Social Icons

IMETOSHA

IMETOSHA

Friday, July 13, 2012

EXCLUSIVE:HII NDIO HOTUBA KALI NA MAKINI ILIYOTOLEWA NA KAMBI YA UPINZANI BUNGENI ISOME HAPA!!!!!!!!

MAONI YA MSEMAJI MKUU WA KAMBI RASMI YA UPINZANI BUNGENI, WIZARA YA KATIBA NA SHERIA,
MHESHIMIWA TUNDU A.M. LISSU (MB.)
KUHUSU
MPANGO NA MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI YA FEDHA YA WIZARA YA KATIBA NA SHERIA KWA MWAKA 2012/2013
(Kanuni ya 99(7) ya Kanuni za Kudumu za Bunge, 2007)
UTANGULIZI
Mheshimiwa Spika,

Ofisi ya Waziri wa Katiba na Sheria imeanzishwa kwa mujibu wa kipengele cha 12 cha Nyongeza ya Waraka wa Rais uliochapishwa kama Tangazo la Serikali Na. 494 la tarehe 17 Desemba 2010. Majukumu ya Ofisi hii yameainishwa katika Tangazo la Ukasimishaji wa Majukumu ya Kiuwaziri la mwaka 2010 (The Ministers [Assignment of Ministerial Functions] Notice, 2010) lililochapishwa katika Gazeti la Serikali kama Tangazo la Serikali Na. 494A la tarehe 17 Desemba 2010. Kwa mujibu wa Nyongeza ya Pili ya Tangazo hilo, pamoja na mengine, Ofisi ya Waziri wa Katiba na Sheria imekasimiwa majukumu ya masuala ya kikatiba, uendeshaji na utoaji wa haki, uendeshaji mashtaka na haki za binadamu.

FEDHA ZA MAHAKAMA NA AHADI HEWA
Mheshimiwa Spika,

Mwaka jana wakati nawasilisha Maoni ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kuhusu Muswada wa Sheria ya Uendeshaji wa Mahakama, 2011 nililiambia Bunge lako tukufu kwamba “... tatizo kubwa linalozikabili mahakama zetu sio uhaba wa uwezo wa kusimamia fedha zinazotolewa kwa ajili yao, bali ni uhaba wa fedha zenyewe! Pili, tatizo la uhaba wa fedha ... linasababishwa ... na ukosefu wa uelewa wa mahitaji halisi ya Mahakama. Tatu, tatizo la ukosefu wa uelewa wa mahitaji halisi ya Mahakama ... linasababishwa na ukosefu wa watu wanaoelewa mahitaji hayo serikalini au ukosefu wa wafanya maamuzi ya migawanyo ya fedha wanaofahamu mahitaji halisi ya Mahakama.” Tatizo la vipaumbele vya Mahakama kutozingatiwa katika migawanyo ya bajeti za Serikali za kila mwaka limeendelea katika mwaka huu wa fedha.

Mheshimiwa Spika,

Kwa mujibu wa Maelezo ya Makadirio ya Mapato, Matumizi ya Kawaida na Mpango wa Maendeleo kwa Mwaka 2012/2013 kwa Fungu la 40 i.e. Mahakama, katika mwaka wa fedha 2011/2012, Mahakama ya Rufani iliidhinishiwa shilingi bilioni 33.201. Kwa mujibu ya Maelezo hayo, hadi mwezi Mei 2012 Mahakama ya Rufani ilikuwa imepokea shilingi bilioni 26.251 au asilimia 79 tu ya fedha zilizoidhinishwa na Bunge. Matokeo ya kuipatia Mahakama ya Rufani fedha pungufu ya bajeti iliyoidhinishwa, Maelezo ya Wizara yanasema, ni kwamba Mahakama ya Rufani iliweza kufanya vikao 26 kati ya 30 vilivyokuwa vimetarajiwa kufanyika katika kipindi hicho.

Kwa upande wa Mahakama Kuu, Maelezo ya Wizara yanasema kwamba katika mwaka wa fedha 2011/2012 Mahakama Kuu iliidhinishiwa shilingi bilioni 19.569[i] Hadi mwezi Mei 2012, Hazina ilikuwa imetoa shilingi bilioni 12.919 zikiwa ni shilingi bilioni 6.159 kwa ajili ya matumizi mengineyo na shilingi bilioni 6.759 kwa ajili ya mishahara. Hii ina maana kwamba Mahakama Kuu ilipatiwa asilimia 66 ya bajeti yake. Mfuko wa Mahakama (Judiciary Fund) – ambao ulipigiwa upatu mkubwa wakati wa mjadala wa Sheria ya Uendeshaji Mahakama kwamba ndio mwarobaini wa matatizo ya fedha za Mahakama – uliidhinishiwa shilingi bilioni 20 katika mwaka wa fedha 2011/2012. Hata hivyo, kiasi kilichotolewa ni shilingi bilioni 14.548 au asilimia 72.74 ya fedha iliyoidhinishwa na Bunge hili tukufu. Kwa rekodi hii, ni wazi kwamba hata kiasi cha shilingi bilioni 28.38[ii] ambazo – kwa mujibu wa randama ya Fungu 40 - zimetengwa kwa Mfuko wa Mahakama kwa mwaka wa fedha 2012/2013 zitatolewa chini ya nusu ya makadirio.
