Social Icons

IMETOSHA

IMETOSHA

Wednesday, February 24, 2016

CUF Watoa Tamko Zito Kuhusiana Na Kukamatwa Kwa Mwanamkakati wa Maalim Seif


TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Wiki iliopita, mnamo tarehe 16 Februari, 2016, aliyekuwa mjumbe wa Timu ya Kampeni ya Chama Cha Wananchi (CUF), Ndugu Mohamed Ahmed Sultan Al-Mugheiry (maarufu kwa jina la Eddy Riyami), alipokea barua ya wito kutoka kwa Jeshi la Polisi Zanzibar ikimtaka kufika Makao Makuu ya Polisi, Ziwani, Zanzibar siku inayofuata, yaani tarehe 17 Februari, 2016, saa 2 asubuhi kwa kile kilichoelezwa kwamba “kuna mambo muhimu yanayomhusu” ambayo walitaka kuzungumza naye.


Bila ya kukosa, Eddy Riyami aliitikia wito huo na kufika Makao Makuu ya Polisi, Zanzibar na kuonana na SSP Simon S. Pasua wa Idara ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai (CID). 

Hata hivyo, hakuhojiwa na badala yake alipewa simu na kutakiwa azungumze na Naibu Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai, Bw. Salum Msangi ambaye alimwambia arudi tena Jumatatu, tarehe 22 Februari, 2016.

Eddy Riyami, akiwa raia mwema, alirudi tena jana kama alivyoagizwa. Alipofika hapo alihojiwa na Polisi na baadaye mwanasheria aliyefuatana naye akatakiwa kutafuta wadhamini wawili watakaomdhamini hadi atakapoitwa tena. 

Wakati mwanasheria wake aliporudi na wadhamini, akaelezwa kwamba Polisi imebadili uamuzi wake na imeamua kumuweka ndani hadi leo, tarehe 23 Februari, 2016. 

Mwanasheria na familia yake wakatakiwa kwenda tena Makao Makuu ya Polisi hiyo leo, saa 3 asubuhi. Walipofika leo asubuhi, wakaambiwa kwamba DCI kaacha maagizo kuwa suala la Eddy Riyami liachwe kwanza na wao warudi tena saa 6 mchana.

Hadi tunapotoa taarifa hii, hakujapatikana maelezo yoyote ya msingi juu ya kinachoendelea na wala Eddy Riyami hajafikishwa Mahakamani kusomewa mashtaka yoyote.

La ajabu zaidi, ni kwamba hata mke wake alipofika kituo cha polisi cha Madema anakoshikiliwa kwa ajili ya kwenda kumuona, hakuruhusiwa kumuona. 

Kutokana na mwenendo huu, Chama Cha Wananchi (CUF) kinalichukulia suala hili kwamba ni mwendelezo wa vitendo vya unyanyasaji wa kisiasa dhidi ya wapinzani wa CCM, vitendo ambavyo tunaamini vinafanywa kwa shinikizo la wanasiasa.

Itakumbukwa kwamba kwa muda mrefu tokea wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu wa Oktoba 25, 2015 tumekuwa tukitoa tahadhari za kuwepo mipango ya kuwakamata viongozi wa CUF na wanaharakati wengine ili kufanikisha malengo ya kisiasa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Tuna kila sababu ya kuamini kwamba hatua ya kumkamata Eddy Riyami na kumuweka ndani bila ya kumfikisha Mahkamani ni utekelezaji wa mipango hiyo. La si hivyo, ikiwa Eddy Riyami ametenda kosa basi angelishafikishwa Mahkamani ndani ya muda wa saa 24 tokea kukamatwa kama sheria inavyotaka.

Chama Cha Wananchi (CUF) kinalitaka Jeshi la Polisi kuacha kutumiwa na kutumika kisiasa kufanikisha malengo ya kisiasa ya CCM. 

Tunashangazwa kwamba siku zote wanaoitwa kuhojiwa, kukamatwa na kuwekwa ndani ni wanasiasa wa vyama vya upinzani na wanaharakati wengine lakini hatujawahi kushuhudia viongozi wa CCM kuitwa kuhojiwa, kukamatwa na kuwekwa ndani.

CUF imetoa taarifa kadhaa kwa Jeshi la Polisi zinazohusu matamshi na vitendo vya viongozi wa CCM vyenye mwelekeo wa uhalifu lakini hakuna hatua zozote zilizochukuliwa. Hizo ni dalili za waziwazi za Polisi kutumiwa na kukubali kutumika kisiasa.

Tunalitaka Jeshi la Polisi iwapo kweli lina kesi dhidi ya Eddy Riyami basi limfikishe Mahkamani haraka ili hatua za kisheria zifuate mkondo wake.

Na iwapo hawana kesi, basi wamwachie huru mara moja. Umefika wakati wa Jeshi la Polisi kufanya kazi zake kitaalamu kama sheria na kanuni zao zinavyoagiza badala ya kuwatumikia wanasiasa wa CCM.

HAKI SAWA KWA WOTE
HAMAD MASOUD HAMAD
KAIMU MKURUGENZI WA HABARI NA MAWASILIANO NA UMMA – CUF
23 Februari 2016

No comments:

Post a Comment