Meya wa Manispaa ya Bukoba, Anatory Amani.
“Hii ni mara yangu ya kwanza kupata nafasi ya
kuzungumzia suala hili. Hakuna unafiki hapa, hili nitalisimamia mahali
popote na nitalisema mahali popote kuwa Pinda, ndiye tatizo katika
mgogoro huu ulioinyima Bukoba maendeleo,” alisema Kagasheki.
“Lakini hiyo hainizuii kusema kuwa Tamisemi ndiyo
tatizo, ingawa waziri wake ni Hawa Ghasia. Pinda ndiye msimamizi na
bungeni alisema Amani siyo meya tena, lakini hakuna lililofanyika hadi
leo na wananchi wanakosa maendeleo,” aliongeza akirejea kauli ya Pinda
bungeni kuwa meya huyo alijiuzulu halafu siku chache baadaye Amani
akaibuka na kukanusha habari za kuachia kiti cha umeya.
Alisema kuwa awali wakati mgogoro huo unafukuta,
uongozi wa juu CCM uliagiza Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Fedha za
Serikali (CAG) kwenda Bukoba, naye akaenda kufanya utafiti, akamaliza na
akatoa kila kitu.
Kagasheki alieleza: “ Nilikwenda katika kikao cha
CCM, Pinda yupo ndani ya chama, kikaagiza madai hayo yafanyiwe kazi,
lakini mpaka leo Takukuru hawajafanya chochote. Ndiyo maana nasema,
Pinda akija kuomba kura (za urais) Bukoba, pale mjini, hali ni ngumu
kwelikweli, atapata shida sana.
“Huu siyo mgogoro, ni wizi wa fedha na ripoti ya
CAG ipo wazi lakini wahusika walio chini ya Waziri Mkuu hawataki
kuifanyia kazi…Jambo hili lisipofanyiwa kazi, lazima itakuwa ajenda
katika Uchaguzi Mkuu.”
Mbunge huyo wa Bukoba Mjini alisisitiza akisema:
“Unajua kuna vitu vinaumiza, maana vile siyo vitu vyangu ni taarifa ya
CAG na kwa kweli huyu CAG aliyeondoka ungekuwa unamuuliza ukweli,
angekwambia amegundua mambo mengi ndani ya Serikali ambavyo hayafanyiwi
kazi. Wizi usio na kifani, upotevu wa fedha na jambo zuri ni kuwa ile
kazi aliyokuwa akafanya CAG ipo kikatiba.”
Alisema kuwa CCM ilitoa maelekezo na kupitia
Serikali ikayapeleka Tamisemi, lakini hadi sasa hakuna pendekezo hata
moja la CCM wala CAG lililofanyiwa kazi, lakini Waziri Mkuu yupo kimya.
“Tunapozungumzia Tamisemi, tunazungumzia Waziri
Mkuu, bahati nzuri yeye pia ni mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM. Uamuzi wa
Kamati Kuu, Pinda hakufanya hata moja na hapo ndipo mgogoro ukapamba
moto,” alidai
- Mwananchi
No comments:
Post a Comment