UONGOZI wa Simba umewasimamisha wachezaji Haruna Moshi 'Boban' na
Kelvin Yondani kutokana na kuchoshwa na vitendo vyao vya utovu wa
nidhamu.
Habari za ndani ambazo Mwananchi imezipata zinasema
Moshi na Yondan tayari wameshaandikiwa barua ya kusimamishwa kwa madai
wachezaji hao wamekuwa wakijiona kuwa ni bora zaidi na hawaudhurii
mazoezini.
"Boban anajiona yeye ni staa zaidi hajatokea na wala
hajapangwa mechi ya Mtibwa, Polisi Dodoma, Kagera Sugar kwa sababu
hafanyi mazoezi, hakuna 'Super Star Simba' njoo mazoezini utapangwa,
hata hivyo uongozi umechoshwa na tabia zake umeamua kumfungashia
virago,"kilidai chanzo hicho.
Mbali na Boban ambaye alikatisha
mkataba wake na timu ya Gefle IF ya nchini Sweden, pia Simba
imemfungashia virago beki wake Yondani ambaye hajaonekana kwenye
mazoezi tangu mechi yao na Kagera Sugar na ile ya Toto African
iliyofanyika mkoani Mwanza.
Chanzo hicho cha habari kimeeleza kuwa tayari wachezaji hao wameshaandikiwa barua za kutimuliwa ndani ya klabu hiyo.
Simba
inayofundishwa na Mganda Moses Basena itawajadili wachezaji, Emmanuel
Okwi na Ulimboka Mwakingwe walioshindwa kufanya mazoezi na timu hiyo
tangu Jumatatu.
Katika hatua nyingine chanzo hicho kilidai kuwa
Okwi aliyeachwa kwenye kikosi cha Uganda hajatokea mazoezini kwa
kisingizio kuwa anaumwa malaria, lakini uongozi umebaini haumwi,
mwenzake Ulimboka alidai amefiwa na baba yake mdogo.
"Kilichopo
hapo ni kwamba Ulimboka umri umeenda sasa hivi mazoezi wanayofanya ni
ya nguvu zaidi na sio chini ya masaa matatu, sasa Ulimboka anaogopa si
mnakumbuka Zanzibar alichanika nyama ya paja kwa sababu ya mazoezi
magumu, hivyo anavuta vuta mpaka ikifika mazoezi mepesi ndio aje,
hakuna cha msiba wala nini,"alidai kiongozi huyo kwa sharti la
kutotajwa jina.
"Kwa upande wa Okwi safari hii hajaitwa timu ya
Taifa, yupo hapo Chang'ombe anajifanya anaumwa hana cha kuumwa wala
nini tumeshawaandikia barua wote kuwaambia wajieleze ni kwa nini
tusiwape adhabu,"alisisitiza na kuongeza.
"Sasa hivi mwalimu
anachofanya Simba kubwa mazoezi wanafanya na timu B lengo ni kuwapa
nafasi zaidi timu B ili akija fanya mabadiliko watu wasishangae wala
kulaumu, hatuwezi fuga maradhi kila siku, mwisho wa siku yatakuja
kutuua.
Akizungumzia suala hilo msemaji wa Simba, Ezekiel
Kamwaga alisema,"Taarifa za wachezaji wote tunazo na tunashughulikia
masuala yao,"alisema bila ya kufafanua.
No comments:
Post a Comment