Social Icons

IMETOSHA

IMETOSHA

Friday, November 20, 2015

CHAMA CHA ADC CHAFUTA VIKOSI VYAKE VYA ULINZI NA USALAMA

index
Na Magreth Kinabo- MAELEZO
Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, imeviasa vyama vingine vya siasa kuiga mfano wa Chama  cha Alliance  For Democratic Change(ADC- Dira  ya Mabadiliko) kutokana na juhudi zake za kutii sheria bila shuruti kutokana na  kuvunja vikosi vya ulinzi na usalama.
 Kauli hiyo imetolewa leo na Naibu Msajili wa Vyama Vya Siasa nchini, Sisty Nyahonza wakati akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jijini Dares Salaam jinsi chama hicho kilivyotekeleza Sheria ya Vyama Vya Siasa Sura ya 258  kifungu cha 9(C) ambayo hairuhusu chama chochote cha siasa kutumia nguvu ili kufikia malengo yake, kwa kutumia vikosi hivyo.
 Naibu Msajili huyo alisema  chama hicho kimefuta Idara ya  Ulinzi na Usalama kijulikanacho  kwa jina la Star Guards kwa mujibu wa barua yao iliyowasilishwa katika ofisi hiyo.

Alisema kwa mujibu wa barua ya chama hicho, iliyosainiwa na  Katibu Mkuu Taifa, Lydia Bendera, Novemba 13, mwaka 2015,  yenye kumbukumbu namba ADC /HQ/GEN/VO1.1/81/15,ambayo ilieleza kwamba kutokana na kikao cha Baraza la Vyama Vya Siasa kilichofanyika Aprili 22,mwaka huu ambacho agenda kuu ilikuwa ni kujadili suala la vyama vya siasa kuwa na vikundi hivyo ni ukiukwaji wa sheria za nchi, na kufikiwa maamuzi yake kuwa;
1.     Vyama vya siasa havina budi kuheshimu sheria za nchi, na kutakiwa kuvunja vikundi vya ulinzi na usalama vilivyoko katika vyama vya siasa.
2.     Vyama vya siasa  vinatakiwa kuondoa  katika Katiba za vyama vifungu,ibara zinazoruhusu kuanzishwa kwa vikundi vya ulinzi na usalama.
Alisema barua hiyo ambayo iliendelea kufafanua kwamba  “kwa kuzingatia maazimio yaliyofikiwa kati ya viongozi wakuu wa vyama vya siasa na ofisi ya msajili wa vyama vya siasa nchini yaliyofikiwa na vyama, chama chetu kimekwisha chukua hatua ya utekelezaji wa maazimio ya baraza la vyama, na yale yote uliyoyaelekeza kupitia barua yako yenye kumb. namba HA.322/362/20/22  ya tarehe 16/06/2015.
“ Kupitia barua hii ninakujulisha rasmi kuwa Mwenyekiti wa Chama Taifa kwa mamlaka aliyopewa na kanuni za chama chetu , ametengua uteuzi wa Mhe. Omari Albert Constantino kuwa mkuu wa idara ya STAR GUARDs,” ilieleza barua hiyo.
Naibu Msajili huyo alisema chama hicho “kimetii sheria ya nchi na  hii iwe chachu kwa vyama vingine kwa kuwa kutuii sheria ni kipaumbele cha demokrasia,” alisema Nyahonza.
 Aliongeza kwamba demokrasia ina vitu vitatu ambavyo ni utii wa sheria, amani na utulivu, hivyo ili demokrasia ifanye kazi lazima kuwe na vitu hivyo.
Aidha Nyahonza alisema Ibara ya 107 ya Katiba ya Nchi inaruhusu Serikali pekee kuanzisha vikosi hivyo.
Akizungumzia kuhusu kwa chama kitakachokiuka agizo hilo, kitachukulia hatua gani alisema kufanya hivyo ni kosa la jinai.
“Sisi tunafanya kazi na jeshi la polisi, ukikataa kufanya hivyo  utakamatwa na utalazimishwa kutii sheria,” alisisitiza.

No comments:

Post a Comment