Aliyekuwa mwakilishi wa CCM wa jimbo la Kiembe Samaki,
Mansour Yusuf Himid, ametangaza kukihama chama hicho na kujiunga na Chama cha
Wananchi (CUF).
Himid aliyewahi kuwa Waziri mwandamizi chini Serikali ya
Umoja wa Kitaifa Zanzibar (SUK) chini ya Rais Ali Mohammed Shein na hapo kabla
chini ya Rais Mstaafu wa Amani Karume, alifukuzwa uanachama wa CCM Agosti 26,
mwaka jana kwa madai ya kukisaliti chama chake.
Himid anayedaiwa kuwa ni shemeji yake Rais Karume, baada ya
kuweka bayana azma hiyo, alisema katika uchaguzi mkuu wa mwakani anakusudia
kugombea kiti cha jimbo hilo kupitia CUF.
Akizungumza katika mkutano wa hadhara wa CUF mjini hapa
mwishoni mwa wiki, alisema atawashauri vijana wampigie kura Katibu Mkuu wa CUF
ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif
Hamad,ili awe Rais wa Zanzibar katika uchaguzi mkuu wa mwakani.
“Mimi ni mpenzi wa Maalim Seif Sharif na kura yangu anayo na
nitashirikiana na wezangu kuzitafuta kura za ziada ili awe Rais wa Zanzibar,
“alisema Himid.
Alieleza kuwa bidhaa zikiwa nyingi sokoni mteja ana haki ya
kuchagua iliyo bora, hivyo ana imani kuwa CUF ndilo kimbilio la Wazanzibari ili
kuifanya nchi hiyo iwe na mamlaka kamili.
Alisema moja ya sababu ya kufukuzwa CCM ni kusema ukweli na
kusimamia maridhiano ya wananchi kwa kutaka muundo wa serikali tatu na kusema
Muungano uliopo wa serikali mbili hauna heshima kwa Wazanzibari na taifa lao.
“Mimi nisiwe kigeugeu, nasema kuwa Muungano huu hauna
heshima hata kidogo, Zanzibar tunahitaji mamlaka kamili ili kujiendesha
kiuchumi,” alisema Himid na kuongeza kuwa Muungano wa nchi na watu siyo mbaya,
lakini muundo uliopo wa serikali mbili haufai kwani Zanzibar itaendelea kuwa
mtumwa chini ya muundo huo.
Katika mkutano huo uliofanyika jimboni Mji Mkongwe na kuhudhuriwa
na umati wa wafuasi ukiambatana na mbwembwe na nderemo hasa baada ya Himid
kupanda jukwaani kwa mara ya kwanza kuwasalimia wananchi, uwanja ulisisimka kwa
kupiga kelele za kauli mbiu ya CUF ‘ya haki sawa kwa wote.’
Mwanachama huyo mpya alidai kutimuliwa uanachama na Kamati
Kuu ya CCM kumetokana na msimamo wake ambao chama hicho kilisema kuwa ulikwenda
kinyume na sera na taratibu inazosimamia.
Kabla ya hatua hiyo alikuwa anatoa kauli mbalimbali za
kutaka Zanzibar imiliki rasilimali zake hasa gesi na mafuta badala ya kuwa
jambo la Muungano.
Aidha, alisimama kidete kutaka muundo wa Muungano wa mkataba
ambao ulikuwa msimamo wa CUF, ingawa chama hicho hivi sasa kimejielekeza
kutetea muundo wa serikali tatu uliopendekezwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba
iliyokusanya maoni chini ya uenyekiti wa Jaji Joseph Warioba.
Himid alikuwa mwakilishi wa jimbo la Kiembe Samaki kwa miaka
minane ambapo alichaguliwa mwaka 2005 kwa kupata kura nyingi, lakini Agosti
mwaka jana alifukuzwa CCM.
Kabla ya kufukuzwa uanachama alipata kuwa Waziri wa Ardhi,
Makazi, Maji na Nishati kuanzia mwaka 2005 hadi 2010 na kuchaguliwa tena kuwa
Waziri wa Kilimo na Maliasili mwaka 2010 hadi 2013 alipoondoshwa kwenye nafasi
hiyo kuwa Waziri asiyekuwa na Wizara Maalum kwa muda wa miezi mitatu hadi
aliopofukuzwa CCM.
Mwakilishi wa Jimbo la Mji Mkongwe, Ismail Jussa Ladhu,
katika mkutano huo alisema kiu ya Wazanzibar ni mamlaka kamili ya dola.Alisema
maridhiano ya SUK hayakuwa tu kuwaunganisha Wazanzibari, lakini pia lengo
lilikuwa kuyarejesha mamlaka kamili ya Zanzibar.
“Ingekuwa viongozi wote wa SUK wangeshirikiana mamlaka
kamili ya Zanzibar ingepatikana,”alisema Jussa.
