Mhe. Zitto Kabwe akitoa Ahsante kwa wananchi wa jimboni
kwake kwa kumchagua kuwa mbunge wao kwa vipindi viwili.
Mwanamapinduzi na Rais wa zamani wa Burkina Faso Thomas
Sankara alisema kuwa ili kuleta mabadiliko ya kimapinduzi ni lazima kuwa na
hali fulani ya uendawazimu.
Ila tusiufikirie uendawazimu huu wa kuokota makopo bali ule
ukichaa mzuri wa kuamini katika mambo au misingi fulani na kuisimamia kwa dhati
pamoja na changamoto nyingi.
Kwa kuamini kwa dhati katika mabadiliko haya na kutaka
kuboresha maisha ya wanakigoma, mwaka 2005 nilikuja kwenu kuwaomba ridhaa ya
kuwatumikia kama mwakilishi wenu Dodoma. Nikiwa na umri wa miaka 29 tu.
Labda ulikuwa ni msukumo wa matumaini yangu makubwa
yanayoambatana na ujana yaliyowashawishi, kwani mliniamini na kunipa kazi hiyo
ya heshima kubwa ya kuwawakilisha.
Mwaka 2010 mliniamini tena, naamini kutokana na utekelezaji
wangu mzuri wa kazi na mafanikio tuliyoyaweza kuyapata katika jimbo letu.
Hivyo kwa miaka kumi tumekuwa bega kwa bega katika safari
hii ya pamoja ya kujenga na kuiendeleza jimbo letu, na leo nimekuja kuwashukuru
kwa fursa mliyonipa kwani safari yetu inafikia mwisho. Fursa mliyonipa ni ya
kipekee kwani ilikuwa fursa si tu ya kuwatumikia ninyi bali kulitumikia Taifa
langu.
Katika miaka kumi hii kuna mambo makubwa tumeyafanya pamoja
na kufanikiwa; na kuna mambo ambayo hatukuweza kuyafanya. Kwa yale ambayo
hatukuweza kuyafanya naomba radhi. Kwa yale ambayo tumeweza kuyafanya naomba
kuwapongeza sana kwa kufanikisha. Kwani kama Mwalimu Nyerere alivyotuambia
kuhusu Uhuru na Maendeleo:
"Uongozi ni kuongea na kujadili na wananchi,
kuwaelewesha na kuwashawishi. Uongozi ni kufanya kazi pamoja na wananchi na
kuonyesha kwa vitendo mnachotaka kufikia. Uongozi ni kuwa mmoja wa wananchi na
kutambua kuwa mko sawa.... Wananchi hawawezi kuendelezwa bali
wanajiendeleza." Na ndivyo tulivyofanya kwa miaka kumi, na kwa ushirikiano
wenu tumeweza kufanikisha miradi mikubwa katika Jimbo letu.
Mwaka 2005 tulikuwa hatuna barabara ya lami hata moja. Leo
hii, ninapoongea nanyi tuna barabara za lami zenye zaidi ya kilomita 100
kuunganisha Jimbo letu na majimbo mengine kwa pande zote za nchi kavu. Vilevile
tuna mradi mkubwa wa kuunganisha vijiji vya ufukweni mwa Ziwa Tanganyika kwa
barabara.
Kiujumla kwa mkoa wa Kigoma tumefanikiwa kumaliza daraja la
Malagarasi na hivyo kuunganisha mkoa wetu na mkoa wa Tabora kwa lami jambo
ambalo lilikuwa kilio chetu cha muda mrefu sana tokea enzi na enzi. Muhimu
zaidi ni kuwa barabara hizi zinatumika na wananchi, wafanyabiashara na wakulima
ili kuwasiliana, kufanya biashara na kupanua masoko.
Tumefanikiwa kuongeza huduma ya Nishati ya Umeme kwa
kuunganisha vijiji zaidi ya 16 hivi sasa. Changamoto kubwa iliyobakia mkoani
kwetu ni uzalishaji mdogo wa umeme na wenye gharama kubwa sana. Suluhisho la
kudumu ni kufanikisha mradi wa Malagarasi wenye uwezo wa kuzalisha 44MW ambao
utakuwa nafuu na kuwezesha pia kusambaza umeme mikoa jirani ya Katavi na
Tabora, na hata kuuza nchi jirani ya Burundi.
Viongozi wa kisiasa wa mkoa wa Kigoma watakaoingia kwenye
uongozi baada ya uchaguzi mkuu mwezi Oktoba mwaka 2015 hawana budi kuweka
kipaumbele kikubwa kwa mradi huu. Bila ya umeme wa uhakika na nafuu hatuwezi
kupiga hatua ya kuongeza thamani ya mazao yetu kwa kujenga viwanda vya
usindikaji na kuongeza ajira ya vijana wetu.