Mheshimiwa Spika, Maelezo ya Wizara yametoa takwimu zinazoonyesha mafanikio makubwa katika kusikiliza na kutoa maamuzi ya mashauri katika mahakama zetu za ngazi zote. Hivyo, kwa mfano, tunaambiwa kwamba katika vikao 26 kati ya 30 vya Mahakama ya Rufani, asilimia 143 ya mashauri yaliyofunguliwa yalisikilizwa na kutolewa maamuzi! Aidha, tunaambiwa na Wizara, “Mahakama Kuu imefanikiwa kusikiliza na kuyatolea maamuzi ... asilimia 123 ya mashauri yaliyofunguliwa. Kwa upande wao, Mahakama za Hakimu Mkazi na za Wilaya ‘zilifanikiwa’ kusikiliza na kuyatolea maamuzi asilimia 125 na 109 za mashauri yaliyofunguliwa; wakati ambapo Mahakama za Mwanzo zimefanikiwa kwa asilimia 99.7 katika kusikiliza na kutoa maamuzi ya mashauri yaliyofunguliwa katika Mahakama hizo. Mheshimiwa Spika, Kama hali halisi ingekuwa ndio hii inayoelezewa na Wizara basi ni wazi kwamba nchi yetu ya Tanzania isingekuwa na tatizo la mlundikano wa kesi katika Mahakama zetu zote. Na, kwa hiyo, Wizara isingetaja kama mojawapo ya changamoto za Mahakama ya Tanzania “ongezeko la mashauri ... hivyo kusababisha mlundikano wa mashauri mahakamani.” Na wala Wizara isingekuwa na changamoto za ‘bajeti finyu isiyokidhi majukumu ya Mahakama’; au ya “fedha kutokutolewa kadiri ya mpango wa kazi ... wa mwaka na kwa wakati” kama inavyodaiwa katika Maelezo ya Wizara hayo hayo yanayotangaza mafanikio makubwa katika usikilizaji wa mashauri na utoaji wa maamuzi ya mashauri hayo. Mheshimiwa Spika, Ukweli ni kwamba, kwa jinsi zilivyowasilishwa katika Maelezo ya Wizara, takwimu za mafanikio ya Mahakama ya Tanzania katika kusikiliza na kutoa maamuzi ya mashauri zinapotosha ukweli ambao upo katika Maelezo hayo hayo. Hivyo, kwa mfano, licha ya Maelezo ya Wizara kutaja ‘mafanikio mazuri yaliyopatikana’, Maelezo hayo hayo yanaonyesha kwamba, kwa sababu ya ‘bajeti finyu isiyokidhi majukumu ya Mahakama’, Mahakama ya Rufani ilifanikiwa “... kupunguza mlundikano wa mashauri kwa asilimia 10.7 (tu).” Aidha, kwa sababu hiyo hiyo ya ‘bajeti finyu’, Mahakama Kuu ilifanikiwa “... kupunguza mlundikano wa mashauri kwa asilimia 6”; wakati Mahakama za Hakimu Mkazi na za Wilaya ‘zilifanikiwa’ – kwa mlolongo huo huo - kupunguza mlundikano wa mashauri kwa asilimia 9.4 na asilimia 11.5. Hii ndio kusema kwamba wastani wa ‘mafanikio’ ya kupunguza mlundikano wa mashauri katika mahakama zetu ni asilimia 9.4 tu! Kwa ushahidi huu wa Serikali yenyewe, kwa sababu ya kutopatiwa fedha za kukidhi mahitaji halisi ya utoaji wa haki, Mahakama ya Tanzania imeshindwa kabisa kutatua tatizo la mlundikano mkubwa wa kesi katika ngazi zote. Mheshimiwa Spika, Bajeti ya maendeleo ya Mahakama ya Tanzania vile vile imekumbwa na tatizo la mgawanyo mbovu wa fedha. Hili nalo linaelekea kuwa tatizo sugu. Kwa mfano, Maelezo ya Wizara yanasema kwamba katika mwaka wa fedha 2011/2012, Mahakama ya Tanzania ilitengewa shilingi bilioni 13.546 kwa ajili ya miradi ya maendeleo. Hata hivyo, hadi kufikia mwezi Mei 2012 Mahakama ilikuwa imepokea shilingi bilioni 2.285 kutoka Hazina, ikiwa ni asilimia 16.86 ya bajeti iliyoidhinishwa na Bunge. Ijapokuwa Serikali inaita kazi zilizofanyika kwa fedha hizi pungufu kuwa ni ‘mafanikio mazuri’, ni vigumu kukubaliana na tathmini hii. Kwanza, hata kwa mapambo ya lugha ya kirasimu ya aina hii, ni vigumu kuamini kwamba kazi zilizofanywa na asilimia 16.86 ya gharama zilizotarajiwa zinaweza kuleta ‘mafanikio mazuri.’ Vinginevyo Serikali iwaeleze Watanzania kwa nini ililiomba Bunge hili tukufu liidhinishe shilingi bilioni 13.546 kama ilikuwa inajua kwamba mgawo wa shilingi bilioni 2.285 utaleta ‘mafanikio mazuri.’ Pili, Serikali yenyewe imekiri kwamba Mahakama ya Tanzania ilikumbana na ‘changamoto’ ya ‘bajeti finyu isiyokidhi majukumu ya Mahakama.’ Aidha, Serikali inakiri kwamba kuna matatizo ya “upungufu wa vitendea kazi kama vile magari, kompyuta, uduni wa mazingira ya kazi na nyumba za kuishi watumishi hususani majaji, mahakimu na watumishi wengine wa umma.” Vile vile, “hali ya majengo ya Mahakama haijaridhisha kiasi cha kutosheleza mahitaji (kwani) kiasi cha fedha za maendeleo kinachotolewa na Serikali ni kidogo sana ukilinganisha na idadi na hali halisi ya majengo ya Mahakama hapa nchini.” Tatu, kama ni kweli – kama inavyodaiwa kwenye Maelezo ya Wizara – kwamba “suala la usafiri kwa ajili ya shughuli za Mahakama limepewa uzito unaostahili kwa Serikali kununua magari manne kwa ajili ya Waheshimiwa Majaji”, inakuwaje basi kwamba katika Maelezo hayo hayo Serikali inakiri kwamba ‘upungufu wa vitendea kazi kama vile magari’, n.k. bado ni changamoto kubwa? Ukweli ni kwamba kauli za aina hii zinalenga kuficha ukweli wa hali halisi ambayo ni mbaya sana. Kwa mfano, Mahakama ya Hakimu Mkazi wa Singida inayohudumia Mkoa Mzima wa Singida wenye Mahakama tatu za Wilaya na Mahakama zaidi ya arobaini za Mwanzo haina gari hata moja na inategemea gari moja la Mahakama ya Wilaya ambalo nalo halifanyi kazi kwa sababu ya ukosefu wa spea! Na kwa hali ilivyo, Mahakama ya Hakimu Mkazi Singida haiwezi kuwa ni mfano wa kipekee wa mapungufu haya kwani Mahakama nyingine nyingi za Hakimu Mkazi na za Wilaya zinakabiliwa na matatizo ya