Social Icons

IMETOSHA

IMETOSHA

Thursday, July 26, 2012

CHADEMA wahoji ununuzi wa mitambo ya kijasusi


KAMBI Rasmi ya Upinzani Bungeni imeitaka serikali kutoa ufafanuzi kama kuna mtambo ulionunuliwa kutoka nchini Israel kwenye Kampuni ya NICE maarufu kama Gi2, ambao ni maalumu kwa ajili ya kufanya “sms spoofing”.
Taarifa hizo zinadai kuwa mtambo huo uliuzwa kwa Jeshi la Polisi nchini Aprili mwaka huu.
Kauli hiyo ilitolewa jana na Naibu Msemaji wa kambi hiyo, Wizara ya Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, Joshua Nassari, wakati akisoma hotuba yao.
Nassari alisema wataalamu waliowasiliana nao na mitandao mbalimbali kama vile www.textfromwho.com walionesha teknolojia hii ya “sms spoofing” yenye uwezo wa kutuma ujumbe wa simu ya mkononi kwa kutumia simu ya mtu mwingine kana kwamba ni mwenye namba ya simu aliyetuma ujumbe huo.
“Mheshimiwa Spika chuo kimojawapo kilichopo India cha “The Asian Schools of Cyber Laws” (Pune) walifanya utafiti juu ya jambo hili na majibu ya utafiti huo ni kuwa waliweza kutuma ujumbe mfupi wa simu kwa kutumia njia hii na waliweza kutumia simu za watu waliokuwa mtandao wa “GSM” kwenye mabara ya Afrika na Asia.
“Utafiti ulionesha kufanikiwa kutumia namba za simu za watu wengine na kutuma ujumbe mfupi wa simu,” alisema na kuongeza kwamba vyanzo mbalimbali vya taarifa ni kuwa mtambo kama huo unatumika kwenye nchi za Israel na Ujerumani ila kwa nchi nyingine kama Australia kufanya tendo hilo ni kosa kisheria kwani wao wamepiga marufuku matumizi ya mfumo huo.
Nassari aliongeza kuwa mwaka 2008 nchini Uingereza, kampuni ya udhibiti wa mawasiliano wa viwango vya juu inayojulikana kama “phone pay plus” ambayo kabla ilijulikana kama ICSTIS walianzisha kanuni kwa ajili ya wateja kuweza kutoa malalamiko kama simu zao zimefanyiwa uharamia huo.
“Kambi ya Upinzani tunataka kupata majibu juu ya mambo yafuatayo; Je, taarifa za mtambo huo wa Gi2 kununuliwa na kuletwa nchini na kutumiwa na Jeshi la Polisi mwaka huu ni za kweli?” alihoji.
Msemaji huyo alibainisha kwamba wanataka kujua mtambo huo umeletwa kwa madhumuni gani hasa na utakuwa unatumika kwenye masuala gani.
“Mtambo utakaonunuliwa na TCRA ni wa aina gani na utakuwa na uwezo wa kufanya sms spoofing, na kwamba kama jibu ni ndio, zitatumika kufanyia shughuli gani hasa,” alisema.
Kauli ya CHADEMA inakuja siku chahe tangu, mjumbe wa Kamati Kuu na mshauri wa chama hicho, Mabere Marando, kudai kuwa wamenasa mbinu za uwepo wa mtambo huo na kuwa ndio ulitumika kumtumia sms za vitisho Mbunge wa Iramba Magharibi (CCM), zikionesha kuwa zimetoka kwa wabunge wa CHADEMA.
Bil 1.3/- zaibiwa mtandaoni
Katika hatua nyingine, kambi ya upinzani bungeni ilitaka kujua serikali imejiandaaje ili kudhibiti uhalifu wa kimtandao unaoshika kasi.
Nassari alisema kwa sasa kiasi kilichoripotiwa Polisi kuhusiana na wizi kwa njia ya mtandao hapa nchini ni sh bilioni 1.3, Euro 8,897 na dola za kimarekani 551,777.
“Uhalifu huu wa kimtandao unaongezeka kwa kasi kubwa sana hapa nchini mwetu na unatishia uhai wa uchumi wetu kama taifa kama hatua hazitachukuliwa mara moja,” alisema.
Kuhusu kubadili mfumo wa utangazaji kutoka analojia kwenda digitali, kambi ya upinzani na Kamati ya Bunge ya Miundombinu waliitaka serikali kuhakikisha ving’amuzi vinauzwa kwa bei ambayo Watanzania wa kawaida wataweza kuimudu, vile vile ihakikishe king’amuzi kinakuwa kimoja chenye kubeba vituo vyote.
Msemaji wa kamati hiyo, Profesa Juma Kapuya alisema wanaitaka serikali kuweka umakini katika uchimbaji wa madini ya urani utakaoanza hivi karibuni huko Namtumbo, Bahi na Manyoni.

Tanzani Daima

No comments:

Post a Comment