Baadhi ya majengo ya Kituo cha Afya kilichopo Kata ya Songwa, Wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga kama linavyoonekana pichani
Ofisa Tabibu wa Kituo cha Afya Songwa, Bundala Nandule
KITUO
cha Afya kilichopo Kata ya Songwa, Wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga
kimekatiwa umeme kwa takribani miezi saba sasa kikidaiwa bili ya umeme
na TANESCO ya jumla ya sh. 38,000 hali inayowabebesha mzigo wa gharama
wananchi wanaofika kupata huduma kituoni hapo.
Wagonjwa
wanautibiwa usiku katika kituo hicho hasa wanawake wajawazito
wanalazimika kugharamia mafuta ya taa kwenye chemli za kituo au
kuchangia sh. 1200 kabla ya huduma yoyoto ili kupatikana mwanga
unaowawezesha wahudumu kufanya kazi zao usiku.
Akizungumza
na Thehabari.com juzi kijijini Songwa, Jamila Nyalulu mkazi wa eneo
hilo alisema wananchi wasio na uwezo wa kuchangia mafuta ya taa hasa kwa
huduma za uzazi wamekuwa wakipata tabu, jambo ambalo limekuwa
likihatarisha maisha yao kiafya.
Ofisa
Tabibu wa Kituo hicho, Bundala Nandule amekiri hali hiyo inakwamisha
ufanisi wa utoaji huduma za afya hasa kwa wagonjwa wa usiku au
wanaopumzishwa na kuongeza kuwa tarari wameripoti suala hilo katika
uongozi wa Halmashauri ya Kishapu lakini bado linafanyiwa kazi.
“Tatizo
la umeme linatusumbua kwa kweli hasa mgonjwa anapokuja kupata huduma
usiku. Wagonjwa wa kawaida hulazimika kuja na tochi, lakini kwa
wajawazito wanatakiwa kuja na fanta moja (chupa ya soda) ya mafuta ya
taa au aje na sh. 1200 kwa ajili ya ununuzi wa mafuta hayo kabla ya
huduma,” alisema Nandule.
Hata
hivyo akizungumzia tatizo hilo, Kaimu Mkurugenzi wa Wilaya ya Kishapu,
Lucas Said alisema wanamshangaa Mkuu wa Kituo hicho cha afya kushindwa
kufuatilia malipo ya bili katika ofisi za halmashauri kwani cheki ya
malipo ya bili hiyo iliandikwa tangu mwaka jana (2011).
“Kituo
hicho kilikuwa kinadaiwa sh. 38,000 na cheki iliandikwa tangu mwaka
jana lakini wahusika hawajatokea ili wakabidhiwe cheki hiyo…huu ni
uzembe,” alisema kiongozi huyo wa Halmashauri ya Kishapu.
Kituo
cha afya cha Songwa kinatoa huduma kwa zaidi ya vijiji vitatu vya
Wilaya ya Kishapu, ambavyo ni pamoja na Kijiji cha Songwa, Bushola,
Seseko na baadhi ya zahanati zilizopo jirani na kituo hicho.
*Habari hii imeandaliwa na Mtandao wa Thehabari.com (www.thehabari.com) kwa kushirikiana na Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP).
No comments:
Post a Comment