Anthony Kayanda, Kigoma
POLISI mkoani Kigoma wamelazimika kutumia
mabomu ya machozi kuwatawanya mamia ya wafuasi wa chama cha NCCR Mageuzi
waliokuwa kwenye mkutano ambao ulipaswa kuhutubiwa na mbunge Kigoma
Kusini, David Kafulila.
Habari zilizolifikia gazeti hili
zimeeleza kuwa tukio hilo lilitokea juzi katika Kijiji cha Kazuramimba
ambako Kafulila alikuwa amejiandaa kufanya mkutano wa hadhara na tayari
alikuwa ameanza kuhutubia akiwa kwenye gari na madiwani wawili wa chama
hicho cha upinzani.
Kafulila aliliambia gazeti hili jana kuwa
polisi hao walizuia mkutano wake na kumkamata kwa mahojiano yaliyodumu
kwa takriban dakika 30, kwa madai kwamba mkutano wake haukufuata
taratibu za kuomba na kupata kibali.
Kafulila ambaye yuko mkoani
Kigoma kwa ziara ya kichama, alisema alipofika kijijini hapo alipata
taarifa kwamba polisi wa kituo kidogo kilichopo eneo hilo waliwazuia
viongozi wa NCCR Mageuzi kufanya maandalizi ya mkutano huo.
Alisema
baada ya kusikia uamuzi huo, alilazimisha wafanye mkutano kwa vile yeye
ni mbunge halali wa jimbo hilo la Kigoma Kusini na anapaswa kuzungumza
na wananchi kuelezea utendaji wake wa kazi kwa kipindi cha mwaka mmoja
uliopita.
“Polisi wamenizuia kufanya mkutano wangu na wametumia
nguvu kubwa kututawanya kwa madai kwamba wametumwa na Mkuu wa Polisi wa
Wilaya ya Kigoma (OCD), Japhet Kibona eti sisi hatujatimiza masharti...,
na pia hatujaomba kibali cha kufanya mkutano. Sasa mimi kama mbunge wa
jimbo nazuiliwa kwa nini?," alihoji Kafulila na kuendelea:
"Inawezekana
huyu OCD ananihujumu na tayari nimewaeleza wakuu wake wa kazi kuanzia
IGP, Said Mwema na Waziri wa Mambo ya ndani, Shamsi Vuai Nahodha ili
wajue hujuma ninayofanyiwa na huyu OCD wa Kigoma,"alisisitiza Kafulila.
Kafulila
ambaye hatma ya ubunge wake iko mikononi mwa Mahakama baada ya kuvuliwa
uanachama wa NCCR-Mageuzi, alisema katika sakata hilo walikuwepo polisi
watano waliovurumisha mabomu ya machozi.
Alisema yeye alikamatwa
na kupelekwa kituo kidogo cha Polisi Kazuramimba kwa mahojiano
yaliyodumu kwa zaidi ya nusu saa, kabla ya kuachiwa huru kwa sharti la
kutoendelea na mkutano wa hadhara.
Alisema kuzuiwa mikutano yake
kulianzia Kijiji cha Ilagala ambako hata hivyo anaeleza kuwa mkutano
ulifanyika kwa busara za Kamanda wa Polisi mkoa wa Kigoma, ACP Frasser
Kashai baada ya kuwa umezuiliwa na askari wa Kituo kidogo cha Polisi
Ilagala.
RPC Kigoma
RPC Kashai alipoulizwa kuhusu suala hilo,
alisema kilichotokea ni mbunge huyo kukaidi na kukiuka utaratibu wa
kisheria katika kufanya mikutano yake ya hadhara, ambayo ni pamoja na
kutoa taarifa ya maandishi polisi ili waweze kuandaa ulinzi.
"Sheria
inatamka wazi kwamba, lazima wanaofanya mkutano watoe taarifa polisi
kupitia kwa OCD saa 24 kabla, ili na sisi tujipange kwa ajili ya kuweka
usalama unakuwepo, sambamba na kujiridhisha kama hakuna mkutano mwingine
unaofanyika katika eneo wanalokusudia kufanya mkutano wao," alisema
Kamanda Kashai.
Hata hivyo, alikanusha kutokea vurugu zozote
katika mkutano huo bali ni kitendo cha polisi kuwazuia wananchi
wasihudhurie kutokana na utaratibu kukiukwa, jambo ambalo haliwezi
kuvumiliwa na Polisi.
"Kafulila anafanya mambo ya ajabu sana kwa
sababu siamini kwamba, hajui sheria na utaratibu wa kufanya mikutano ya
hadhara, yeye ana tabia ya kuleta barua siku hiyo hiyo ya mkutano,
lakini sheria inaeleza bayana ni lazima taarifa iletwe saa 24 kabla,"
alisisitiza Kashai.
Alisema hadi jana hakuwa amepata taarifa
zozote za kuwepo kwa watu waliojeruhiwa katika tukio hilo, hali
inayoashiria kwamba hapakutokea vurugu zozote.
Kafulia livuliwa
wadhifa wa ukatibu mwenezi wa NCCR Mageuzi, tukio lililofuatiwa na
kuvuliwa uanachama katika kikao cha Halmashauri Kuu ya chama hicho
kilichofanyika Desemba 17, mwaka jana.
Mbunge huyo alikuwa
akituhumiwa kuratibu mpango wa mapinduzi dhidi ya mwenyekiti James
Mbatia, pia kukiuka taratibu na katiba ya chama kwa kuzungumza baadhi ya
mambo nje ya vikao vya chama.
Uamuzi huo ulikuwa unampotezea
ubunge wake lakini, alikimbilia mahakamani kufungua kesi ya msingi
kupinga uamuzi huo huku pia akiomba pingamizi la mahakama dhidi ya
uongozi wa NCCR-Mageuzi, kuuzuia usitekeleze kitu chochote hadi kesi
hiyo ya msingi itakapomaliza.
No comments:
Post a Comment