UTANGULIZI
1.0 Wakati
PSRC ilipokuwa chini ya Wizara ya Mipango na Ubinafsishaji, mwaka 2002
iliuza kiwanja Na. 192 kwa Mohamed Enterprise (T) Limited (METL) na
mwaka 2003 ikauza kiwanja Na. 191 kwa Dar es Salaam RTC.
Viwanja hivyo viliuzwa kabla ya PSRC kuvunjwa tarehe 31 Desemba, 2007
na shughuli zake kukabidhiwa CHC tarehe 1 Januari, 2008, ambapo ndiyo
shughuli za CHC zilihamishiwa Wizara ya Fedha.
Kiwanja Na. 192 (au Na. 11 kwa sasa),
cha GAPEX (iliyovunjwa na baadhi ya mali zake kukabidhiwa PSRC) na
kiwanja Na. 191 cha Dar es Salaam RTC, vilikuwa katika eneo moja
vikitumia barabara moja kuingia kwa kupitia ndani ya kiwanja Na. 191
kutokea barabara ya Nyerere (Pugu Road). Hata hivyo, PSRC waliuza
viwanja hivyo bila kwanza kutoa njia (access road) kuingia kiwanja Na.
192.
2.0 Dar
es salaam RTC walianza kupatiwa hati ya kiwanja Na. 191, hivyo kukawa
na mgogoro wa muda mrefu kwa sababu METL hakuweza kupatiwa hati na
Manispaa ya Temeke bila ya kuwa na njia. Vile vile Dar es Salaam RTC
kutokana na kero ya magari makubwa ya METL, walikataa yasiendelee kupita
katika kiwanja chao bila malipo. Malipo ya madai ya Sh. 2.34bn ya
barabara yanayodaiwa na Dar es Salaam RTC hayakuwahi kulipwa na Serikali
hadi sasa.
3.0 Kwa misingi hiyo PSRC ilitakiwa kutoa access road kwa
METL. Kamati ya Serikali chini ya CHC ilitafakari suala hilo nakuona
kwamba, kiwanja Na. 10 ambacho kiliwekwa chini ya PSRC kupitia mali za
TANGOLD iliyokuwa kampuni tanzu ya NMC, kingeweza kutumiwa kutatua
tatizo hilo. Kiwanja Na. 10 kilikuwa kimepangishwa kwa M/s Noble Azania
Investment Ltd (NAIL) na aliweka pingamizi asinyang’anywe na PSRC.
METL alikubali kwamba endapo atapewa kiwanja hicho ili apate barabara
atachukua na kesi na madai ya NAIL.
4.0 Katika
Mkutano wake wa Saba wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
masuala kadhaa yalijitokeza na kujadiliwa. Aidha, katika majadiliano
hayo baadhi ya waheshimiwa wabunge walichangia hoja za POAC na PAC kwa
kumshutumu Mhe Waziri wa Fedha. Baadhi ya Waheshimiwa Wabunge
wakichangia hoja walisema kuwa, baadhi ya Mawaziri ni wezi na kuwa
wanatafuna fedha za Watanzania bila ya woga, na kuwa Mhe. Waziri wa
Fedha ameuza viwanja vya CHC. Aidha, walidai kuwa, alihusika katika
uuzaji wa mali ya Serikali katika kiwanja Na. 10 barabara ya Nyerere na
kwamba ameingilia utendaji wa Mashirika ya Serikali ikiwamo CHC.
5.0 Tungependa
kutoa ufafanuzi kuhusu hoja hizo kama ifuatavyo:- Kiwanja
Na. 10 barabara ya Nyerere hakikuuzwa na Wizara ya Fedha, wala na
Waziri wa Fedha. Kiwanja hicho kiliuzwa na aliyekuwa Mwenyekiti na Kaimu
Mkurugenzi wa CHC kinyume na maelekezo ya Wizara ya Fedha na Kamati ya
Wataalam (DTT), kwamba kiwanja hicho kiuzwe kwa bei ya soko kwa
kuzingatia Sheria na Taratibu.
6.0 Ukweli
upo kwamba, baada ya maelekezo ya Wizara ya Fedha kwamba bei ya soko na
taratibu na sheria zitumike, Kamati ya Wataalamu wa Serikali, ilikaa na
kushauri kwamba taratibu na sheria ni kutangaza ili kupata bei ya soko.
7.0 Bodi
ya CHC ilikaa na kujadili maelekezo ya Wizara ya Fedha na ushauri wa
Kamati ya Wataalam. Baadhi ya Wajumbe wa Bodi walishindwa kuelewa maana
ya taratibu na sheria na bei ya soko, hivyo Bodi iliagiza Waziri wa
Fedha aombwe ufafanuzi. Mwenyekiti na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa CHC
walitumwa na Bodi wamwone Waziri wa Fedha ili warudishe majibu kwenye
Bodi. Waziri wa Fedha alitoa maelezo kwao kwamba, tayari alishatoa
maelekezo kwa maandishi hivyo waendelee kwa kuzingatia maelekezo
yaliyotolewa.
8.0 Aliyekuwa
Mwenyekiti wa Bodi na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa CHC hawakurudi kwenye
Bodi baada ya kupata ufafanuzi kutoka kwa Waziri wa Fedha, bali waliamua
kuuza kiwanja hicho kwa bei ya Mtathmini, badala ya kutangaza na kupata
bei ya soko kama walivyoelekezwa na Wizara ya Fedha na Kamati ya
Wataalam. Aidha, hawakurudi kwa Wizara ya Fedha kutoa taarifa ya
utekelezaji wa maelekezo ya Wizara.
9.0 Aidha
ni vyema ijulikane kwamba, ukaguzi maalumu uliofanywa huko CHC na
Mkaguzi wa Nje, wakati wote wa ukaguzi Wizara ya Fedha haikuhusishwa
kutoa ufafanuzi au taarifa yoyote.
10.0 Tuhuma
kuhusu kwamba, Wizara ya Fedha ilihusika katika uuzwaji wa kiwanja
hicho kwa kutoa maagizo kwa uongozi wa Shirika kuuza kiwanja Na. 10
barabara ya Nyerere bila kuishirikisha Bodi ya Wakurugenzi, hazina
ukweli.
11.0 Hakuna
maagizo yoyote ya Wizara ya Fedha yanayosema kuwa, kiwanja Na. 10
barabara ya Nyerere kiuzwe kwa kampuni ya METL kwa kiasi cha shilingi
bilioni 2.46 bila kuzingatia sheria ya Manunuzi ya mwaka 2004 na kanuni
zake za mwaka 2006.
12.0 Kwa
kuzingatia maelekezo ya Waziri wa Fedha ni dhahiri kuwa, Mhe. Waziri wa
Fedha, hakuhusika na uuzaji wa kiwanja Na. 10 barabara ya Nyerere na
wala hakuingilia utendaji wa CHC. Maelekezo aliyotoa yaliitaka CHC
ifanye maamuzi kwa kufuata sheria, taratibu na kanuni.
Badala yake, aliyekuwa Mwenyekiti wa
Bodi pamoja na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa CHC waliamua kuuza kiwanja hicho
bila kuzingatia ushauri wa Kamati ya Wataalam (DTT) na maelekezo ya
Wizara ya Fedha.
13.0 Kwa misingi hiyo, tuhuma kwamba, Mhe. Waziri wa Fedha alihusika na uuzaji wa kiwanja Na. 10 barabara ya Nyerere sio za ukweli.
KATIBU MKUU
WIZARA YA FEDHA
APRILI, 2012
No comments:
Post a Comment