Social Icons

IMETOSHA

IMETOSHA

Wednesday, December 23, 2015

WARAGHABISHI WA KIJIJI CHA OLOLOSOKWANI WILAYA YA LOLIONDO WAPIGWA MSASA NA PALISEP


Mraghbishi Kootu Tome (wa pili kushoto) akiwa na mtendaji wa kijiji Rabie Lebuna (mwenye shati la njano) na Mwenyekiti wa Kijiji, Kerry Dukonya (wa pili toka kulia).
Na Kisuma Mapunda,Loliondo

Sasa ni dhahiri waraghbishi wanatambua majukumu na haki zao ndani ya jamii. Uelewa wao umewapa fursa ya kuchukua hatua na kusimamia kile wanachoamini kwa manufaa ya wanajamii wanaowatumikia.
Watu hawa wamekuwa mhimili muhimu wa kuleta mabadiliko katika maeneo wanayoishi. Lakini inapendeza zaidi kuona waraghbishi hao wakijawa na dhamira ya dhati ya kuwatumikia wananchi wao kwa kujitokeza kuwania nafasi mbalimbali za uongozi kama ilivyo kwenye Kijiji cha Ololosokwani, kilichopo katika tarafa ya Loliondo, wilayani Ngorongoro, mkoani Arusha.
Kijiji hiki kina jumla  ya kaya 1,520 zinazoundwa na vitongoji vinne vya kijiji, ambavyo ni Sero, Ololosokwani, Mairowa A na B. Baadhi ya wanaounda kaya hizo ni pamoja na waraghbishi wanaofanya kazi na mradi wa Chukua Hatua, akiwamo Kootu Tomu, mama wa watoto sita kutoka kitongoji cha Mairowa. 

 
Tomu ni mmoja wa waraghbishi wa kwanza kuanza kufanya  kazi na mradi wa Chukua Hatua wakiwa na jukumu la  kufuatilia ahadi za wagombea wakati wa uchaguzi wa mwaka  2010. Ni katika uraghbishi huu wa kufuatilia ahadi zilizokuwa zinatolewa na wagombea, ndipo alipojifunza taratibu na kanuni za kuwa kiongozi bora.
Miaka mitano baadaye, alijitokeza katika kinyang’anyiro cha kuomba kuchaguliwa na wanachama wenzake wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika kura ya ndani ya maoni. Na baada ya hapo alipata fursa ya kupeperusha bendera ya chama chake na kuchaguliwa katika uchaguzi uliofanyika mwezi Disemba mwaka 2014.
Akielezea jinsi ilivyokuwa Kootu Tomu anasema:
“Nilifahamu jukumu lililokuwa mbele yangu katika kusimamia haki kwenye migogoro ya ardhi katika eneo letu. Hivyo, katika uchaguzi uliopita wa serikali za mitaa niliomba ridhaa ya kuchaguliwa kuwa mjumbe wa kijiji kupitia CCM na nilichaguliwa. Sasa naweza kuwafikia wananchi wengi zaidi hasa akinamama kupitia fursa hii ya uongozi niliyopata,”
Ndani ya halmashauri ya serikali ya kijiji cha Ololosokwani, mraghbishi huyu amechaguliwa kuwa mmoja kati ya wajumbe 9 wanaounda kamati ya elimu. Akiwa kama mjumbe wa kamati hiyo, anafafanua majukumu yake:
“Moja ya jukumu la kamati yetu ni kusimamia upatikanaji wa ada kwa wanafunzi. Kijiji chetu kinapata fedha kutoka idara ya wanyama pori, ambazo ndiyo hutumika kulipia ada za watoto kwenye kijiji chetu.”
Katika kijiji cha Ololosokwani, kila mtoto anapata fursa ya kupata elimu kwa kulipiwa gharama stahiki kuanzia ngazi ya shule ya msingi hadi kiwango cha shahada ya uzamili.
Serikali ya kijiji hiki imejiwekea utaratibu wa kuhakikisha walengwa wanapata huduma husika na kuhakikisha wanatoa taarifa za kweli.
Akifafanua utaratibu huo, mwenyekiti wa kijiji cha Ololosokwani, Kerry Dukonya anasema:
“Jambo la kwanza ni mwanafunzi kutafuta shule na baada ya kupata atatakiwa kuleta fomu na barua ya kukubaliwa kujiunga na shule husika kama kielelezo. Barua hiyo ndio inayotoa maelezo ya ada na mahitaji mengine ya shule.  Ndipo hapo kamati inafuatilia na kuhakiki taarifa, kabla ya kupitishwa na halmashauri ya serikali ya kijiji.”
Waraghbishi wamekuwa msaada mkubwa katika kutimiza majukumu ya serikali kwa kuwa mstari wa mbele katika harakati za kuhimiza wananchi kutambua haki na majukumu yao katika kijiji. Na viongozi wa kijiji wanakiri kwamba waraghbishi wamekuwa wakishawishi wananchi kuchukua hatua mbalimbali, ikiwamo kuwawajibisha viongozi wazembe.