aina hiyo hiyo. Katika hotuba yake ya mwaka jana, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni ilielezea upungufu mkubwa wa watumishi wa ngazi mbali mbali wa Mahakama ya Tanzania ambao ni matokeo ya moja kwa moja ya kunyimwa fedha na Serikali. Tatizo hili halijapatiwa ufumbuzi wowote na kuna uwezekano kwamba linazidi kuwa kubwa zaidi. Kwa mujibu wa Maelezo ya Wizara, “uhaba wa watumishi wenye sifa zinazotakiwa bado unaendelea kuwa tatizo. Maslahi yasiyokidhi hali ya utendaji katika Mahakama inapelekea baadhi ya watumishi kuacha kazi.” Aidha, Mheshimiwa Spika, Mahakama ya Tanzania imeendelea kufedheheka kwa kuwa mdeni mkubwa na sugu. Hadi wakati tunaandika Maoni haya, Mahakama ya Tanzania inadaiwa na majaji na watumishi wengine wa Mahakama, watoa huduma, wenye nyumba za kupangisha majaji, wajenzi na wazabuni mbali mbali jumla ya shilingi bilioni 5.2. Yote haya ni madeni ya miaka ya nyuma hadi kufikia mwaka wa fedha 2010/2011! Mheshimiwa Spika, Kwa mujibu wa Sheria ya Malipo na Mafao ya Majaji (Judges (Remuneration and Terminal Benefits) Act) ya mwaka 2007, majaji wanastahili kulipiwa – nje ya malipo ya mshahara – nyumba yenye samani ya Daraja A; gharama za matibabu kwa ajili yao wenyewe na familia zao; gari ya Serikali pamoja na dereva. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inafahamu kuwa kila Jaji mteule huandikiwa barua ya ajira kutoka Ofisi ya Rais inayofafanua stahili hizi. Hata hivyo, kwa sababu ya kutokupatiwa ‘fedha zinazokidhi mahitaji ya Mahakama’, sasa majaji wetu wanaishi katika nyumba za kupanga ambazo zinadaiwa kodi na wenye nyumba; wanalazimika kujilipia gharama za matibabu yao na ya familia zao, na baadhi wanatembelea mikweche ya magari. Fedheha hizi kwa majaji wetu na watumishi wengine wa Mahakama ya Tanzania zinaonyesha sio tu ukiukwaji makusudi wa sheria tajwa bali zinathibitisha jinsi gani ambavyo mfumo wa utoaji haki na uhuru wa Mahakama haujawa kipaumbele cha Serikali hii ya CCM. Mheshimiwa Spika, Nilipendekeza, wakati wa mjadala wa Sheria ya Uendeshaji Mahakama, kwamba badala ya Mahakama kutegemea ukomo wa bajeti unaowekwa na Hazina, sheria ielekeze – kama ilivyo kwa Bunge na vyama vya siasa vyenye uwakilishi Bungeni na nchi jirani ya Kenya - kwamba bajeti ya Mahakama ya kila mwaka isiwe pungufu ya asilimia 3 ya bajeti ya kila mwaka ya Serikali ili kuiwezesha Mahakama kuwa na uhakika wa fedha zake na kuiwezesha kupanga mipango yake kwa uhakika zaidi. Pendekezo langu lilikataliwa. Matatizo ya bajeti ya Mahakama ambayo tumeyaeleza hapa yanathibitisha wazi kwamba utaratibu wa sasa wa kutegemea mgawo wa Hazina hauwezi kutatua matatizo ya fedha ya Mahakama ya Tanzania. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali itoe kauli Bungeni ni kwa nini inakataa kuihakikishia Mahakama fedha zake kwa kurekebisha Sheria ya Uendeshaji Mahakama ili kuweka a minimum percentage ya bajeti ya Serikali kwa ajili ya Mahakama - kama ilivyofanya kwa Bunge na kwa vyama vya siasa. Mheshimiwa Spika, Haki iliyocheleweshwa ni haki iliyonyimwa. Ndio maana ibara ya 107A(2)(b) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, 1977 inatamka kwamba “katika kutoa uamuzi wa mashauri ya madai na jinai kwa kuzingatia sheria, Mahakama zitafuata kanuni zifuatazo, yaani ... kutochelewesha haki bila sababu ya msingi.” Takwimu za Mahakama ya Tanzania juu ya mlundikano wa kesi katika ngazi mbali mbali za Mahakama zinaonyesha jinsi hali ilivyo mbaya. Kwa mfano, hadi tunaandika Maoni haya Mahakama ya Rufani ina mlundikano wa kesi 1,743; Mahakama Kuu kesi 8,911; Mahakama Kuu Divisheni ya Biashara kesi 285; Mahakama Kuu Divisheni ya Kazi kesi 1,238; na Mahakama Kuu Divisheni ya Ardhi kesi 5,543. Hali ya mlundikano wa kesi katika ngazi za chini katika Mahakama ya Tanzania ni mbaya zaidi. Kwa mfano, Mahakama za Hakimu Mkazi zina backlog ya kesi 25,002; Mahakama za Wilaya kesi 31,025 na Mahakama za Mwanzo kesi 124,959. Kwa ushahidi huu, Mheshimiwa Spika, ni wazi kwamba Mahakama ya Tanzania imeshindwa kutekeleza wajibu wake huu wa kikatiba kwa sababu ya kunyimwa fedha na vitendea kazi vingine na Serikali hii hii inayodai kwamba dira yake ni ‘haki kwa wote na kwa wakati’! Kwa maana nyingine, maelfu ya mahabusu na wafungwa ambao wamejaa katika magereza yetu wakisubiri maamuzi ya kesi zao, na maelfu ya wadaawa ambao kesi zao zimelundikana katika mahakama zetu zote wanateseka kwa sababu sera za utoaji haki za Serikali hii ya CCM hazitekelezeki. Na, Mheshimiwa Spika, dawa ya Serikali na chama ambacho sera zake hazitekelezeki na hivyo kusababisha mateso kwa wananchi ni ile aliyoigusia Baba wa Taifa katika kitabu chake Uongozi Wetu na Hatima ya Tanzania: “Hatulazimiki kuendelea na uongozi mbovu wa Chama na Serikali. Wala tukiendelea na hali hii, bila kubadili uongozi wa Chama na Serikali, sina hakika kama tutafika huko salama. Masuala muhimu ya nchi yetu hayatashughulikiwa.... Na masuala mengine muhimu ... yataachwa yajitatue yenyewe. Nasema katika hali kama hiyo sina hakika kama tutafika salama; na tukifika salama tukiwa na uongozi huu huu wa Chama na Serikali mbele kutakuwa ni giza tupu. Majuto ni mjukuu, huja baadaye.
