WAZAZI ACHENI KUSEMA UONGO - PINDA

WAZIRI
MKUU Mizengo Pinda amewataka wazazi wenye uwezo wa kulipia watoto wao
katika Vyuo Vikuu waache kusema uongo kwani kwa kufanya hivyo
wanawakosesha watoto wa maskini kupata mikopo wanayostahili.
Ametoa kauli hiyo leo (Jumamosi, Novemba 5, 2011)
wakati akiwahutubia washiriki wa mahafali ya pili ya Chuo Kikuu cha St.
John’s yaliyofanyika kwenye chuo hicho mjini Dodoma. Jumla ya wahitimu
1,002 walitunukiwa vyeti, stashahada, shahada na stashahada za juu
katika fani za theolojia, uuguzi, famasia, sayansi na ualimu, biashara,
uhasibu na fedha, masoko na teknolojia ya habari na mawasiliano.
“Bado
kuna malalamiko nayapata kupitia njia mbalimbali kuhusu utaratibu wa
Bodi ya Mikopo hasa pale watoto wa maskini, tena waliofaulu vizuri
wanapokosa mikopo. Nawasihi wazazi wenye uwezo waache kusema uongo kwa
sababu si busara kuwatumia watoto wao kupata mikopo wakati watoto
wanaostahili wanaikosa…,” alisema.
Alisema wazazi wakiwa wakweli na kuamua kuwalipia watoto wao, fursa za watoto maskini kupata mikopo zitaongezeka.
Alitumia
fursa hiyo kuzungumzia changamoto zinazoikabili Serikali katika
kukabiliana na kasi ya ongezeko la watu na kuonya kuwa linaleta
changamoto kubwa katika utoaji wa huduma za jamii.
“Ongezeko
la watu liko juu sana na kasi yake haioani na ukuaji wa uchumi… ukuaji
huu unaathiri sana nyanja nyingi hasa elimu na ndiyo maana tunakabiliana
na ongezeko la wanafunzi wanaoomba mikopo katika Bodi ya Mikopo kila
mwaka,” alisema.
Alikitaka Chuo Kikuu kikuu cha St. John’s kiweke mikakati maalumu ya kusomesha wanataaluma wake wenyewe kwa sababu utaratibu
wa kuazima wanataaluma kwa njia moja au nyingine unawakwaza wanafunzi
kwani hawapati muda wa kutosha wa kuwasiliana na mwalimu wao.
”Nawasihi
muongeze bidii ya kusomesha wanataaluma wenu kwa kasi ile ile ya
kuongeza wanafunzi katika vyuo vyenu. Kama Taasisi inayojitegemea hamna
budi kusomesha wataalam wenu wenyewe kwa msaada wa Bodi ya Mikopo ya
Elimu ya Juu,” alifafanua.
Akitoa wosia kwa wahitimu, Waziri Mkuu alisema: “Ombi langu kwenu ni kuwa, mkatumie
elimu mliyoipata hapa chuoni kwa manufaa yenu, jamii na Taifa kwa
ujumla. Msianze kwa kujifikiria nafsi zenu, kwani huo ni mwanzo wa
tamaa, uchoyo, dhuluma, rushwa na pengine wizi.”
No comments:
Post a Comment