Watu wanaosadika kuwa ni majangili wameitungua kwa risasi helikopta ya doria katika pori la akiba la Maswa liliko wilayani Meatu Mkoani Simiyu, kusini mwa hifadhi ya taifa ya Serengeti.
Majangili hao wanadaiwa kumpiga risasi na kumuua rubani wa ndege hiyo, George Goer ambaye ni raia wa Uingereza na kusababisha helkopita hiyo kupoteza muelekeo na kuanguka.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe amelaani tukio hilo na kuahidi kuwasaka kwa nguvu zote majangili na kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria.
“Vita hii tutapambana nao mpaka tutawashinda. Hizi maliasili ambazo tunazo ni mali ya Watanzania wote,” alisema Maghembe alipofika kwenye eneo la tukio na kushuhuda helkopta hiyo iliyotunguliwa.
“Hawa ni watu wenye ubinafsi wa hali ya juu, kama watu ambao wanaingiza madawa ya kulevya. Kwamba wanataka kutumia maliasili hizi kwa faida zao binafsi,” aliongeza.
Waziri Maghembe pia aliwaonya watumishi wa umma wanaoshirikiana na wahalifu katika matukio
ya kijangili kuwa hatua kali zitachukuliwa dhidhi yao.
Tukio hilo limetajwa kuwa tukio jipya kabisa la kijangili kufanyika katika kipindi cha hivi karibuni.
No comments:
Post a Comment