Social Icons

IMETOSHA

IMETOSHA

Thursday, December 3, 2015

Mashine za MRI, CT-SCAN Hazitakwama Tena - Katibu Mkuu


Serikali imewahakikishia Watanzania kwamba mashine ya Magnetic Resonance Imaging (MRI) pamoja na Computerized  Tomography Scan (CT-SCAN) katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH)  hazitakwama kufanya kazi kwa kuwa imeweka utaratibu mzuri wa kuzitengeneza.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii Dk. Donan Mmbando amesema serikali imezungumza na Philips na wamekubaliana kwamba mashine hizo hazitakwama na endapo litatokea tatizo la kiufundi watashughulikia mara moja.

“Mwaka ujao ni mwaka wa bajeti  serikali itatenga fedha kwa ajili ya kutengeneza mashine za CT-SCAN na MRI,  lakini mtambue kwamba si tu mashine hizo zinapaswa kutengenezwa bali na mashine nyingine.”amesema Dk Mmbando.

Pia, Dk Mmbando  amefungua duka la dawa  la Bohari Kuu ya Dawa (MSD) ndani ya Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) na kueleza kwamba kufunguliwa kwa duka hilo kutasaidia wananchi kupata huduma haraka na kununua dawa kwa gharama nafuu  na huduma hiyo itatolewa kwa saa 24.


Akifafanua  kuhusu mashine za MRI na CT-Scan, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili Profesa Lawrence Mseru amesema Novemba 25, 2015  alifika fundi kutoka Afrika Kusini ambaye pia ni fundi wa MRI na kuitengeneza na kuanza kufanya kazi tangu Novemba 26 mpaka Disemba 2, mwaka huu. Wagonjwa 152   wamepimwa na kwamba wengi wagonjwa wa dharura.

Amesema hivi sasa mafundi wanafunga mashine ya Digital X-Ray iliyotolewa na serikali kupitia Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii ambapo  usimikaji unatarajiwa  kukamilika mwishoni mwa juma hili.

Akielezea utekelezaji wa agizo la wagonjwa wanaolala chini kupatiwa vitanda, Profesa Mseru amesema ili kuondoa wagonjwa wote waliolala chini, serikali kupitia MSD ilileta vitanda 300 pamoja na magodoro yake, vitanda hivyo vyote vilipelekwa kwenye Taasisi ya Tiba ya Mifupa Muhimbili (MOI) na tayari MOI imeanza kuhamisha wagonjwa waliokuwa wamelala chini kutoka wodi za MNH walizokuwa wanazitumia, mpaka sasa wagonjwa 120 wamehamishwa.

Novemba 9, mwaka  huu Rais John Magufuli alifanya ziara MNH na kutoa maagizo kwamba ndani ya wiki mbili mashine ya MRI na CT-SCAN ambazo zilikuwa zimeharibika ziwe zinafanya kazi, wagonjwa waliolala chini wawe wamepata vitanda  na Bohari Kuu ya Dawa (MSD) ifungue duka la dawa ndani ya hospitali ili kuondoa ukosekanaji wa dawa.

No comments:

Post a Comment