Tumefanikiwa kuanza miradi ya Bandari na Soko kubwa kijiji
cha Kagunga. Lengo likiwa ni kukuza biashara ya bidhaa kati yetu na nchi ya
Burundi. Kigoma ni mji wa biashara kiasili na biashara ilichukua nafasi kubwa
ya uchumi wa mkoa huu kwa miaka mingi sana. Kuimarishwa kwa miundombinu ya
Biashara ni sehemu ya miradi ya kimkakati katika kuuweka mkoa kuchukua nafasi
yake ya kiuchumi katika nchi yetu.
Katika muktadha huo ndio maana tunaendelea na miradi ya
Bandari Kibirizi na Bandari ya Nchi Kavu Katosho. Ndio maana tunaendelea na
mradi wa Kituo cha Usafirishaji Mwandiga ( Mwandiga International
Transportation Terminal ) na eneo maalumu la kiuchumi Ujiji. Haya yote
tuliyaanzisha kwa pamoja nanyi ili kuhakikisha kuwa uchumi wetu unazalisha
ajira kwa watu.
Tumefanikiwa kuongeza udahili wa wanafunzi wa sekondari kwa
kuwa na shule katika kata na baadhi ya kata tumejenga shule kila kijiji. Hata
hivyo, tuna changamoto kubwa sana ya ubora wa elimu katika mkoa wetu. Katika
jimbo la Kigoma Kaskazini zaidi ya 90% ya watahiniwa wa Kidato cha Nne wanapata
madaraja ya mawili ya chini, wakati ule daraja la nne na daraja la sifuri.
Tumeanzisha mradi wa majaribio ya kutoa motisha kwa Walimu
ili kuona namna bora zaidi ya kuhakikisha elimu inaboreshwa. Shirika la Twaweza
linaendesha mradi mkubwa wa motisha kwa walimu na baada ya mwaka huu tutakuwa
tumejifunza njia bora za kuongeza ubora wa elimu kwa watoto wetu. Bila Elimu
bora miradi yote niliyoeleza hapo awali haina maana yeyote.
Serikali imetoa Sera mpya ya Elimu, ni wajibu wetu kuona
namna ya kuitekeleza katika ngazi yetu ili kupata mafanikio. Hata hivyo,
uongozi wa kisiasa utakaoingia baada ya uchaguzi mkuu mwaka huu hauna budi
kujielekeza vya kutosha katika elimu ya ufundi ili kujenga stadi za kazi kwa
vijana waweze kujiajiri na kuajiriwa.
Tumefanikiwa kupanua huduma ya Afya kwa kuboresha Zahanati
zetu chache zilizokuwepo na kujenga zahanati kadhaa mpya na miradi ya vituo vya
afya vya Mahembe na Nyarubanda. Hata hivyo nasisitiza sana umuhimu wa kinga
kuliko tiba kwani gharama za afya zimekuwa kubwa sana. Ndiyo maana tulipojadili
hili suala, ilionekana kuwa suluhisho linatakiwa lipatikane kwa kufanya kile
ambacho hatujawahi kufanya ili kuleta maendeleo ya kweli.
Na mniruhusu hapa kunukuu wosia wa Baba wa Taifa Mwalimu
Nyerere, alipotuasi kuwa "Maendeleo ni maendeleo ya watu. Barabara,
Majengo, kuongezeka kwa uzalishaji wa mazao na masuala mengi kama haya si
maendeleo, bali ni vitendea kazi tu vya maendeleo" Ndiyo maana kulikuwa na
umuhimu wa kutafuta njia mpya na mbadala kuboresha maisha ya mwananchi, hususan
kwa upande wa afya. Uthibitisho wa ubunifu wetu ni kuwa katika kipindi hiki cha
miaka 10 tumefanikiwa kuanzisha hifadhi ya jamii kwa wakulima.
Tulianza na Ushirika wa Wakulima wa Kahawa wa RUMAKU ambapo
wananchi walijiunga na NSSF na hivyo kupata mikopo ya muda mfupi, huduma za
afya bure na kujiwekea akiba kwa ajili ya mafao ya muda mrefu. Mafanikio
makubwa yaliyopatikana yamewezesha wazo hili kusambaa nchi nzima na hivi sasa
wakulima wa Korosho, Chai, Pamba, Tumbaku wanafuata nyayo za Wakulima wa
Ushirika wa RUMAKU.
Hapa Kigoma wazo hili sasa linatekelezwa kwa wavuvi wa
mwambao mwa Ziwa Tanganyika. Ndoto yetu ni wananchi zaidi ya theluthi moja
kwenye nguvu kazi wawe na Hifadhi ya Jamii. Natoa wito kwa wananchi wengine wenye
uwezo wa kuchangia hifadhi ya jamii wajiunge na vikundi vya ushirika na
kuchangia ili kufaidika na mafao ya muda mrefu kama pensheni lakini pia yale ya
muda mfupi kama bima ya afya, mikopo kupitia SACCOS na mengine yatakayoanzishwa
kama bima ya mazao.
