Mabingwa watetezi wa ligi kuu Tanzania bara timu ya Yanga imeendeleza wimbi la ushindi katika kuhakikisha inalitetea vyema taji lake baada ya kutoa kipigo kingine cha goli 3-0 mbele ya Tanzania Prisons ‘wajelajela’ kutoka jijini Mbeya kwenye mtanange uliomalizika jioni ya leo kwenye uwanja wa Taifa.
Yanga walianza kupata goli la kwanza kipindi cha kwanza kupitia kwa Mbuyu Twite aliyemalizia mpira uliomponyoka mlinda mlango wa Prisons Mohamed Yusuf na kumkuta Twite aliyeachia shuti kali akiwa hatua chache kutoka langoni.
Wakati ikiwa imeongezwa dakika moja ya nyongeza ili mchezo kwenda mapumziko, Amis Tambwe aliifungia Yanga bao la pili baada ya golikipa Mohamed Yusuf kuutema mpira wa adhabu ndogo uliopigwa na kiungo wa Yanga Thabani Kamusoko na Tambwe kumalizia kwa kichwa na kuifanya Yanga kwenda mapumziko ikiwa mbele kwa goli 2-0.
Kipindi cha pili kilianza kwa Tanzania Prisons kumpumzisha golikipa wao Mohamed Yusuf na kumuingiza Aron Kalambo.
Mshambuliji wa Yanga Donald Ngoma aliihakikishia Yanga ushindi mnono kwa kufunga mkwaju wa penati kufuatia James Josephat kumchezea vibaya Simon Msuva kwenye eneo la hatari. Kutokana na Josephat kumfanyia madhambi Msuva, mwamuzi aliizawadia Yanga mkwaju wa penati pamoja na kumtoa nje Josephat kwa kadi nyekundu.
Huo unakuwa ni ushindi wa pili mfululizo kwa klabu ya Yanga baada ya kushinda mchezo wake wa awali kwa goli 2-0 dhidi ya Coastal Union kwenye uwanja huohuo wa Taifa wakati Tanzania Prisons wao wamepoteza michezo yote miwili waliyocheza jijini Dar es Salaam. Walifungwa goli 2-1 na Azam FC kwenye uwanja wa Azam Complex kabla ya leo kuchezea kichapo cha goli 3-0 mbele ya Yanga.
No comments:
Post a Comment