Akifafanua hali hiyo na jinsi viongozi wanavyojisikia iwapo uraghbishi utagusia masilahi yao hasa linapokuja suala la kuwawajibisha, mwenyekiti wa kijiji anasema:
“Sisi kama viongozi, tunamruhusu Kootu kwenda popote na akinamama hawa wamekuwa mstari wa mbele kutukosoa na kutukumbusha majukumu yetu. Hii ni njia mojawapo ya kuruhusu haki itendeke. Hivyo ni haki ya wananchi kujua mapato na matumizi ya serikali yao ambayo sisi kama viongozi  tunayasimamia.”
Kama mwanamke ndani ya halmashauri ya serikali ya kijiji, amepatiwa jukumu maalumu la kuhakikisha wanawake na wasichana wanashiriki katika shughuli za maendeleo.  Akifafanua jambo hilo, mwenyekiti wa Ololosokwani, Kerry alisema:
“Tungependa kuona anakuwa kielelezo cha mwanaharakati mwanamke kutokana na nafasi yake kama mjumbe wa halmashauri ya serikali ya kijiji. Lakini pia wanawake wamekuwa ni kundi la pembezoni, ikiwamo walemavu. Mraghbishi huyu atakuwa mstari wa mbele kuwahamasisha wenzake kutambua umuhimu wa elimu.”
Mraghbishi Kootu Tome (kushoto) akigawa nakala za Riwaya za Chukua Hatua kwa baadhi wa wananchi wa kijiji cha Ololosokwani ikiwa kama sehemu yake ya uraghbishi. (Picha na Kisuma Mapunda)

Mraghbishi Tome, kwa kutumia mbinu za kiuraghbishi, anahakikisha watoto wa kike wanakwenda shule. Katika hili, anaeleza anaeleza mikakati yake:
“Kama mraghbishi, nimepata fursa ya kukutana na akinamama na kuhakikisha watoto wa kike wanapata nafasi za kusoma. Lakini siku zote nimekuwa nikiwataka kuwasiliana na walimu ili watambue changamoto zinazowakabili watoto wao wa kike, hasa kwa wale ambao wapo mashuleni tayari,”
Kwa upande wake, mtendaji wa kijiji Rabia Legula anasema:
“Ninapozungumzia mraghbishi, namaanisha wale wanaohamasisha wananchi kudai haki zao za msingi, ikiwamo kuwawajibisha viongozi. Si hivyo tu, waraghbishi wamekuwa mstari wa mbele kunisaidia masuala yanayohusu wanawake. Kupitia ujuzi wao na kama wanawake waraghbishi tunatoa kipaumbele kwa wanawake.”
Katika jamii ya kimasai ambayo bado wanawake hawajapata nafasi ya kutosha, uwepo wa waraghbishi wanawake umekuwa chachu nzuri ya kuwawezesha wenzao kuongea katika mikutano ya hadhara.
“Tunapenda waraghbishi waendelee kuhamasisha akinamama kuongelea masuala yao katika mikutano ya vijiji. Kwa kutumia nafasi yangu ya utendaji, nitahakikisha natoa fursa kwa waraghbishi hawa kuzungumza kwa uwazi mambo ya  wanawake.”
Kama mjumbe wa halmashauri ya serikali ya kijiji, mraghbishi amekuwa na jukumu la kuhakikisha  wananchi wanahudhuria mikutano ya kijiji.
“Huwa nawahamasisha akinamama wenzangu kuhudhuria mikutano ya kijiji kila tunapokutana kwenye vikundi vyetu vya ushirikiano,” anasema. Mkurugenzi Mtendaji wa PALISEP, Roberth Kamakia,akielezea jambo katika mkutano uliokutanisha waraghabishi toka mikoa ya Arusha ,Simiyu na Shinyanga uliofanyika hivi karibuni 

Awamu ya pili ya mradi wa Chukua Hatua, unalenga kuwawezesha waraghbishi wa zamani kufundisha waraghbishi wapya waliochaguliwa na serikali za kijiji, kama anavyoelezea Mkurugenzi Mtendaji wa PALISEP, Roberth Kamakia,

“Tuliwaandikia barua serikali za vijiji tukiwaomba watuchagulie watu wanaofaa kuwa waraghbishi. Tuliwapa sifa za watu hao na mwongozo wa jinsi ya kuwachagua.
Baada ya waraghbishi hao kuchaguliwa, waliandaliwa kwa ajili ya mafunzo ya pamoja ikijumuisha wale wa zamani na wapya. Na baada ya hapo waraghbishi wa zamani walikuwa na jukumu la kuwafundisha wenzao jinsi ya kufanya uraghbishi.
Katika mafunzo hayo, walikumbushwa maana ya uraghbishi na sifa za uraghbishi. Ndipo wale waraghbishi wa zamani, akiwamo Kootu walipopewa jukumu la kufundisha wenzao kwa kutumia uzoefu waliopata wa uraghbishi.
Akielezea jinsi wao waraghbishi wa zamani wanalivyofundisha waraghibishi wapya wanaotoka vitongoji vya Ololosokwani na Njoroi, Kootu anasema:
“Tulikaa pamoja PALISEP na kuwafundisha waraghbishi wapya. Kwa upande wangu, nilifundisha maana ya uraghbishi na kutoa maana ya mtu anayeitwa mraghbishi Kazi yake ni kuwahamasisha wananchi. Mraghbishi anatakiwa awe na sikio kubwa la kusikiliza, mdomo mdogo wa kuongelea na macho makubwa ya kuangalia,” anasema.  
Kootu si mraghbishi pekee aliye kwenye halmashauri ya serikali ya Kijiji cha Ololosokwani, mraghbishi mwingine ni Noorkishili Naing’isa ni mjumbe wa halmashauri na  kamati ya fedha. Ni dhahiri waraghbishi wanawake wameendelea kuwa chachu ya maendeleo kutokana na utendaji wao mzuri kwenye serikali za kijiji. Hivyo ni jukumu letu sote kuhakikisha harakati hizi za uraghbishi ndani ya halmashauri za vijiji vyetu zinaungwa mkono.


                           CHANZO ; MWANAHARAKATI MZALENDO BLOG 


No comments:

Post a Comment