UTEUZI WA MAJAJI
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inatambua ukweli kwamba Rais Kikwete ameteua Majaji wengi wa Mahakama Kuu ya Jamhuri ya Muungano kuliko Marais wengine wote waliomtangulia kwa ujumla wao. Rekodi hii peke yake inaonyesha kwamba Rais anatambua umuhimu wa Mahakama Kuu kuwa na watendaji wa kutosha wa utoaji haki ili kutekeleza dira ya ‘haki kwa wote na kwa wakati.’ Hata hivyo, Mheshimiwa Spika, kuteua Majaji wengi ni jambo moja. Kuteua Majaji wengi wenye uwezo, ujuzi na wanaofaa kukabidhiwa madaraka ya Jaji wa Mahakama Kuu ni jambo jingine kabisa. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inasikitishwa na dalili zinazoanza kuonekana wazi kwamba baadhi ya Majaji walioteuliwa na Rais hawana uwezo, ujuzi na/au hawakufaa kukabidhiwa madaraka ya Jaji ya Mahakama Kuu. Mheshimiwa Spika, Kwa mujibu wa ibara ya 109(6) ya Katiba, mtu anaweza kuteuliwa Jaji wa Mahakama Kuu ikiwa ana ‘sifa maalum’, na amekuwa na mojawapo ya sifa maalum kwa muda usiopungua miaka kumi. Sifa hizo, kwa mujibu wa ibara ndogo ya (7), maana yake “ni mtu aliye na shahada ya sheria kutoka chuo kikuu kinachotambuliwa na mamlaka ya ithibati Tanzania na amekuwa hakimu; amefanya kazi katika utumishi wa umma akiwa na sifa za kufanya kazi ya uwakili au ni wakili wa kujitegemea; ana sifa ya kusajiliwa wakili, na amekuwa na sifa hizo mfululizo kwa muda usiopungua miaka kumi.” Sharti la kuwa na sifa hizo kwa miaka kumi mfululizo linaweza kutenguliwa endapo Rais – baada ya kushauriana na Tume ya Utumishi wa Mahakama - atatosheka kwamba mhusika ana uwezo, ujuzi na kwa kila hali anafaa kukabidhiwa madaraka ya Jaji wa Mahakama Kuu na kuna sababu za kumfanya mtu huyo astahili kukabidhiwa madaraka hayo. (ibara ya 109(8) Tume ya Utumishi wa Mahakama inaundwa na Jaji Mkuu ambaye ni Mwenyekiti wake, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji mmoja wa Mahakama ya Rufaa atakayeteuliwa na Rais kwa kushauriana na Jaji Mkuu, Jaji Kiongozi na wajumbe wawili watakaoteuliwa na Rais. Jukumu la kwanza la Tume hii, kufuatana na ibara ya 113(1)(a), ni “kumshauri Rais kuhusu uteuzi wa Majaji wa Mahakama Kuu.” Ni wazi kwamba utaratibu huu wa uteuzi wa Majaji wa Mahakama Kuu ulilenga kumwezesha Rais – ambaye sio lazima awe mwanasheria na/au mwenye ufahamu wa masuala ya kisheria – kuteua Majaji baada ya kupata ushauri kutoka kwa viongozi waandamizi wa Mahakama ya Tanzania na pia kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali ambaye anawajibika kikatiba “... kutoa ushauri kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano kuhusu mambo yote ya kisheria....” (ibara ya 59(3) Kwa maoni ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Rais hana mamlaka ya kufanya uteuzi wa Majaji wa Mahakama Kuu nje ya utaratibu huu uliowekwa na Katiba. Hata hivyo, Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni ina taarifa kwamba utaratibu huu wa kuteua Majaji umeachwa kufuatwa. Kwa mujibu wa taarifa tulizo nazo, sasa watu wanateuliwa kuwa Majaji wa Mahakama Kuu ambao hawajawahi kupendekezwa na Tume ya Utumishi wa Mahakama na - kwa sababu hiyo - hawajafanyiwa vetting yoyote na mamlaka hiyo ya kikatiba juu ya uwezo na ujuzi wao na kama ‘wanafaa kwa kila hali kukabidhiwa madaraka ya Jaji wa Mahakama Kuu.’ Inaelekea watu hao – wengi wao wakiwa wamekaribia muda wao wa kustaafu kwingineko katika utumishi wa umma – wanapewa ‘zawadi’ ya ujaji ili kuwawezesha kupata mafao ya Majaji wastaafu ambayo yameboreshwa sana katika miaka ya karibuni. Matokeo yake ni kuwa na majaji ambao wamechoka na hawawezi au hawajui namna ya kufanya kazi ya Jaji wa Mahakama Kuu. Mheshimiwa Spika, Madhara ya kukiuka utaratibu huu wa kikatiba wa uteuzi wa Majaji wa Mahakama Kuu ni makubwa na yameanza kujitokeza wazi. Kwanza, wapo Majaji ambao – kwa sababu ya kutokufanyiwa vetting na Tume ya Utumishi wa Mahakama – hawana uwezo wa kuandika mwenendo wa mashauri na hukumu zinazosomeka kwa sababu ya, ama kutokuwa na uwezo na ujuzi wa sheria, au kutokuwa na weledi wa lugha ya Kiingereza ambayo ndiyo lugha rasmi ya mwenendo wa mashauri na hukumu. Aidha, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inazo taarifa kwamba wapo Majaji ambao – kwa sababu hizo hizo za kutokufanyiwa vetting juu ya uwezo na ujuzi wao na mamlaka husika ya kikatiba – wameshindwa kabisa kuandika hukumu za kesi walizozisikiliza na hivyo kusababisha mlundikano wa kesi mahakamani usiokuwa na sababu yoyote ya msingi. Kazi ya Jaji wa Mahakama Kuu, kama ilivyo kazi ya mawakili na wanasheria kwa ujumla, ni kazi ya kisomi. Ni kazi inayohitaji watu wenye uwezo mkubwa kitaaluma na utafiti, weledi wa uchambuzi (analytical skills) na wa kuandika na kuzungumza kwa lugha ya kimombo fasaha. Watu hawa hawaitwi ‘wanasheria wasomi’ kama mapambo tu. Wanatakiwa kuwa wasomi kweli kweli. Kwa maoni ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, kuwa na Majaji wasiokuwa na sifa hizi sio tu kunafifisha utoaji wa haki kwa wadaawa katika mashauri yaliyoko mahakamani, bali pia kunaifedhehesha taaluma nzima ya sheria, Mahakama ya Tanzania na mamlaka yao ya uteuzi, yaani Rais mwenyewe. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali itoe ufafanuzi juu ya jambo hili na pia itoe kauli mbele ya Bunge hili tukufu kwamba utaratibu wa uteuzi wa Majaji uliowekwa na Katiba utaheshimiwa kwa Rais kuteua Majaji watakaotokana na ushauri wa Tume ya Utumishi wa Mahakama ili kuondokana na aibu na fedheha hii ya kuwa na Majaji wasiojua wanachotakiwa kufanya.