Tumefanikiwa kujenga heshima ya watu wa Kigoma hapa nchini.
Hivi sasa watu wa Kigoma tunatembea kifua mbele bila woga kuliko hapo awali.
Kujiamini na kushiriki kikamilifu katika Ujenzi wa Jamhuri ya Muungano ni
wajibu wetu kama raia. Changamoto za kujiona raia wa daraja la pili zimeondoka
na zinaendelea kutokomezwa. Juhudi zetu ni silaha kubwa katika kuhakikisha
tunakuwa sehemu ya Jamhuri yetu katika kila Nyanja za maisha yetu. Nafurahi
kupata fursa ya kushiriki nanyi katika kujenga heshima hiyo ya Mkoa wetu.
Nitaendelea kushiriki katika kudumisha heshima hiyo.
Nimejifunza mengi sana katika safari hii ya utumishi kwenu.
Kama nilivyosema hapo awali, mliamua kufanya kile kisichozoeleka katika siasa
ya nchi yetu kwa kunipa jukumu hili nikiwa kijana mdogo. Naamini kuwa ule
ukichaa wangu mzuri wa kusimamia misingi ya kuleta maendeleo kwa wananchi wangu
na kuhakikisha huduma muhimu zinawafikia nimezipigania. Na katika safari hii
nimejenga marafiki wengi sana na pengine hata maadui ingawa hao ni wachache.
Lakini haijalishi kwani mi binafsi sina uhasama na binadamu mwenzangu.
Katika utumishi wangu kwenu, bungeni nimejifunza namna nchi
yetu inaendeshwa. Katika kujifunza huko kuna mambo kadhaa nimefanya ya
kujivunia na mengine ni makosa. Mliniruhusu kufanya makosa na kuyarekebisha
makosa hayo kwa hiyo kukomaa zaidi.
Shukrani za dhati ziwaendee wazee wangu ambao mliniongoza
mpaka hapa tulipofika na kunishauri hata kunionya pale palipohitajika. Kwa
ujumla nimejifunza kuwa mzalendo zaidi kwa nchi yangu na kuwatumikia watu wa
nchi hii. Ndio maana hamkunisikia tu kutetea watu wa Kigoma pekee, bali watu
maeneo mengine ya nchi yetu na makundi mbalimbali ya kijamii kama Wakulima,
Wafanyakazi, Wasanii, Wavuvi, Wana michezo na wana habari.
Katika safari hii ya miaka 10 kuna watu nimewafurahisha na
kuna watu nimewaudhi. Kwa wale niliowaudhi ninaomba radhi. Kwa wale
niliowafurahisha ninaomba wasiache kuniongoza na kunishauri kila wakati.
Haikuwa safari rahisi na sikutegemea iwe rahisi. Kiuhalisia ilikuwa safari
ngumu yenye mafunzo makubwa kwangu. Ilikuwa ni safari yangu kama kiongozi na
pia safari yangu binafsi ya kupevuka kifikra na kupata mafunzo kuhusu maisha.
Ukifika ulikokuwa unakwenda katika safari, unaweza
kutathmini mengi kuhusu safari hiyo, lakini mwisho wa siku unatakiwa ujue kama
safari hii ilikuwa njema ama la. Ninajivunia safari hii na ninasema kwa dhati
kabisa ilikuwa ni safari njema.
Ni wakati sasa wa kutoa nafasi kwa nguvu mpya kuongoza Jimbo
letu. Kushika kijiti pale ninapoishia. Kurekebisha pale nilipokosea. Kuimarisha
pale nilipofikia.
Sitakuwa mbunge wenu baada ya Uchaguzi Mkuu mwezi Oktoba
lakini nitaendelea kutetea maslahi ya Mkoa wa Kigoma na Taifa letu kwa njia
nyingine.
Sitaacha ule uendawazimu mzuri aliyoizungumzia Thomas
Sankara unaoleta maendeleo ya kimapinduzi. Na misingi ni ileile na maadui ni
walewale ambao mwasisi wetu Mwalimu Nyerere aliyokuwa anasema tupambane nao, yaani
umaskini, ujinga, maradhi na sasa tumeongeza ufisadi.
Kizazi chetu kina jukumu la kipekee kuendeleza mapambano
haya na nitaendelea kuhakikisha tunafanya mapinduzi na kuwa na Taifa lenye
misingi madhubuti ya uwajibikaji ili kuondoa kila aina ya ufisadi na kutumia
rasilimali za nchi kuondoa umasikini, ujinga na maradhi.
Asanteni sana Kigoma Kaskazini!
No comments:
Post a Comment