BARAZA la Maadili ya Viongozi wa Umma, limemsomea rasmi
mashitaka aliyekuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa
Anna Tibaijuka (pichani), na kubainisha kuwa kiongozi huyo anastahili kujibu
mashitaka kwa kosa la kuomba na kujipatia fedha kinyume na Sheria ya Maadili ya
Viongozi wa Umma.
Hata hivyo, Profesa Tibaijuka alikana mashitaka hayo, na
kusisitiza kuwa hakukiuka maadili hayo ya viongozi wa umma, kwa kuwa fedha hizo
hakuziomba kwa maslahi yake binafsi, bali kwa ajili ya kuendeleza na kuboresha
taasisi yake inayotoa huduma ya elimu kwa
watoto wa kike wasio na uwezo lakini
wenye vipaji.
Akimsomea mashitaka hayo mbele ya baraza hilo, Mwanasheria
wa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Wemaeli Mtei alisema Profesa
Tibaijuka ambaye ni kiongozi wa umma, alishawishi na kuomba fedha na baadaye
kupokea Sh bilioni 1.6 kutoka kwa James Rugemalira na mkewe.
Aidha, Sekretarieti hiyo kupitia shahidi wake ambaye ni
Katibu Msaidizi wa Idara ya Viongozi wa Siasa kutoka Sekretarieti hiyo, Waziri
Kipacha, alisema kupitia Kamati ya Uchunguzi iliyoundwa na sekretarieti
kufuatilia sakata hilo, ilibaini kiongozi huyo aliomba na kupokea fedha hizo
kupitia barua aliyoandika Februari 4, mwaka 2012.
“Tulibaini kuwa fedha alizoomba mlalamikiwa zilitumwa kwake
kupitia akaunti yake namba 00120102640201 ya Benki ya Mkombozi iliyopo St
Joseph jijini Dar es Salaam,” alisema huku akikabidhi baraza hilo barua hiyo ya
Tibaijuka ya kuomba fedha na taarifa za kibenki kama ushahidi.
Alisema pamoja na hayo, kamati hiyo pia katika uchunguzi
wake ilibaini mlalamikiwa ni mmoja wa wadhamini katika Bodi ya Wadhamini ya
Taasisi ya Barbro Johansson Girls Education Trust, ambapo barua kutoka Wakala
wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA), ilithibitisha suala hilo. Na kwamba
wamiliki wa shule hiyo ndiyo wadhamini.
“Tumebaini kuwa mlalamikiwa alipokea kiasi hicho cha fedha
na wadhifa aliokuwa nao kama Waziri, jambo lililomwingiza katika mgongano wa
kimaslahi,” alisema.
Alisema kitendo cha mlalamikiwa kupokea fedha hizo na
kuingizwa katika akaunti yake binafsi, ni kosa kwa mujibu wa masharti ya
maadili ya viongozi wa umma kwa kuwa viongozi wa umma hawaruhusiwi kuomba fedha
au msaada au kujipatia maslahi ya kiuchumi au kumpatia mtu mwingine maslahi
hayo ya kiuchumi.
Wakili wa Tibaijuka, Dk Rugemeleza Nshara, alidai mbele ya
Baraza mteja wake hakuna kosa alilofanya, bali alitumia wadhifa alionao kama
viongozi wengine akiwemo Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, kuomba na kuchangisha
fedha kwa ajili ya maendeleo ya wananchi na si binafsi.
“Nataka kuuliza Baraza hili, ina maana juzi Waziri Mkuu,
alivyoongoza uchangishaji fedha kwa ajili ya maendeleo alikwenda kinyume na
maadili ya uongozi?,” alihoji. Profesa Tibaijuka, alikiri kuomba fedha hizo kwa
ajili ya kuendeleza taasisi hiyo yenye lengo la kujenga shule za mfano za
wasichana wenyewe vipaji kila kanda ili kukuza na kuimarisha elimu ya mtoto wa
kike nchini.
“Huu si msaada wa kwanza, tumekuwa tukifadhiliwa na Serikali
ya Sweden kupitia msaada tuliopatiwa na Rais mstaafu, Benjamin Mkapa, ambaye
alitambua juhudi zetu na kutuunga mkono, tumechangiwa na taasisi za ndani na
nje na watu binafsi, kiasi kinachohitajika kuboresha shule hizi ni dola za
Marekani milioni 14 sawa na takribani Shilingi bilioni 25.2,” alisema.
Alisema pamoja na Rugemalira aliyetoa Sh bilioni 1.6, pia
mfanyabiashara maarufu nchini, Reginald Mengi alichangia taasisi hiyo Sh
milioni 278, ikiwemo Serikali ya Sweden iliyomaliza mkataba wake iliyochangia
Sh bilioni 8.1.