MIKOA NA WILAYA MPYA
Mheshimiwa Spika, Mfumo wetu wa tawala za mikoa na wilaya umefafanuliwa katika ibara 2(2) na 61 za Katiba na katika Sheria ya Tawala za Mikoa, Sura 189 ya Sheria za Tanzania. Mfumo huu ulirithiwa kutoka mfumo wa dola la kikoloni uliokuwa umeangikwa kwenye majimbo na wilaya. Mabadiliko ya mwaka 1962 yaliyofuta majimbo kuanzisha mikoa hayakuwa mabadiliko ya mfumo bali yalikuwa ni kugawa majimbo – yaliyokuwa makubwa kijiografia – kwenda mikoa iliyokuwa midogo kieneo. Mambo mengine yote ya kimfumo, kwa mfano, mamlaka ya kugawa maeneo katika majimbo na wilaya na ya kuteua wakuu wa maeneo hayo hayakubadilishwa kimsingi bali yalihamishwa kutoka kwa gavana wa kikoloni kwenda kwa Rais. Katika mfumo huo wa kikoloni, wananchi hawakushirikishwa kwa namna yoyote katika maamuzi ya kugawa maeneo kuwa majimbo na wilaya. Dola la uhuru halijabadilisha mfumo huo kwa namna yoyote ya maana hata baada ya nusu karne ya uhuru. Kama ilivyokuwa wakati wa ukoloni wananchi, ambao ibara ya 8(1)(a) ya Katiba inadai kwamba ‘ndio msingi wa mamlaka yote’, wameendelea kutegemea karama za watawala za kutengewa mikoa au wilaya mpya. Vile vile, malengo ya kuteua wakuu wa maeneo haya nayo hayajabadilika sana. Wakati ambapo wengi wa Wakuu wa Majimbo na Wilaya wa kikoloni walikuwa maafisa wa kijeshi walioshiriki katika vita mbali mbali za kikoloni na kwa hiyo lengo la uteuzi wao lilikuwa ni kudhibiti wananchi kwa manufaa ya kiuchumi ya kikoloni; wengi wa Wakuu wa Mikoa na Wilaya wa Tanzania ya leo ni makada wa CCM. Mamlaka ya watu hawa hayatokani na wananchi kwani hawachaguliwi na mtu yeyote; na, kwa sababu hizo hizo, hawawajibiki kwa wananchi kwa utekelezaji wa kazi na majukumu yao. Aidha, kama ilivyokuwa wakati wa ukoloni, wengi wao bado ni wanajeshi. Kwa vyovyote vile, lengo la uteuzi wa Wakuu hawa wa Wilaya ni kudhibiti wananchi – na katika zama hizi za vyama vingi vya siasa, vyama vya upinzani - kwa manufaa ya CCM. Hii inathibitishwa na matakwa ya Katiba ya CCM yenyewe. Mheshimiwa Spika, Katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita Rais Kikwete – kwa kutumia mamlaka yake chini ya ibara ya 2(2) ya Katiba – amegawa mikoa mipya ya Geita, Katavi, Njombe na Simiyu. Aidha, kwa kutumia mamlaka hayo hayo, Rais Kikwete amegawa wilya mpya za Chemba katika Mkoa wa Dodoma; Mbogwe katika Mkoa mpya wa Geita; Mlele katika Mkoa mpya wa Katavi; Buhigwe, Kakonko na Uvinza katika Mkoa wa Kigoma; Butiama katika Mkoa wa Mara; Momba katika Mkoa wa Mbeya; Wanging’ombe katika Mkoa mpya wa Njombe; Nyasa katika Mkoa wa Ruvuma; Busega na Itilima katika Mkoa mpya wa Simiyu; Ikungi na Mkalama katika Mkoa wa Singida na Kaliua katika Mkoa wa Tabora. Sambamba na ugawaji wa mikoa na wilaya mpya, Rais Kikwete pia aliteua Wakuu wapya wa Mikoa na Wilaya husika.
WAKUU WA WILAYA NA CCM
Mheshimiwa Spika, Wakuu wa Mikoa na Wilaya wote ni, na wanatakiwa kuwa, wanachama wa CCM. Hii ni kwa sababu, tangu kuanzishwa kwake mwaka 1977, Wakuu wa Wilaya wamekuwa ni wajumbe wa vikao vyote vikuu vya CCM katika ngazi ya Wilaya. Kwa mfano, kwa mujibu wa Katiba ya CCM Toleo la 1982, Mkuu wa Wilaya ni mjumbe wa Mkutano Mkuu wa Wilaya (ibara ya 42(3); ni mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Wilaya (ibara ya 44(3); na ni mjumbe wa Kamati ya Siasa ya Halmashauri Kuu ya Wilaya (ibara ya 46(3). Hata baada ya miaka thelathini tangu toleo hilo la Katiba ya CCM litolewe, na licha ya miaka ishirini ya mfumo wa vyama vingi vya siasa nchini, hali bado iko vile vile kuhusiana na nafasi ya Wakuu wa Wilaya katika vikao rasmi vya CCM. Ndio maana, kwa mujibu wa ibara ya 76(1)(c) ya Katiba ya CCM Toleo la 2010, Mkuu wa Wilaya ni mjumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM wa Wilaya; ni mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM ya Wilaya (ibara ya 78(1)(c); na ni mjumbe wa Kamati ya Siasa ya Halmashauri Kuu ya CCM ya Wilaya (ibara ya 80(1)(c). Mheshimiwa Spika, Kuna ushahidi wa kutosha kwamba kugawa mikoa na wilaya ni namna tu ya kupata fursa ya kuwapatia makada wa CCM – ambao kwa sababu mbali mbali wamekosa - nyadhifa na marupurupu serikalini kwa kuwateua kuwa Wakuu wa Mikoa na wa Wilaya. Uthibitisho wa kauli hii ni uteuzi wa Wakuu wapya wa Mikoa na Wilaya uliofanywa katika siku za karibuni na Rais Kikwete. Katika uteuzi huo, kati ya Wakuu wa mikoa wapya, wawili ni Wabunge wa Viti Maalum katika Bunge hili hili. Aidha, kati ya Wakuu wapya wa Wilaya, watano ni Wabunge wa Viti Maalum katika Bunge hili hili; 15 ni waliowahi kuwa Wabunge au wabunge wa Bunge la Afrika Mashariki; na 22 waligombea ubunge lakini wakashindwa kwenye hatua za kura za maoni za ndani CCM au kwenye Uchaguzi Mkuu. Aidha, Mheshimiwa Spika, katika hali inayoonyesha kukithiri kwa matumizi mabaya ya madaraka na rasilimali za umma, Wabunge wa Viti Maalum walioteuliwa kuwa Wakuu wa Mikoa na Wilaya wameendelea kushiriki katika vikao vinavyoendelea vya Bunge hili tukufu. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali itoe kauli rasmi mbele ya Bunge hili tukufu hawa Wakuu wa Mikoa na Wilaya Wabunge wanalipwa mshahara upi wanapokuwa Bungeni. Aidha, Serikali itoe kauli ni kwa nini watu hawa wanaendelea kuja Bungeni kuhudhuria vikao vya Bunge wakati wameshakubali uteuzi wao kama Wakuu wa Mikoa au Wilaya. Vile vile, Serikali ilieleze Bunge hili watu hawa wanamwachia nani majukumu yao ya Ukuu wa Wilaya wao wanapokuja Bungeni na kwa nini iwe hivyo. Zaidi ya hayo, kwa vile ibara ya 67(2)(g) ya Katiba inamwondolea mtu sifa za kustahili kuchaguliwa au kuteuliwa kuwa Mbunge “... ikiwa mtu huyo ameshika madaraka ya afisa mwandamizi katika utumishi wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano...”, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali itoe kauli rasmi mbele ya Bunge hili tukufu kama Wabunge wote walioteuliwa kuwa Wakuu wa Mikoa au Wilaya bado wana sifa za kuendelea kuwa Wabunge.
