Marehemu Mariam Samuel enzi za uhai wake.
Na Mohemed Shabani, Manyara
DUNIA inazidi kufikia ukingoni! Mwanaume mmoja aliyejulikana kwa jina la Paulo Mahinda, 40, (pichani), mkazi wa Kijiji cha Ndaleta wilayani Kiteto, Manyara anatafutwa na jeshi la polisi wilayani hapa kwa madai ya kumuua mke wake, Mariam Samuel (45) hivi karibuni kwa kumpiga na nyundo kwenye paji la uso, pia kumjeruhi mtoto wake wa mwaka mmoja.
Taarifa za awali kutoka kwa viongozi wa Kijiji cha Ndaleta zinasema kuwa, mwanamke huyo hakuwa tayari kuishi na mumewe ambapo kila mara walikuwa wakigombana na kusuluhishwa na viongozi wa kijiji lakini bila mafanikio.
“Kila mara tulikuwa tukimsuluhisha Mahinda na mkewe walipogombana bila mafanikio, lakini leo umati umeshuhudia mauaji yasiyo ya lazima kwa familia hii,” alisema mkazi wa kijiji hicho aliyejitambulisha kwa jina la Lazaro Gideon.
Akaendelea: “Huyo mtuhumiwa amezaa na marehemu mtoto mmoja ambaye ndiye huyo aliyejeruhiwa, lakini mkewe alikuwa na watoto wengine kumi wa kuwazaa na wanaume wengine.
Mtuhumiwa.
“Tulikuwa tukimshauri kuachana na mwanamke huyo lakini ilikuwa vigumu kwake kutokana na mapenzi yao. Mwisho wa siku ameamua kufanya maamuzi magumu ya kumuua mkewe,” alisema shuhuda huyo.
Kwa mujibu wa mashuhuda, wakati wa kutenda unyama huo, mtuhumiwa alimjeruhi mtoto wake mdogo wa umri wa mwaka mmoja na kukimbizwa Zahanati ya Njoro kwa matibabu.
Katika tukio hilo, watu wanne wakiwemo watoto wa marehemu wawili walipoteza fahamu baada ya kushuhudia mauaji hayo ya kikatili.Kamanda wa Polisi Mkoa wa Manyara, Kamishna Msaidizi, Christopher Fuime alithibitisha kutokea kwa tukio hilo akasema chanzo ni wivu wa mapenzi ambapo mwanamke huyo alikuwa hataki kuishi na mtuhumiwa kutokana na sababu mbalimbali za kifamilia.
Mwili wa marehemu ukipelekwa mazikoni.
Alisema baada ya polisi kupata taarifa hizo, walifika eneo la tukio na kumkuta marehemu akiwa amelala kifudifudi huku damu nyingi zikimwagika, wakauchukua mwili na kwenda kuuhifadhi chumba cha maiti katika Hospitali ya Wilaya ya Kiteto.
Mazishi ya marehemu huyo yalifanyika juzi mjini Kibaya eneo la Kaloleni huku waliokuwa wamepoteza fahamu nao wakirejea katika hali ya kawaida.
No comments:
Post a Comment