Alisema ili mamlaka kamili ya Zanzibar ipatikane ni mpaka
Maalim Seif awe Rais wa Zanzibar na ana imani kuwa dawa ya hilo karibu
litapatiwa ufumbuzi ambapo 2015 atakuwa Rais.
Akizungumzia kuhusu mchakato wa katiba, Jussa alisema
hawatakubali rasimu ambayo haitazingatia matakwa ya Wazanzibari ambayo ni
muundo wa serikali tatu ili bendera ya Zanzibar ipepee katika Umoja wa Mataifa
(UN).
Pia alisema suala la uraia na uhamiaji Zanzibar ni muhimu
kwani ni kisiwa hivyo lazima kuwe na udhibiti wa wageni kutoka nje ya Zanzibar
na kila Mzanzibari kuwa na paspoti ya nchi hiyo.
ALIVYOFUKUZWA
Agosti 16, mwaka jana Himid alivuliwa uanachama wake na
Kamati Kuu Maalum ya Zanzibar iliyokaa chini ya Rais wa Zanzibar na Makamu
Mwenyekiti wa chama hicho, Dk. Ali Mohamed Shein..
Agosti 26, mwaka jana Halmashauri Kuu (NEC) ya CCM ikikutana
mjini Dodoma iliridhia maamuzi ya Kamati Kuu maalum ya Zanzibar ya kumvua uanachama baada ya kusikiliza na kuridhia
tuhuma dhidi yake kama zilivyokuwa zimekwisha kuamulia Zanzibar.
TUHUMA MAHUSUSI
Katibu wa NEC Itikadi na Unezi wa CCM, Nape Nnauye alidai
Himid alishindwa kusimamia malengo ya CCM na kutekeleza masharti ya uanachama.
Nape alitaja tuhuma nyingine ni kushindwa kutekeleza wajibu
wa mwanachama na kukiuka maadili ya kiongozi wa CCM.
Tuhuma nyingine ni kuikana Ilani ya CCM ya uchaguzi Mkuu wa
CCM wa mwaka 2010-2015 na kuisaliti CCM.
MANSOUR NI NANI HASA
Mansour aliteuliwa kuwa mjumbe wa Baraza la Wawakilishi na
Rais Karume mwaka 2000 na kuteuliwa kushika wadhifa wa Naibu Waziri wa Maji,
Nishati Ujenzi na Ardhi hadi mwaka 2005.
Mwaka 2005 alichaguliwa kuwa Mwakilishi wa Kiembe Samaki
kupitia CCM, nafasi ambayo amedumu nayo hadi sasa. Mwaka huo aliteuliwa na Rais
Karume kuwa Waziri wa Maji, Nishati Ujenzi na Ardhi hadi mwaka 2010.
Kati ya 2005 -2010 alikuwa Mweka Hazina wa CCM Zanzibar wadhifa ulimpa fursa ya kuwa Mjumbe wa NEC na
Kamati Kuu ya CCM. Mwaka 2010 hadi mwaka 2012, alikuwa Waziri wa Kilimo na
Rasilimali.
Ilipofika 2009 alikuwa mstari wa mbele kuushutumu Muungano
kuwa ni chanzo cha kudorora kwa Zanzibar huku akiendesha kampeni juu ya suala
la mafuta kutokuwa la Muungano.
Katika uchaguzi wa mwaka jana ndani ya CCM, Mansour
hakugombea nafasi yoyote ndani ya CCM.
Aidha, alihudumu kama mjumbe wa Baraza la Biashara la
Zanzibar kati ya mwaka 2002 hadi 2012.
Kutokana na misimamo yake ndani na nje ya chama na Serikali,
Oktoba 15, 2012, Dk. Shein ilifuta uteuzi wa Mansour kama waziri hivyo kubakia
kuwa mjumbe wa Baraza la Wawakilishi hadi alipofukuzwa mwaka jana.
Mansour ni mwanasiasa na mfanyabiashara aliyezaliwa Novemba
3, 1967 kisiwani Unguja. Alisoma masomo yake ya msingi na sekondari nchini
India kati ya mwaka 1976 na 1987.
Kabla ya kuingia rasmi katika siasa mwaka 2000, aliteuliwa
kuwa mjumbe katika Baraza la Wawakilishi na alijihusisha katika biashara ya
hoteli.
Mwanasiasa huyo ni mtoto wa Mkuu wa Kwanza wa Jeshi la
Zanzibar baada ya Mapinduzi, Brigedia Jenerali Yussuf Himid.
Amekuwa akisimamia maridhiano ya Wazanzibari na Umoja wa
Kitaifa akiwa mmoja wa wajumbe sita wa Kamati ya Maridhiano aliyoshiriki
kikamilifu kuyaanzisha mwaka 2009.
Pia ni miongoni mwa Wazanzibari walio mstari wa mbele
kutetea muundo wa Muungano, utakaoipa Zanzibar mamlaka kamili ya dola.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment