MADAKTARI
146 wamefukuzwa katika hospitali mbalimbali nchini kutokana na
kushiriki mgomo unaoendelea nchi nzima kwa lengo la kuishinikiza
Serikali kutekeleza madai yao.
Uchunguzi
wa Mwananchi umebaini kuwa, madaktari hao walitimuliwa katika
Hospitali za Bugando na Sekou Toure mkoani Mwanza na Hospitali ya Rufaa
ya Mkoa wa Mbeya na ile ya Rufaa Dodoma.
Wakati
Serikali ikichukua hatua hiyo, mgomo huo jana uliendelea katika
Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Ocean Road, Taasisi ya Mifupa
Muhimbili (MOI) za jijini Dar es Salaam, Hospitali ya Mkoa wa Dodoma na
Hospitali ya Rufaa ya KCMC mkoani Kilimanjaro.
Katika
kile kinachoonekana kuwaunga mkono wenzao, madaktari bingwa wa MOI,
MNH na Ocean Road jijini Dar es Salaam, jana walitangaza rasmi kuingia
kwenye mgomo huo hadi madai hayo yatekelezwe.
Madai
ya madaktari ni hali bora ya mazingira ya utoaji huduma nchini,
ongezeko la mishahara, posho za kufanya kazi katika mazingira magumu,
posho za kufanya kazi katika mazingira hatarishi na posho za kuitwa
kazini.
Tamko
la madaktari hao bingwa, lilitolewa jana na msemaji wao, Dk Catherine
Mng'ong'o muda mfupi baada ya kumalizika kwa kikao chao kilichofanyika
jijini Dar es Salaam.
Tamko
hilo limekuja siku moja baada ya baadhi yao kuanza kushiriki mgomo huo
juzi, kushinikiza pamoja na mambo mengine, Serikali itoe tamko juu ya
tukio la kutekwa na kujeruhiwa kwa Dk Ulimboka.
Hata
hivyo, wakati madaktari hao wakitoa tamko hilo, uongozi wa Moi jana
ulitoa tangazo kuwataka madaktari wote walioshiriki mgomo huo kurejea
kazini ifikapo Julai 2, mwaka huu, vinginevyo watafukuzwa kazi.
Jana
jengo la MOI lilikuwa limefungwa kwa makufuli, huku wagonjwa
wakielezwa kuwa huduma zote hazitolewi zikiwamo za dharura ambazo awali
ziliendelea kutolewa.
Mmoja wa walinzi aliwambia waandishi wa habari kuwa, amefunga mageti kutokana na amri ya mkuu wake wa kazi.
“Mimi
ninatekeleza amri ya bosi wangu, amenitaka kufunga geti na hakuna mtu
kuingia, awe mgonjwa au ninyi waandishi wa habari kwa kuwa hakuna
huduma zinazotolewa humu,” alisema.
Mkoani Mwanza
Madaktari
63 walio katika mafunzo ya vitendo kazini wa Hospitali ya Rufaa ya
Bugando, Hospitali ya Mkoa Sekou Toure wametimuliwa na kurejeshwa
wizarani kutokana na mgomo huo.
Mkurugenzi
wa Hospitali ya Rufaa ya Bugando, Dk Charles Majinge alisema kuwa,
juzi aliwataka madaktari waliokuwa katika mgomo kurejea kazini, lakini
hawakufanya hivyo na jana akaamua kuwarejesha 47 wizarani.
Katika
Hospitali hiyo ya Mkoa wa Mwanza Sekou Toure, Mganga Mkuu wa Mkoa, Dk
Valentino Bangi alisema, madaktari 16 wamesimamishwa kufanya kazi
kutokana na agizo la wizara.
Chanzo: Vijimambo Blog
No comments:
Post a Comment