WAZIRI
wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi, amesema wizara
yake imehuisha viwango vya kodi, ada na tozo mbalimbali za ardhi kwa
lengo la kupata viwango vinavyopangika.
Lukuvi alitoa kauli hiyo bungeni mjini Dodoma jana, wakati akiwasilisha makadirio na matumizi ya wizara yake kwa mwaka 2015/16.
Alisema
kodi ya pango la ardhi imepungua kwa wastani wa asilimia 30 na viwango
vingine vinavyomgusa mwananchi wa kawaida vimepungua kwa asilimia 50 au
zaidi.
“Kwa
mfano kodi ya kupima mashamba imepungua kwa asilimia 60, kutoka Sh
1,000 hadi Sh 400, na mashamba ya biashara imepungua kwa asilimia 50
kutoka Sh 10,000 hadi Sh 5,000 kwa ekari.
“Ada
ya upimaji ardhi imepunguzwa kwa asilimia 62.5 kutoka Sh 800,000 hadi
Sh 300,000 kwa hekta, nyaraka za tahadhari na vizuizi vimepunguzwa kwa
asilimia 66.7 kutoka Sh 120,000 hadi Sh 40,000, nyaraka za ubadilishaji
wa majina zimepunguzwa kwa asilimia 62.5 kutoka Sh 80,000 hadi Sh
30,000.
“Vilevile
gharama za kupata nakala ya hukumu kwenye mabaraza ya ardhi zimepungua
kwa asilimia 62.5 kutoka Sh 16,000 hadi Sh 6,000, ada ya kuomba umiliki
wa ardhi imepungua kwa asilimia 75 kutoka Sh 80,000 hadi Sh 20,000,”
alisema.
Aidha
Lukuvi alisema pia ada za maandalizi ya hati imepunguzwa kwa asilimia
68.8 kutoka Sh 160,000 hadi Sh 50,000 ambapo viwango vyote hivyo
vitaanza kutumika Julai Mosi mwaka huu.
Kwa
upande wa tozo la mbele, kwa mwaka wa fedha 2015/16 itapungua kwa
asilimia 50 kutoka asilimia 15 ya kiwango cha sasa hadi asilimia 7.5 ya
thamani ya ardhi na kiwango hicho ndicho kitakacholipwa kwa mashamba na
viwanja wakati wa kumilikishwa.
Kuhusu
uendelezaji wa mji mpya wa Kigamboni, alisema Serikali imefanya mapitio
na kurekebisha matangazo yake ambapo eneo la mpango limepunguzwa kwa
kuondoa kata tatu za Pembamnazi, Kisarawe II na Kimbiji zenye ukubwa wa
hekta 44,440 ambazo hazitakuwapo kwenye mpango, hivyo kubakia na kata
sita zenye ukubwa wa hekta 6,494.
No comments:
Post a Comment