Kikosi cha Kuzuia Ujangili Kanda ya Magharibi kinamsaka fisi
mmoja kati ya wawili waliowashambulia Samwel Gamalaya na kusababisha kifo chake
na kumjeruhi Kusekwa Ngeleja wakati wakikata kuni katika pori lililopo
Kitongoji cha Isukamahela Manispaa ya Tabora.
Fisi hao wawili walimshambulia kwa kumng’ata Gamalaya maeneo
mbalimbali ya mwili na kusababisha kifo chake, huku wakimjeruhi Ngeleja mikono
na miguu.
Kamanda wa Kikosi cha Kuzuia Ujangili Kanda ya Magharibi,
Charles Msilanga alisema jana (juzi) kuwa baada ya polisi kumpiga risasi fisi
mmoja na kumuua, mwingine alikimbia.
Alisema wanaendelea kumsaka fisi huyo ili kuzuia madhara
zaidi kwa wakazi wa kitongoji hicho.
“Fisi aliyekimbia anaweza kuleta madhara kwa watu na ndiyo
maana tunamsaka kwa udi na uvumba,” alisema Msilanga.
Mwenyekiti wa kitongoji hicho, Iddi Cheyo alisema Gamalaya
alifariki dunia baada ya kukaa muda mrefu bila matibabu tangu aliposhambuliwa
na fisi hao.
Baadhi ya wakazi wa kitongoji hicho, Sophia William na Juma
Kapambala walisema tukio hilo limewastaajabisha kwani kwa miaka mingi wanafanya
shughuli zao ndani ya msitu huo bila kushambuliwa na wanyama.
“Tunafanya shughuli zetu katika msitu huu kwa miaka mingi
bila kuvamiwa, lakini hatujaona mnyama kuingia eneo hilo,” alisema Sophia.
MWANANCHI
No comments:
Post a Comment