“Sisi tuliopo kwenye taasisi hii, tunaaminiana na ni
waadilifu ndiyo maana fedha nilizoomba ziliingizwa kweli kwenye akaunti yangu
lakini niliziwasilisha, zilizobaki ni deni nililokuwa naidai taasisi, lakini
pia nimekopa Benki M Sh bilioni mbili kwa ajili ya kuboresha taasisi hii na
kuweka dhamana nyumba yangu iliyopo Oysterbay. Mbona hili hamlioni?,” alihoji.
Wakati akijitetea, Tibaijuka aliomba akabidhi andiko lake
mbele ya baraza hilo. “Nina andiko langu na naomba nilikabidhi, kabla hujafa
hujaumbika, nasimama hapa leo kwa sababu tayari nimeshahukumiwa bila
kusikilizwa, niliomba hata bungeni nipewe nafasi lakini nilihukumiwa kama
Waziri nikavuliwa madaraka, nashangaa leo nimesimamishwa hapa kama mbunge,”
alisema.
Alisema “mimi mpaka sasa nasema sijakiuka maadili labda
wanasheria wanieleweshe kwa sababu nilisimama kama mimi wakati wa kuomba fedha
na si kama waziri au mbunge, hivyo sasa naona lengo ni kunivunja moyo,
kunidhalilisha, kunifanya kama mwanamke mhuni na tapeli.” Aliendelea kujitetea,
“nimekuja kujieleza ila..
Mimi siyo mwanasheria ila ukweli sina kosa na ndiyo maana
nyaraka zote ambazo zipo hapa, mimi ndo nimewapa, nimekuja hapa kwa nia njema
na naamini kwamba Baraza hili litanisikiliza kwa sababu ukweli ndiyo mwanzo wa
maadili, lazima tupiganie haki na tupiganie ukweli.
“Kama mimi nimefanya kosa kusimama kuwasaidia watoto wenye
vipaji ni kosa, naomba mwanasheria anieleweshe na naomba ukweli usimame maana
tukienda na fitina peke yake, hatutafika. Mimi ni profesa na mchumi na ni
mstaafu wa muda mrefu na nina pensheni, sina makuu, maisha yangu ni ‘simple’
(ya kawaida) huwezi kunikuta Dubai... Ila nipo tunafanya maendeleo na wananchi
wangu,” alisema.
Hata hivyo alisema fedha anazodaiwa kuhamisha baada ya
kupokea na kukatwa za kulipa deni la Benki M, zilizobaki zilikuwa ni halali
yake kwa kuwa alikuwa akidai shule hivyo fedha hizo zilizobaki ni kwa ajili ya
matumizi yake binafsi. “Mimi ni mchakarikaji, mtafuta fedha na kiongozi
anayeshindwa kutafuta fedha kwa ajili ya watu wake hafai.
Hivyo nilipolipwa milioni 117 (Shilingi), nilitoa milioni
mbili nikachangia Kanisa la Makongo na nikatoa laki nne nikapeleka kanisani na
milioni 10 niliitoa kwa ajili ya matumizi yangu ya kununulia mboga, “ alisema.
Shahidi wa Profesa Tibaijuka ambaye ni Mjumbe wa Bodi ya Wadhamini wa Taasisi
hiyo, Balozi Paul Rupia katika ushahidi wake mbele ya Baraza, alisema fedha
hizo zimetafutwa na Profesa Tibaijuka.
Alisema aliitaarifu bodi kwamba zipo fedha zimeingia katika
akaunti yake na zinatakiwa kulipa madeni wanayodaiwa. Alisema katika kikao
hicho cha kutoa uamuzi wa kugawanywa kwa fedha hizo kilichofanyika Luguruni ,
hakuhudhuria, ingawa alikuwa na taarifa zote za kinachoendelea.
Rupia alisema bodi hiyo haikumpa masharti yoyote Profesa
Tibaijuka ya kumaliza kulipa madeni hayo kwa sababu hawakuona sababu ya
kumfuatilia kwa kuwa walimwamini, kutokana na juhudi zake binafsi za kupata
fedha hizo. Shauri hilo lilianza saa 3 na baadaye kuahirishwa kwa muda hadi saa
6.30 mchana, lilipoanza kusikilizwa tena na kumalizika saa 11.45 jioni.
Katika shauri hilo, Profesa Tibaijuka alitoa ushahidi kwa
zaidi ya saa tatu, akilalamika kuonewa na kuhukumiwa bila kusikilizwa. Shauri
hilo liliahirishwa hadi Machi 13 mwaka huu, kutokana na muda kutotosha. Wakili
aliomba udhuru wa kwenda Marekani kwa siku 10 na Jaji Msumi alikubali.
Jaji Msumi alisema wajumbe watapitia shauri hilo na siku
hiyo itaamuliwa, endapo hukumu itatolewa wazi au kwa uamuzi wa ndani.
No comments:
Post a Comment