Social Icons

IMETOSHA

IMETOSHA

Saturday, June 23, 2012

MRISHO NGASSA ATUA JANGWANI




Mrisho Ngassa.
KIUNGO wa Azam FC, Mrisho Ngassa, jana Alhamisi alitua makao makuu ya klabu ya Yanga yaliyopo Jangwani jijini Dar es Salaam na kupokewa kwa shangwe kubwa.
Ngassa ana uwezekano mkubwa wa kuwemo kwenye kikosi cha Yanga kitakachoshiriki michuano ya Kombe la Kagame inayotarajiwa kuanza Julai 14, mwaka huu.
Ngassa aliwasili Jangwani saa 5:07 asubuhi akiwa ndani ya gari lake aina ya Toyota Corona lenye namba za usajili T 508 AUB, ikiwa ni muda mfupi baada ya mazoezi ya timu hiyo kumalizika kwenye Uwanja wa Kaunda, kisha kwenda kuegesha gari lake sehemu maalum inayotumiwa na viongozi na wachezaji wa Yanga pindi wanapowasili klabuni hapo.
Wakati umati wa mashabiki uliokuwa ukishuhudia mazoezi ukijiandaa kuondoka, ghafla ulimuona Ngassa na ndipo ukalizunguka gari lake na kuanza kumshangilia. Kuona hivyo Ngassa alisita kwa muda kutoka kisha kufungua mlango wa gari na kutoka.
Mashabiki hao walimvamia na kumbeba juujuu kwa furaha huku wakiimba kwa kulitaja jina lake ‘Ngassa! Ngassa! Ngassa! Ngassa!’ Lakini baadaye aliwataka wamshushe, mashabiki hao walitii amri hiyo.
Baada ya hapo, alianza kuelekea ndani ya jengo huku akisalimiana na wachezaji wa Yanga waliokuwepo eneo hilo, muda mfupi baadaye Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Yanga, Seif Ahmeid ‘Seif Magari’ alitokea ndani ya jengo hilo na kuingia naye kwenye chumba namba saba.
Baadaye, Ngassa alipandisha ghorofani na kuingia kwenye chumba namba saba ambapo alikuwemo mshambuliaji wa timu hiyo, Jerry Tegete. Mpaka gazeti hili lilipoondoka klabuni hapo 5:45 asubuhi, Ngassa alikuwa hajatoka chumbani humo.
Alipoulizwa kuhusiana na ujio wake Jangwani, Ngassa alisema: “Nimekuja kuonana na Jerry, tulipanga tukutane hapa kwa ajili ya kufanya mazungumzo yetu binafsi, siyo ya mpira.”
Aidha, habari za ndani kutoka kwa mmoja wa viongozi wa klabu hiyo, zimethibitisha kuwa kweli Jangwani wamefanya mazungumzo na Azam, kilichobakia ni makubaliano ya mwisho kabla ya kumtambulisha rasmi Ngassa kuwa mchezaji wa Yanga.
Mpigapicha wa gazeti hili, Richard Bukos, alimpiga picha mchezaji huyo wakati akiwasili klabuni hapo lakini Ngassa na baadhi ya mashabiki walimuomba kufuta picha hizo sababu mambo hayajakamilika na kudai zinaweza kumsababishia matatizo ya uhamisho wake.

No comments:

Post a Comment