WAKUU WA WILAYA WANAJESHI
Mheshimiwa Spika, Kuna utata mkubwa wa kikatiba kuhusiana na baadhi ya wateuliwa wa Ukuu wa Mikoa na Wilaya. Kwanza, orodha ya Wakuu wapya wa Mikoa na Wilaya walioteuliwa na Rais Kikwete inaonyesha kuwapo pia wanajeshi nane, ambao kati yao watatu wanatajwa kuwa maafisa wastaafu wa Jeshi. Watano waliobaki hawatajwi kama wastaafu na kwa hiyo inaelekea bado wako katika utumishi wa Jeshi. Kama tulivyokwisha kusema katika maoni yetu, Wakuu wa Mikoa na Wilaya wanatakiwa kuwa wanachama wa CCM na wajumbe wa vikao vyote vikuu vya chama hicho katika mikoa na wilaya. Wakati jambo hili linaweza lisizue mshangao katika mazingira mengine, kuwateua wanajeshi kuwa Wakuu wa Mikoa na/au Wilaya katika mazingira ya sasa ya kisiasa ambapo wanatakiwa wawe wanachama wa CCM na wahudhurie vikao vya maamuzi vya chama hicho ni jambo lenye mgogoro mkubwa kikatiba. Hii ni kwa sababu, kwa mujibu wa ibara ya 147(3) ya Katiba, “itakuwa ni marufuku kwa mwanajeshi yeyote kujiunga na chama chochote cha siasa....” Ibara ya 147(4) inatafsiri ‘mwanajeshi’ kuwa “... ni askari aliyeajiriwa kwa masharti ya muda au ya kudumu katika Jeshi la Ulinzi, Jeshi la Polisi, Jeshi la Magereza au Jeshi la Kujenga Taifa.” Kwa sababu hiyo, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali itoe kauli rasmi mbele ya Bunge hili tukufu kama Wakuu wapya wa Mikoa ya Kagera, Wilaya za Kakonko, Kalambo, Kyerwa, Misenyi na Mlele ni ‘wanajeshi’ au walikwisha kustaafu ili Bunge hili tukufu lifahamu kama uanajeshi wao, Ukuu wao wa Wilaya uCCM wao vinaendana na matakwa ya Katiba ya nchi yetu.
KUENDEKEZA RUSHWA NA UFISADI
Mheshimiwa Spika, Uteuzi wa baadhi ya Wakuu wapya wa Wilaya unaashiria kukithiri kwa rushwa na ufisadi na kukosekana kwa maadili kwa mamlaka ya uteuzi. Hapa, Mheshimiwa Spika, tutatumia mifano ya Wakuu wa Wilaya ya Kishapu katika Mkoa wa Shinyanga, na Mbarali mkoani Mbeya. Katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010, Wilson Elisha Nkhambaku, ambaye ndiye Mkuu mpya wa Wilaya ya Kishapu, aliteuliwa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kuwa mgombea wake wa ubunge katika Jimbo la Singida Magharibi. Licha ya kuwekewa pingamizi dhidi ya uteuzi na aliyekuwa mgombea wa CCM, Bwana Nkhambaku alifanikiwa kuteuliwa na Msimamizi wa Uchaguzi wa Jimbo la Singida Magharibi kuwa mgombea ubunge wa CHADEMA katika Jimbo hilo. Hata hivyo, muda mfupi baada ya kampeni za uchaguzi kuanza rasmi, Bwana Nkhambaku alionekana katika mkutano wa kampeni za uchaguzi wa CCM katika Jimbo la Kibaha Vijijini uliohutubiwa na aliyekuwa Katibu Mkuu wa CCM Yusufu Makamba na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii Mheshimiwa Lazaro Nyalandu. Katika mkutano huo, Bwana Nkhambaku alitangaza kwamba amejitoa kwenye kugombea ubunge wa Jimbo la Singida Magharibi kwa tiketi ya CHADEMA na kwamba alikwisharudi CCM! Mheshimiwa Spika, Kifungu cha 48 cha Sheria ya Uchaguzi, Sura ya 343 ya Sheria za Tanzania kinaruhusu mgombea ubunge yeyote aliyeteuliwa na Msimamizi wa Uchaguzi kujitoa katika kugombea uchaguzi husika. Hata hivyo, Mheshimiwa Spika, kifungu cha 91B cha Sheria hiyo kinatamka wazi kwamba ni kosa la jinai ya rushwa ya uchaguzi kumrubuni au kumshawishi mgombea kujitoa kugombea kwa malipo, au ahadi ya malipo. Kwa mujibu wa kifungu hicho, adhabu ya kosa hilo ni kifungo kisichozidi miaka mitano jela. Aidha, Mheshimiwa Spika, kifungu cha 21(1)(b) cha Sheria ya Gharama za Uchaguzi, 2010 kinakataza mtu yeyote, moja kwa moja au kwa namna nyingine yoyote, yeye mwenyewe, wakala wake au kupitia chama chake cha siasa, kwa niaba yake kutoa au kusaidia kutoa au kumpatia wadhifa au sehemu ya ajira mpiga kura au mtu mwingine yeyote kwa nia ya kumshawishi mpiga kura huyo kuacha kupiga kura au kumrubuni kutenda kitendo hicho. Vile vile, kifungu cha 21(1)(f) cha Sheria hiyo kinatamka kwamba ni rushwa ya uchaguzi kwa kila mpiga kura ambaye amepokea au amekubali kupokea wadhifa, sehemu au ajira kwa ajili yake mwenyewe kwa ajili ya kuacha kupiga kura wakati wowote wa uchaguzi. Kwa mujibu wa kifungu cha 94 cha Sheria ya Uchaguzi, makosa haya mawili ya jinai yana adhabu ya faini isiyopungua shilingi laki tano au kifungo cha kati ya mwaka mmoja hadi mitatu jela au vyote viwili kwa pamoja. Hoja hapa, Mheshimiwa Spika, ni kwamba uteuzi wa Wilson Elisha Nkhambaku kuwa Mkuu wa Wilaya ya Kishapu ni ushahidi wa wazi wa rushwa ya uchaguzi. Ni wazi kwamba mtu huyo alirubuniwa au kushawishiwa kujitoa kugombea ubunge kwa niaba ya CHADEMA. Hilo lilikuwa kosa la jinai kwa mujibu wa kifungu cha 91B cha Sheria ya Uchaguzi. Sasa mtu huyo amepewa wadhifa wa Mkuu wa Wilaya. Nalo ni kosa la jinai kwa mujibu wa kifungu cha 21(1)(b) na (f) cha Sheria ya Gharama za Uchaguzi. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali itoe kauli rasmi mbele ya Bunge hili tukufu kama ni sera ya Serikali hii ya CCM kuhonga wagombea wa vyama vingine kwa kuwapa nyadhifa katika utumishi wa umma ili wajitoe kama wagombea wa vyama vyao. Aidha, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali itoe kauli rasmi Bungeni kama mtu aliyepokea rushwa ya wadhifa ili ajitoe kuwa mgombea ubunge anastahili kupewa wadhifa wa Mkuu wa Wilaya au wadhifa mwingine wowote katika utumishi wa umma.
