Social Icons

IMETOSHA

IMETOSHA

Tuesday, February 2, 2016

WAFUNGWA MIAKA MITANO JELA KWA KUSAFIRISHA WAHAMIAJI HARAMU

Wahamiaji haramu waliowahi kukamatwa na mamlaka. Picha na Maktaba

Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Iringa, imewahukumu kifungo cha miaka mitano jela, dereva Hance Mwakyoma (28) na msaidizi wake, Alex Adam (32) kwa kosa la kusaidia kuwasafirisha raia wa kigeni walioingia nchini bila kibali.
Dereva huyo aliyekuwa akiendesha gari aina ya Scania lililotumika kuwasafirisha wahamiaji haramu hao ambao ni raia wa Ethiopia, ameamriwa pia kulipa faini ya Sh1.5 milioni.
Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Mkoa wa Iringa, Andrew Scout alisema aliwahukumu pia raia 83 wa Ethiopia adhabu ya kifungo cha miaka mitatu jela au kulipa faini ya Sh1 milioni.
Akisoma hukumu hiyo, Hakimu Scout alisema ameridhika na maelezo yaliyotolewa na Wakili wa Serikali pamoja na vielelezo likiwamo gari lililotumiwa na watuhumiwa hao kusafiri kutoka Kongowe kwenda Mbeya.

“Baada ya kupokea maelezo kutoka kwa watuhumiwa walioniomba niwasamehe na maelezo kutoka kwa wakili wa Serikali aliyeomba mahakama itoe adhabu kali kwa kuwa kosa hili hujirudia kila mara, nimeamua kuwapa adhabu hii ili iwe fundisho kwa wengine wenye nia ya kufanya kosa kama hili,” alisema Hakimu Scout.
Baada ya hukumu hiyo kutolewa, raia hao wa Ethiopia waliangua kilio mahakamani hapo na kusababisha umati kujaa katika mahakama hiyo.
Awali, akiwasomea mashtaka watuhumiwa hao baada ya kukiri kosa lao, Wakili wa Serikali kutoka Idara ya Uhamiaji, Godfrey Ngwijo aliiambia mahakama kuwa Januri 16, mwaka huu, watuhumiwa walikutwa kwenye gari aina ya Scania eneo la Ruaha Mbuyuni wakisafiri kutoka Kongowe mkoani Dar es Salam kwenda nchini Malawi kinyume cha Sheria ya Uhamiaji ya Mwaka 2002 iliyofanyiwa marejeo mwaka jana.

No comments:

Post a Comment