Social Icons

IMETOSHA

IMETOSHA

Wednesday, November 25, 2015

MAADHIMISHO YA SIKU YA UKIMWI DUNIANI MWAKA 2015 KUFANYIKA KITAIFA DESEMBA MOSI MKOANI SINGIDA

 Mwenyekiti Mtendaji wa Tume ya Taifa ya Kudhibiti Ukimwi Tanzania (TACAIDS), Dk.Fatma Mrisho (kushoto), akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari Dar es Salaam leo mchana, kuhusu Maadhimisho ya Siku ya Ukimwi Duniani mwaka 2015 yatakayofanyika kitaifa Desemba Mosi mkoani Singida. Kulia ni Mkurugenzi wa Habari na Uraghibishi.
 National Programe Officer wa UNAIDS, Fredrick Macha (kulia), akizungumza katika mkutano huo.
 Mkurugenzi wa Uendeshaji Programu wa Taasisi ya Tunajali, Dk.Mussa Ndile akizungumza katika mkutano huo.

 
 Ofisa Uhusiano wa Tacaids (kulia), akizungumza katika mkutano huo.
 Wapiga picha wa TV wakichukua tukio hilo.
 Wanahabari wakichukua taarifa hiyo.
Wadau wa masuala ya Ukimwi wakiwa katika mkutano huo wakisubiri kujibu maswali ya wanahabari.


Na Dotto Mwaibale

MAAMBUKIZI ya virusi vya Ukimwi nchini yameongezeka kwenye kundi la vijana wenye umri wa miaka kati ya 19 mpaka 24 tofauti na ilivyokuwa miaka minne iliyopita, ambako kundi lililokuwa limeathiriwa zaidi lilikuwa miaka kati ya 25 mpaka 34, imeelezwa.

Pia licha ya kwamba kiwango cha maambukizi mapya ya virusi hivyo nchini kimeshuka kutoka asilimia 7 mwaka 2004 mpaka kufikia asilimia 5.3 mwaka huu, takwimu za baadhi ya mikoa ikiwemo Singida, Kigoma, Arusha, Mtwara, Kilimanjaro na Kagera zimeonekana kuongezeka.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Kudhibiti Ukimwi Tanzania (Tacaids) kuhusu maandalizi ya maadhimisho ya siku ya Ukimwi duniani kwa mwaka huu, Dk. Fatma Mrisho,  alisema kazi kwa ujumla kazi kubwa imefanyika.

Alisema ikilinganishwa na miaka 10 iliyopita, maambukizi mapya ya virusi vya Ukimwi yamepungua kwenye maeneo mengi ya nchi kutokana na jitihada za serikali, wadau na wananchi kwa ujumla.

Dk. Mrisho alisema licha ya mikoa kadhaa kuendelea kuandamwa na maambukizi hayo, kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo maendeleo na mwingiliano wa watu, mikoa ya Tanga na Manyara ndiyo yenye takwimu chache za maambukizi zikiwa na asilimia 4 pekee.

Alisema kutokana na takwimu hizo, maadhimisho ya mwaka huu ya siku ya Ukimwi duniani kitaifa yatafanyika mkoani Singida, ambapo yatazinduliwa leo wilayani Singida mjini na Mkuu wa mkoa huo Parseko Kone, huku Rais Dk. John Magufuli akitarajiwa kuwa mgeni rasmi kwenye kilele Desemba 1, mwaka huu.

Alisema maadhimisho hayo yatatumika kufanya kazi kama ilivyo kauli mbiu ya uongozi wa serikali ya awamu ya tano ambapo pamoja na mambo mengine, zaidi ya watu 3,500 wanatarajiwa kupimwa afya zao huku zaidi ya 10,000 wakitegemewa kupewa mafunzo maalumu kuhusu Ukimwi na virusi vya Ukimwi (VVU).

Alisema kauli mbiu ya mwaka huu ya maadhimisho hayo ni “Tanzania bila maambukizi mapya ya VVU, vitokanavyo na Ukimwi na ubaguzi, unyanyapaa inawezekana,” hivyo kila mtu ashiriki kikamilifu katika kutekeleza mikakati ya serikali ya kudhibiti Ukimwi kitaifa na kimataifa ikiwa ni pamoja na kufikia malengo ya maendeleo endelevu ya milenia (MSDG)

inayofikia tamati 2030.
“Kauli mbiu hii inalenga kutoa msukumo wa utekelezaji wa mikakati mbalimbali ya kudhibiti Ukimwi kitaifa na kimataifa ili kufikia azma ya sifuri tatu yaani, maambukizi mapya sifuri, vifo vya Ukimwi sifuri na unyanyapaa sifuri,” alisema.

Aliongeza kuwa kufanyika maadhimisho hayo mkoani Singida kutatoa fursa kwa wananchi wa mkoa huo na jirani kushuhudia maonyesho ya shughuli za wadau wa udhibiti Ukimwi nchini ikiwemo utoaji elimu, huduma

mbalimbali za kiafya na burudani.

Alisema kumeandaliwa kongamano la kitaifa kutathmini hali ya mwelekeo wa udhibiti Ukimwi nchini litakalofanyika Novemba 29 na 30 pamoja na uzinduzi wa mfuko wa fedha wa kudhibiti Ukimwi nchini (AIDS Trust Fund) unaolenga kuongeza uwezo wa ndani wa kugharamia huduma muhimu kudhibiti Ukimwi.

Pia alisema, “Katika maadhimisho ya mwaka huu tutakuwa na uzinduzi wa kituo cha maarifa ya kudhibiti Ukimwi kilichoko Manyoni kilichojengwa na TACAIDS kupitia program ya ‘Kilimanjaro Challenge Against HIV na AIDS’, inayoratibiwa na kampuni ya uchimbaji madini ya Geita (GGM).

“Lengo la kituo hiki ni kutoa elimu ya udhibiti Ukimwi na huduma mbalimbali kama vile upimaji na ushauri nasaha kwa wasafirishaji

ukizingatia jografia ya eneo lile (Manyoni), lina makutano ya watu wengi kutokana na uwepo wa kituo cha treni, mapumziko makubwa ya
magari ya mizigo.”


Pamoja na kituo hicho, TACAIDS watazidua vituo vingine sita vilivyojengwa katika maeneo ya Bandari ya Dar es Salaam vituo viwili,

Iringa (viwili) na Mbeya eneo la Tunduma vituo viwili. Kwa mujibu wa Dk. Mrisho, Vituo hivi vimeanzishwa kwa ushirikiano wa TACAIDS na Taasisi ya North Star Alliance (NSA).

No comments:

Post a Comment