Social Icons

IMETOSHA

IMETOSHA

Thursday, January 14, 2016

Wizara ya Nisahati na Madini yatoa ufafanuzi mradi wa umeme wa Kinyerezi II‏

Mkuu wa Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Nishati na Madini, Badra Masoud, akizungumza na waandishi wa habari, Dar es Salaam, wakati alipokuwa akitoa ufafanuzi kuhusu mradi wa umeme wa Kinyerezi Awamu ya Pili, akielezea kuhusu habari zilizoandikwa kimakosa katika moja ya magazeti ya kila siku nchini jijini leo. Kulia ni Ofisa Habari Mwandamizi wa Idara ya Habari-Maelezo, Magreth Kinabo. (Picha na Kassim Mbarouk-www.bayana.blogspot.com)


Na Nyakongo Manyama- MAELEZO
14/01/2016
WIZARA ya Nishati na Madini  imekanusha habari iliyopotosha umma kuhusu   mradi wa umeme wa Kinyerezi II kuwa bado haujaanza na gharama zilizoandikwa si za kweli.

Wizara hiyo imekanusha habari hiyo, iliyoandikwa katika gazeti la Mtanzania la leo Januari 14, mwaka huu toleo namba8063,  lenye kichwa cha habari “ Harufu ya Jibu Mradi wa Umeme.”


Habari hiyo  ambayo ilieleza kwamba mradi huo ulizinduliwa na Rais Mstaafu wa  Serikali ya Awamu ya Nne, Mhe. Dkt.Jakaya Kikwete uligharimu Sh. trilioni 1.6 na kwamba fedha za ujenzi wa mradi huo zimetokana ubia kati ya Serikali ya Tanzania na Japan,ambapo Serikali ya Tanzania itakuwa na hisa ya asilimia 40 na kampuni ya SUMITOMO ya Japan asilimia 60. 

 Aidha habari hiyo ilidai kuwa Serikali inachangia fedha za ndani kwa asilimia 12 na zilizobaki zikiwa na mkopo kutoka benki ya Japan na kwamba gharama za mradi huo ziko juu ikilinganishwa miradi mingine akitolea mfano Kampuni ya TALLAWARA Power Station ya nchini Australia anayodai ilitaka kujenga mradi huo kwa dola za Marekani milioni 350.

Hayo yamesemwa leo na  Mkuu wa Mawasiliano Serikali  wa wizara hiyo,  Badra  Masoud alipokuwa akizungumza  na waandishi wa habari kuhusu habari hiyo katika ukumbi wa Idara ya Habari (MAELEZO) jijini Dar es Salaam. 

“Serikali  ya Tanzania  iliingia makubaliano na Serikali ya Japan  ya mkopo wa masharti nafuu  wa dola za Marekani  milioni 292  kwa ajili ya kutekeleza mradi wa  kuzalisha umeme wa Megawati 240 utakaojengwa na kampuni ya SUMITOMO kama mkandarasi wa “EPC contractor” na sio kama mbia wa Serikali yaTanzania kama ilivyodaiwa.

“Mradi huo unamilikiwa na Serikali kwa asilimia 100 kupitia TANESCO  na hakuna mwekezaji mwingine katika mradi huo.Hivyo si kweli kwamba Serikali ya Tanzania na kampuni ya SUMITOMO zinawekeza kwa ubia wa asilimia 40 (kwa Serikali ya Tanzania) na asilimia 60 kwa SUMITOMO. Kwa maana hiyo, hatutauziwa umeme utakaozalishwa na mradi huu kwani ni mali yetu na hakuna gharama yoyote ya ziada kama alivyodai mwandishi wa habari hiyo,” alisema Badra.

Aidha Badra alisema mwandishi huyo alidai kwamba mradi huo ulizinduliwa na Rais wa  Serikali ya Awamu ya Nne Mhe. Dkt. Jakaya Kikwete, wakati ni  kwamba mradi huo haujazinduliwa bado na sasa upo katika maandalizi ya kuwekwa katika jiwe la  msingi.

 Akizungumzia kuhusu gharama za mradi huo, alieleza kuwa unatekelezwa kwa dola za Marekani milioni 344 sawa na Sh. bilioni 740 zikiwa ni mkopo wa masharti nafuu wa asilimia 85 sawa  na dola za Marekani 292 na mchango wa Serikali ya Tanzania kwa asilimia 15 sawa na dola za Marekani milioni 52 na sio asilimia 12 kama ilivyodaiwa na mwandishi huyo. 
“Mwandishi wa habari hii amejaribu kufananisha uwekezaji huu na uwekezaji wa TALLAWARA Power Station ya Australia na kudai kwamba gharama yake ingekuwa ndogo kuliko gharama ya mradi huu. 

Taarifa hii haina ukweli wowote kwa sababu gharama ya dola milioni 344 zinazotarajiwa kutumika mkatika mradi huu iko chini kuliko dola milioni 350anazodai mwandishi kwamba zingetumiwa na kampuni TALLAWARA.

“Aidha, kampuni ya TALLAWARA haijawahi kuomba au kuonesha nia ya kuwekeza katika mradi wowote wa kufua mradi wa umeme nchini. Pia ni muhimu ifahamike kwamba makubaliano ya mkopo huu yalikuwa yanakwenda sambasamba na utekelezaji wa mradi wenyewe (EPC with Financing).  
   
Badra aliongeza kwamba pamoja na kwamba gharama za uwekezaji wa mradi huo wa kwanza wa aina ya “Combined Cycle” nchini zinawiana na gharama za miradi mingine ya aina hiyo duniani, gharama za uwekezaji zinaweza kutofautiana kutegemeana na mazingira ya nchi na nchi, teknolojia iliyotumika na aina ya mitambo.

Hivyo sio suala la kulinganisha gharama ya mradi mmoja na mwingine.

Wizara hiyo imeshauri waandishi wa habari kufuata miiko na maadili ya uandishi wa habari kwa kuandika habari  zenye ukweli na sahihi na zilizozingatia pande zote mbili kwa kuwa ipo na tayari kujibu maswali ya waandishi wakati wowote.

No comments:

Post a Comment