KUENDEKEZA SIASA ZA KIBAGUZI
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni imeshangazwa na kusikitishwa sana na uteuzi wa Bwana Kifu Gulamhussein Kifu kuwa Mkuu wa Wilaya ya Mbarali. Wakati wa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2000, Bwana Gulamhussein Kifu alichaguliwa kuwa Mbunge wa Jimbo la Kigoma Kusini. Hata hivyo, matokeo ya uchaguzi wake yalipingwa katika Mahakama Kuu na baadae katika Mahakama ya Rufani ya Tanzania. Mnamo tarehe 18 Juni 2002, Mahakama ya Rufani ya Tanzania katika Shauri la Rufaa Na. 2 la 2002 katika Manju Salum Msambya dhidi ya Mwanasheria Mkuu na Kifu Gulamhussein Kifu, ilifuta matokeo ya uchaguzi wa Bwana Gulamhussein Kifu kwa sababu Mahakama ya Rufani ilithibitisha kwamba mtu huyo alifanya kampeni kwa misingi ya ukabila. Mahakama ya Rufani ilinukuu kauli ifuatayo ya Bwana Gulamhussein Kifu wakati wa kampeni za uchaguzi huo: “... Waha wenzangu tuelewe kwamba mwaka huu ni mwaka wetu kujikomboa. Tumetawaliwa na kabila la Wabembe kwa muda mrefu. Kabila la Wabembe tunajua ni watu wa Kongo siyo wa Tanzania. Ni ajabu Waha tulio wengi katika jimbo hili tuendelee kutawaliwa na kabila chache. Muha popote alipo ahakikishe anipigie mimi Muha mwenzie. Angalieni wanakuja watu huku. Yuko mtu aliyepandikizwa na Msambya. Huyu mtu anakuja na Kabourou.... Kabourou na Msambya wote ni damu ya Kongo, wote ni Wanyakumawe.” Katika mkutano mwingine wa kampeni, Mahakama ya Rufani ilithibitisha kwamba Bwana Gulamhussein alitamka maneno yafuatayo: “Tumetawaliwa na wageni kwa muda mrefu ... umefika wakati wa kujikomboa kutoka kwa wageni kutoka Kongo.... Ni wakati mzuri kunichagua mimi kama Muha, Muha mwenzenu ... kwa kuwa sisi ndio tulio wengi katika jimbo hili.” Sasa mtu huyu aliyepatikana na hatia ya kufanya siasa za kibaguzi za aina hii ameteuliwa kuwa Mkuu wa Wilaya. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali itoe kauli rasmi mbele ya Bunge hili tukufu kwamba uteuzi wa Bwana Gulamhussein Kifu uko sambamba na matakwa ya Katiba yetu inayopinga aina zote za kibaguzi.
‘KUSOGEZA MAENDELEO KWA WANANCHI’?
Mheshimiwa Spika, Kuna dhana imejengwa na kuaminishwa kwa wananchi kwa miaka kwamba lengo la kugawa mikoa au wilaya mpya ni “... kusogeza na kurahisisha utoaji wa huduma kwa wananchi”, na kwa hiyo inaonekana kama jambo jema. Ndio maana suala la kutenga maeneo katika wilaya au mikoa mipya limejitokeza sana katika chaguzi za miaka ya karibuni kama sehemu ya ahadi za kampeni wagombea urais wa CCM. Dhana hii haina budi kuhojiwa na ukweli wake, kama upo, kuthibitishwa. Kwanza, nchi zote jirani na Tanzania ambazo zina mikoa au majimbo machache zaidi yetu hazina tofauti kubwa ya kimaendeleo na nchi yetu. Nyingine kama Kenya, kwa mfano, yenye majimbo 11 na ambayo sehemu yake kubwa ya Kaskazini na Kaskazini Mashariki ni nusu jangwa ina uchumi mkubwa kuliko wa Tanzania ambayo sasa ina mikoa ishirini na saba. Pili, hakuna ushahidi wa kuthibitisha kwamba kugawa mikoa au wilaya mpya kunaongeza bajeti ya maendeleo ya maeneo husika hasa hasa katika miradi ambayo ina umuhimu kiuchumi au kijamii kwa wananchi. Badala yake, ushahidi uliopo unaonyesha kwamba gharama za uendeshaji wa Serikali – yaani bajeti ya matumizi ya kawaida - zinaongezeka pale ambapo mikoa na wilaya mpya zinapotengwa. Kwa mfano, kwa mujibu wa Juzuu ya III Makadirio ya Matumizi ya Kawaida ya Mikoa kwa mwaka huu wa fedha 2012/2013, bajeti ya matumizi ya kawaida ya mikoa katika mwaka wa fedha 2010/2011 ilikuwa shilingi trilioni 1.887 na shilingi trilioni 2.321 katika mwaka wa fedha 2011/2012. Hii ilikuwa kabla ya kuongezwa kwa mikoa minne mipya na wilaya mpya kumi na tisa. Hata hivyo, baada ya kuongezwa kwa mikoa mipya minne, bajeti ya matumizi ya kawaida ya mikoa katika mwaka huu wa fedha imepanda hadi kufikia shilingi trilioni 2.882. Hii ndio kusema kwamba katika kipindi cha miaka miwili 2010/2011 – 2012/2013, bajeti ya matumizi ya kawaida imeongezeka kwa takriban asilimia 53. Kwa mujibu wa Makadirio haya, bajeti ya matumizi ya kawaida ya mikoa mipya minne ya Geita, Katavi, Njombe na Simiyu ni shilingi bilioni 257.443 kwa mwaka huu peke yake. Kwa upande mwingine, bajeti ya matumizi ya kawaida ya wilaya kumi na tano zilizotajwa hapo juu ni shilingi bilioni 2.502 kwa mwaka huu wa fedha. Kwa hiyo, kwa mujibu wa Makadirio haya, gharama za kuendesha Serikali katika maeneo haya mapya kwa mwaka huu wa fedha peke yake ni takriban shilingi bilioni 260. Kwa ulinganisho, kwa mujibu wa Juzuu ya IV Makadirio ya Matumizi ya Miradi ya Maendeleo kwa Wizara na Mikoa kwa mwaka huu wa fedha inaonyesha kwamba bajeti ya maendeleo kwa ajili ya mikoa mipya minne iliyogawanywa mwaka huu ni shilingi bilioni 60.021. Hii ni sawa na asilimia 23.3 ya bajeti ya matumizi ya kawaida kwa kipindi hicho hicho. Makadirio haya hayaonyeshi fedha yoyote iliyotengwa kwa ajili ya miradi ya maendeleo katika wilaya mpya 19 zilizoanzishwa. Kwa ushahidi huu, Mheshimiwa Spika, dhana kwamba kutenga mikoa na wilaya mpya ni kusogeza maendeleo kwa wananchi ni kivuli cha kisiasa tu chenye lengo la kuhalalisha ongezeko la matumizi ya watawala. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaamini kwamba wakati umefika kwa nchi yetu kuweka utaratibu wa kikatiba na kisheria utakaodhibiti – kama sio kupunguza - ongezeko la maeneo ya kiutawala ambayo sio tu ni mzigo kwa walipa kodi bali ni mzigo kwa uchumi kwa ujumla kwani yanatumia rasilmali ambazo zingeelekezwa katika shughuli za maendeleo ya kiuchumi na kijamii.
