Social Icons

IMETOSHA

IMETOSHA

Thursday, January 21, 2016

AUAWA KISA LAKI 7, MOSHI


 Wakazi wa Kijiji cha Kindi Tarafa ya Kibosho Wilayani Moshi Mkoani Kilimanjaro, wakiwa kwenye  mazishi ya marehemu Eugeni Mboro mfanyabiashara wa mahindi aliyeuawa kwa kukatwa na shoka nyuma ya shingo yake na kuporwa sh700,000.
Paroko wa Kanisa Katoliki Parokia ya Anthony wa Padua, Kijiji cha Kindi Tarafa ya Kibosho Wilayani Moshi Mkoani Kilimanjaro, Padri John Senya, akiongoza ibada ya mazishi ya marehemu Eugeni Mboro mfanyabiashara wa mahindi aliyeuwa kwa kukatwa na shoka nyuma ya shingo yake na kuporwa sh700,000.
Na Woinde Shizza, Moshi

WANANCHI wa Kijiji cha Kindi Wilaya ya Moshi Mkoani Kilimanjaro wamesema ili kukomesha mauaji ikiwemo tukio la kukatwa na shoka nyuma ya shingo kwa Eugeni Mboro kwa sababu ya sh700,000 wauaji hao wachukuliwe hatua.

Mkazi wa kijiji hicho Richard Massawe alisema jana chanzo cha kifo hicho ni sh700,000 alizokuwa nazo Mboro baada ya kuuza mahindi yake ndipo baadhi ya watu aliokuwa nao kupanga njama za kumuua na kuzichukua fedha hizo.

“Tunaomba serikali ichukue hatua kwani Mboro alikuwa ni mjasiriamali mdogo anayeibukia hapa Kindi na asiyekuwa na tatizo na mtu ila hao kina Gasto na Kisimati walishikwa na tamaa ya kumuua ili wachukue pesa,” alisema Massawe.

Mjomba wa marehemu Joseph Mwacha aliiomba serikali kuchukua hatua kwa wahusika wote wa mauaji hayo kwani ndugu yao hakudhulumu kitu cha mtu ila ni roho mbaya zilizosababisha kifo hicho na kumpora sh700,000 zake.

Hata hivyo, akiongoza ibada ya mazishi hayo, Paroko wa kanisa katoliki parokia ya Anthony wa Padua, Padri John Senya, aliwataka wakazi wa eneo hilo kupiga vita matukio ya uuaji kwa mtu asiye na hatia.

“Tunapaswa kubadiliwa jamani watu Kindi kwani itafikia siku mtu ukisema umetoka Kindi watu watakuangalia mara mbili mbili hivyo unasema umetoka Kibosho badala ya kutaja eneo hili tulipozaliwa,” alisema Padri Senya.

Kwa upande wake, kamanda wa polisi mkoani Kilimanjaro, Ramadhan Mungi alisema mwili wa Mboro ulikutwa kwenye shamba la Michael Makabili huku akiwa na jeraha nyuma ya shingo lililotokana na kupigwa na kitu chenye ncha kali.

Kamanda Mungi alisema pia marehemu aliibiwa fedha zake sh700,000 na wanawashikilia watuhumiwa wawili kwa uchunguzi akiwemo Gasto Costa (25) mkazi wa kijiji cha Kindi na mtu mwingine ambaye hakumtaja jina lake.

“Huyu mtuhumiwa Gasto tulifanya upekuzi kwenye nyumba yake na kukuta kuna shuka lenye damu na nguo za marehemu Mboro ila huyu mtuhumiwa mwingine bado tunaendelea na uchunguzi juu yake,” alisema Kamanda Mungi.

No comments:

Post a Comment