HOTUBA YA NDG. ZITTO KABWE KWA TAARIFA YA KAMATI YA KILIMO
NA KAMATI YA ARDHI HIYO HAPO CHINI
Kilimo
Mheshimiwa Spika,
Mwaka 2014 umekuwa ni mwaka mwema kwa sekta ya kilimo
nchini. Uzalishaji umeongezeka, mazao ya chakula tumezalisha ziada kwa 125% ya
mahitaji yetu ya chakula. Kwa upande wa mazao ya biashara, zao la Korosho
limeweka rekodi Mpya kwa kuzalisha takribani tani 200,000 za Korosho.
Hata hivyo wananchi hawana furaha na mafanikio haya kwa
sababu ya kutojiandaa kwetu. Wakulima wa mahindi hawajalipwa na bado
tunahangaika na soko la mahindi na mchele. Serikali bado inaruhusu Mchele
kutoka nje kuingia nchini ilihali mchele wetu unakosa soko. Maghala ya
kuhifadhi nafaka bado kujengwa na Serikali inasema inaongea na nchi ya Poland
kupata mkopo wa kujenga maghala. Ni kama vile Serikali haikuwa na mipango
wakati inajua kuwa uzalishaji utaongezeka zaidi ya maradufu.
Mheshimiwa spika,
Mwaka 2014 tunaweza kuwa tumevuka $1bn ya mauzo nje katika
sekta ya kilimo kufuatia mafanikio makubwa katika Korosho na Tumbaku. 60% ya
mapato ya fedha za kigeni katika kilimo yanatokana na mazao 2 tu: Tumbaku na
Korosho. Mazao haya yanalimwa mikoa ya Tabora, Ruvuma, Mtwara, Lindi, Katavi na
Kigoma.
Ukitazama takwimu za Bajeti, mikoa hii ndio yenye kupata
fedha kidogo zaidi za miradi ya maendeleo kuliko mikoa mingine nchini. Vile
vile wakulima wa mikoa hii ndio wananyonywa zaidi kutokana na mfumo mbovu wa
usambazaji wa pembejeo na soko la mazao yao.
Taarifa ya kamati ya PAC iliyopitishwa na Bunge wiki
iliyopita inaonyesha namna mfumo wa kifisadi katika zao la Korosho unavyowaacha
wakulima wa Korosho katika umasikini wa kutupwa. Wakulima wa Lindi na Mtwara
wanapewa pembejeo zilizo expire na hakuna hatua inayochukuliwa.
Bado tunaendelea kuuza nje Korosho ghafi na ku export maelfu
ya kazi ambazo zingefanywa na vijana na wanawake wa Mtwara. Korosho nyingi
inaibiwa vijijini na vyama vya msingi havilindi maslahi ya mkulima mdogo.
Mheshimiwa spika, napendekeza kwamba sasa tuseme basi na
kuacha kabisa kuuza nje Korosho ghafi. Tunapoteza wastani wa dola 115m kila
mwaka kwa kuuza korosho ghafi nje ya nchi. Iwapo tungekuwa tunauza Korosho
iliyobanguliwa kwenda nje Tanzania ingekuwa na mapato ya fedha za kigeni zaidi
ya dola 500m kwa mwaka kwa Korosho peke yake.
Napendekeza tutumie makato ya ' export levy' katika kipindi
cha miaka 5 ijayo kujenga viwanda vya kubangua Korosho vijijini kwa ushirikiano
kati ya vyama vya ushirika, serikali na sekta binafsi.
Mheshimiwa Spika, kwa upande wa Tumbaku naomba Serikali
ilieleze bunge hatua ambazo imechukua dhidi ya viongozi wa ushirika waliotafuna
fedha za wakulima wa tumbaku mkoa wa Tabora. Naibu Waziri Kilimo alitamka hapa
kwamba jalada lipo kwa IGP, tuelezwe hatua ambazo zimechukuliwa dhidi ya
ubadhirifu mkubwa huo na ni namna gani wananchi wanafidiwa kutokana na upotevu
huo mkubwa wa fedha.
Mheshimiwa spika, narejea pendekezo langu kwamba Serikali
ianzishe rasmi Hifadhi ya jamii kwa wakulima ili sio tu wapate mafao ya muda
mrefu na wa mfupi lakini pia kuwezesha wakulima kufaidika na kilimo kwa kupata
mikopo ya pembejeo na shughuli za kuongeza thamani bidhaa zao.
Akiba ya wakulima inaweza kabisa kusaidia benki ya kilimo
kwa mfuko wa pensheni kwa wakulima kuwekeza hisa zake kwenye Benki hiyo na
hivyo miradi mikubwa ya kilimo kuwa na chanzo cha fedha za maendeleo badala ya
kutegemea Bajeti ya serikali.
Ardhi
Mheshimiwa Spika,
Kamati ya PAC imefanya uchunguzi maalumu kuhusu makusanyo
madogo katika wizara ya ardhi yanayotokana na kutokuwa na rekodi sawa sawa za
viwanja nchini. Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali alieleza katika
taarifa yake ya mwaka 2012/13 kwamba, viwanja zaidi ya 263,000 jijini Dar Es
salaam havipo katika rekodi ya Msajili wa hati.
Maana yake ni kwamba Serikali inapoteza mapato zaidi ya tshs
83 bilioni Kwa mwaka. Viwanja hivi vinashikiliwa na maafisa wa wizara ya ardhi.
PAC imependekeza kwamba mara moja Serikali ianze kutoa Hati za Ardhi za
kidigiti ( digital land titles) na kuziwianisha na nambari za utambuzi wa mlipa
kodi ( TIN ).
Hatua hii itaondoa kabisa tatizo la hati zaidi ya moja kwa
kiwanja kimoja kwa mtu zaidi ya mmoja. Mfumo huu uanze kwa Manispaa za Jiji la
Dar Es Salaam na baadaye nchi nzima. Serikali, kwa kuwa haina Bajeti, ifanye
mradi huu kwa kutumia PPP kwa kushirikisha sekta binafsi.
Mheshimiwa Spika, napendekeza kufanya marekebisho katika
mapendekezo ya taarifa ya taarifa ya kamati kwa kuweka pendekezo la kuitaka
Serikali kuanza mradi huu katika mwaka wa fedha unaoanza mwezi Julai mwaka huu.
Utalii
Mheshimiwa Spika, taarifa ya Kamati inaonyesha kuwa Waziri
wa Utalii ameshindwa kutoa tangazo la Serikali ili tozo Mpya za concession zianze
kutozwa. Tozo Mpya hazitozwi toka mwaka 2011 na hivyo TANAPA kupoteza zaidi ya
shilingi 80 bilioni.
Wafanyabiashara walikwenda mahakamani na kushindwa kesi.
Waziri miezi minne amekaa bila kutekeleza hukumu. Waziri anapaswa kuwajibishwa
kwa kupotezea mapato Serikali. Bunge limuazimie Waziri huyu iwapo mpaka mwisho
wa siku Leo atakuwa hajatoa tangazo la Serikali.
Zitto Kabwe
2/2/2015
No comments:
Post a Comment