...Akipanda gari lake kuondoka katika ukumbi wa Karimjee
jijini Dar es Salaam.
ALIYEKUWA Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Mwenyekiti wa
Kamati ya Uandishi katika Bunge Maalum la Katiba (BMK) Andrew Chenge amekataa
kuhojiwa mbele ya Baraza la Sekretarieti ya Maadili ya viongozi wa umma juu ya
tuhuma za kunufaika na fedha zilizotoka katika akaunti ya Tegeta Escrow, wakati
alipoitika wito katika ukumbi wa Karimjee jijini Dar es Salaam leo.
Chenge alitajwa kuwa mmoja wa watu waliopewa fedha na
Mkurugenzi wa kampuni ya PAP, James Rugemalila, zilizotolewa katika akaunti
hiyo ya umma ambayo ilikuwa ikihifadhi hela za Tanesco na IPTL, kiasi cha
shilingi bilioni 1.6, kitendo kilichosababisha kuondolewa katika nafasi ya
Uenyekiti wa Kamati ya Bajeti katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Lakini baada ya kufika mbele ya kikao cha Baraza hilo,
kilichokuwa chini ya Mwenyekiti wake, Jaji Mstaafu Hamis Msumi, Chenge alisema
hawezi kuhojiwa na kikao hicho kwa vile suala lake tayari lipo mahakamani,
kauli iliyomfanya Msumi na wajumbe Selina Wambura na Hilda Gondwe kukosa la
kufanya.
Baadaye Jaji Msumi aliwaambia waandishi wa habari kuwa
atatoa tamko la Baraza kuhusu suala hilo kesho, huku likijiandaa pia kuwaita na
kuwahoji wanasiasa wengine, akiwemo Waziri wa zamani wa Ardhi, Nyumba na
Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka, ambaye naye alipewa kiasi kama
hicho cha fedha.
Wengine watakaoitwa kuhojiwa ni pamoja na mbunge wa
Sengerema, William Ngeleja, Mkuu wa wilaya ya Korogwe, Mrisho Gumbo na kiongozi
mwandamizi wa Ikulu, anayetajwa kwa jina la Shaaban Gurumo.
(HABARI: DENIS MTIMA, HARUNI SANCHAWA/GPL)
No comments:
Post a Comment