Social Icons

IMETOSHA

IMETOSHA

Friday, April 3, 2015

HOMA YA UCHAGUZI: ZITTO, UKAWA NGOMA NZITO


Mh. Zitto Kabwe
Homa ya uchaguzi inazidi kupanda kuelekea uchaguzi mkuu wa madiwani, wabunge na rais unaotarajiwa kufanyika Oktoba, mwaka huu huku habari kubwa ikiwa ni jeuri ya fedha iliyooneshwa na chama kipya cha Zitto Kabwe, Alliance for Change and Transparency (ACT- Tanzania) kufanya uzinduzi wa kihistoria uliogharimu mamilioni ya fedha.
Zitto aliyekuwa Mbunge wa Kigoma Kaskazini kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo 

 
(Chadema), alitimuliwa kwenye chama hicho hivi karibuni na siku chache baadaye, akaibukia kwenye chama hicho na kuchaguliwa kuwa Kiongozi Mkuu Taifa wa chama hicho.
Baada ya uchaguzi huo, Machi 29, 2015, ACT kilizinduliwa rasmi katika hafla kubwa iliyoacha gumzo, iliyofanyika kwenye Ukumbi wa Diamond Jubilee jijini Dar es Salaam na kuwakutanisha watu mbalimbali kutoka mikoa kadhaa ya Tanzania sambamba na wageni waalikwa kutoka nje ya nchi.

Jeuri ya fedha iliyotumika kwenye uchaguzi huo, kwa kukodi ukumbi wa gharama, kuwagharamia wajumbe wote kutoka mikoani na kurusha matangazo ya runinga moja kwa moja kupitia runinga za ITV na Azam TV, ilisababisha minong’ono mingi kuanza kusambaa kwamba nyuma ya chama hicho, kulikuwa na mkono wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).

“Haiwezekani chama ndiyo kwanza kimeanzishwa juzijuzi tu halafu wawe na jeuri ya fedha kiasi hiki, kurusha matangazo ya moja kwa moja kwenye runinga mbili za ITV na Azam TV kunagharimu fedha nyingi sana, Zitto na wenzake wamepata wapi fedha hizo? Kuna mkono wa mtu hapa,” mdau mmoja aliyeomba hifadhi ya jina lake, aliliambia Uwazi Mizengwe nje ya ukumbi huo wakati uzinduzi ukiendelea.

Wasomaji wengine waliofuatilia uzinduzi huo, walipiga simu chumba cha habari na kudai kuwa kuna zengwe limeandaliwa kumpaisha Zitto na chama chake kwa lengo la kupunguza kura za Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) katika uchaguzi mkuu ujao.

“Hawa jamaa (CCM) ni wajanja sana, wameamua kuwekeza ACT kwa kuwapa fedha na kuwagharamia kila kitu ili kuwachanganya wapinzani. Unajua mpaka sasa tayari kuna watu walikuwa Ukawa wameshahamia kwa Zitto, CCM wamefanya makusudi ili waendelee kutawala, wanatumia ile falsafa isemayo ‘Divide and Rule’ (Gawanya kisha Tawala),” alisema Sunday Makweta wakati akizungumza na gazeti hili.

Ili kupata ukweli wa zengwe hilo, Uwazi Mizengwe liliingia kazini ambapo lilianza kwa kumtafuta Zitto. Alipopatikana, alisomewa madai kwamba chama chake kinadaiwa kufadhiliwa na CCM kwa lengo la kudhoofisha Ukawa ambapo alishangaa madai hayo na kufunguka:

“Huyo anayetuhumu hivyo aseme huyo mfadhili ni nani na kafadhili nini. Yeyote mwenye mawazo hayo hafikirii. Wanachama wamejitolea, gharama za kurusha matangazo ya moja kwa moja tumepewa discounts (punguzo la bei). Tumechanga kutoka kwa marafiki, hiki chama ni sawa na moto wa pumba, ni chama kikubwa na tumedhamiria.”

Uwazi Mizengwe lilimtafuta pia mwenyekiti wa chama hicho (Taifa), Annastazia Mghwira alisema si kweli kwamba chama chao kinafadhiliwa na CCM kwa sababu kwanza wana kesi dhidi ya chama hicho mahakamani kutokana na madai ya kuibiwa kura kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa.
“Chama chetu kinapaa kutokana na wanachama kujitolea na tunataka kuhamisha uwezo kwa wananchi na kuing’oa CCM madarakani.”

Baada ya kusikia kwa upande huo, Uwazi Mizengwe pia lilimtafuta Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye na kumuuliza kuhusu madai ya chama chake kukifadhili ACT kwa lengo la kudhoofisha nguvu za Ukawa ambapo alikanusha vikali chama chake kuhusika kwa namna yoyote na chama cha ACT.

“CCM ni taasisi kubwa yenye wanachama na wapenzi wengi. Huwezi kuihusisha na chama chochote cha siasa. Najua kuna watakaosema chama cha Zitto ni CCM B lakini ukweli ni kwamba wanaovumisha hayo ni Ukawa ambao wamefilisika.
“Ninachoweza kutabiri kwa sasa ni kwamba mara baada ya kura za maoni kuhusu Katiba Inayopendekezwa kupigwa, Ukawa itakufa na watasema pia kuna mkono wa CCM wakati ukweli ni kwamba watakuwa hawana ajenda tena,” alisema Nape.

Aliongeza kwamba hivi sasa wanashughulika na ukaguzi wa uhai wa chama nchi nzima na juzi walikuwa wakimalizia ziara yao mkoani Kilimanjaro.
“Hapa tumefanya vizuri sana na uhai wa chama umeimarika... wapinzani waachane na kudhani CCM itaacha kazi zake na kushughulika nao, tuna kazi nyingi za kushughulikia kero za wananchi maana ndiyo wapiga kura wetu na migogoro yao wasituingize, Zitto amekosana na Chadema siku nyingi na sisi CCM tulikuwa tukisoma tu kwenye vyombo vya habari,” alisema Nape.

Kwa upande wa Ukawa, Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa, akizungumzia ujio mpya wa Zitto na hofu ya chama hicho kupunguza kura zao kwenye uchaguzi mkuu ujao, alifunguka:
“Katika vitu ambavyo havitunyimi usingizi katika uchaguzi mkuu ujao ni ACT na Zitto...siyo tishio kwa Ukawa hata kidogo. Hawezi kuipasua Chadema wala Ukawa na mtakubaliana nami baada ya uchaguzi mkuu kufuatia matokeo atakayoyapata.”

Naye Mkuu wa Idara ya Sayansi, Siasa na Utawala wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk. Benson Bana, akizungumza na waandishi wa habari hivi karibuni, alisema Ukawa hawapaswi kuipuuza ACT kwani kama itajipanga vizuri na kuepuka migogoro ya ndani ya chama, inaweza kujizolea kura nyingi kwenye uchaguzi ujao na hivyo kupunguza nguvu ya Ukawa.

“Zitto bado ni hai kisiasa, anajua kujenga hoja na akaisimamia mpaka mwisho. Ana ushawishi mkubwa, anaheshimika, na kupendwa na nchi nzima kwa jumla, uwepo wake ndani ya ACT wanaweza kupanda chati haraka na kuwa miongoni mwa vyama vya siasa vyenye wafuasi wengi na vyenye nguvu nchini,” alisema

No comments:

Post a Comment