UTEKAJI NYARA NA HAKI ZA BINADAMU
Mheshimiwa Spika, Mnamo usiku wa kuamkia tarehe 3 Julai 2012, Dr. Steven Ulimboka - kiongozi wa madaktari waliokuwa wamegoma kwa kudai haki na stahili zao mbali mbali – alitekwa nyara na kisha kuteswa kwa namna ya ukatili mkubwa na baadae kutupwa vichakani katika Msitu wa Mabwe Pande nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam. Tukio hili la kinyama na la aina yake lilitokea sambamba na kauli ya Waziri Mkuu ndani ya Bunge hili tukufu kwamba Serikali ilikuwa imeamua kuwa ‘litakalokuwa na liwe’ kuhusiana na mgogoro huo wa madaktari. Mara baada ya tukio hilo na kwa haraka kubwa, Serikali – kwa kupitia kwa Waziri wa Mambo ya Ndani na Waziri Mkuu mwenyewe – ilitoa taarifa ya kukanusha kuhusika kwake na tukio hilo. Hata hivyo, vyombo vya habari vimechapisha taarifa zinazoihusisha Serikali na kutekwa nyara na kuteswa kwa Dr. Ulimboka. Katika toleo lake la tarehe 11-17 Julai, 2012, gazeti la MwanaHalisi linataja maafisa watatu – Jack Zoka na ‘Rama’, wanaodaiwa kuwa maafisa wa Idara ya Usalama wa Taifa na Ujasusi, na ASP Ahmed Msangi ambaye ni Mkuu wa Upelelezi wa Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam – kuwa wahusika wakuu wa tukio hilo. Mheshimiwa Spika, Kuteka nyara kwa lengo la kuua au kuumiza ni kosa kubwa la jinai kwa mujibu wa sheria zetu. Chini ya kifungu cha 248 cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu, Sura ya 16 ya Sheria za Tanzania, “mtu yeyote anayemteka nyara mtu kwa lengo la mtu huyo kuuawa au kuwekwa kwa namna inayoweza kusababisha mtu huyo kuuawa anakuwa ametenda kosa na anaweza kufungwa jela kwa miaka kumi.” Aidha, kwa mujibu wa kifungu cha 250 cha Sheria hiyo, kuteka nyara kwa lengo la kumuumiza mtekwa nyara ni kosa la jinai vile vile na adhabu yake ni kifungo jela kwa muda wa miaka kumi. Kwa vyovyote vile, Dr. Ulimboka alitekwa nyara kwa lengo la ama kuuawa au kuumizwa. Kwa hiyo, kwa vyovyote vile, wahusika wa tukio hili la kinyama ni wahalifu kwa mujibu wa vifungu tajwa vya Kanuni ya Adhabu. Watu hawa wanatakiwa kuchukuliwa hatua stahili za kisheria. Kwa sababu hiyo, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inamtaka Mkurugenzi wa Mashtaka atumie mamlaka yake chini ya Katiba na chini ya Sheria ya Utumishi wa Mashtaka ya Taifa, Na. 27 ya 2008 (National Prosecutions Service Act, 2008) na kuamuru kukamatwa kwa Jack Zoka, Rama na ASP Msangi ili tuhuma za kuhusika kwao na utekaji nyara na utesaji wa Dr. Ulimboka ziweze kupelelezwa kwa kina na ukweli wake kuthibitishwa. Kufanya hivyo, Mheshimiwa Spika, kutaonyesha wananchi kwamba Serikali haiungi mkono kwa vitendo vya kihalifu vinavyofanywa kwa kinachoelekea kuwa malengo ya kisiasa kama ilivyotokea kwa Waheshimiwa Wabunge Highness Kiwia wa Ilemela na Salvatory Machemli wa Ukerewe kukatwa mapanga mbele ya askari polisi, Waziri wa Uchukuzi Mheshimiwa Dr. Harrison Mwakyembe kuwekewa kinachoaminika kuwa ni sumu na Mhariri Mtendaji wa MwanaHalisi Saed Kubenea na mshauri wa habari na mawasiliano wa gazeti hilo Ndimara Tegambwage kuvamiwa kwa mapanga na kumwagiwa tindikali mwanzoni mwa Januari 2008. Kufanya hivyo kutaonyesha vile vile kwamba Serikali ya CCM haiko tayari kuruhusu vitendo vya mauaji kama namna mpya ya mapambano ya kisiasa katika nchi yetu.
UENDESHAJI WA MASHTAKA YA JINAI
Mheshimiwa Spika, Mamlaka ya uendeshaji wa mashtaka ya jinai imekasimiwa kwa Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka kwa mujibu wa ibara ya 59B(2) ya Katiba. Aidha, kwa mujibu wa ibara ya 59B(4), katika kutekeleza mamlaka yake, “Mkurugenzi wa Mashtaka atakuwa huru, hataingiliwa na mtu yeyote au na mamlaka yeyote na atazingatia ... nia ya kutenda haki, kuzuia matumizi mabaya ya taratibu za utoaji haki na maslahi ya umma.” Kanuni hii kuu imetamkwa pia na kifungu cha 8 cha Sheria ya Utumishi wa Mashtaka ya Taifa, Na. 27 ya 2008 (National Prosecutions Service Act, 2008) ambayo pia imefafanua na kutilia nguvu mamlaka haya ya kikatiba. Kwa mujibu wa Sheria hii, Mkurugenzi wa Mashtaka ana mamlaka sio tu ya kudhibiti mashtaka yote ya jinai bali pia kuratibu shughuli za upelelezi wa makosa ya jinai [kifungu cha 16(1)]. Aidha, kwa mujibu wa kifungu cha 17(1) na (3), Mkurugenzi ana uwezo wa kutoa maelekezo ya maandishi kwa ofisa yeyote wa umma ili apatiwe taarifa yoyote inayohusu upelelezi au uendeshaji wa mashtaka ya jinai na ofisa huyo anatakiwa kutii maelekezo hayo. Mheshimiwa Spika, Ili kumwezesha Mkurugenzi wa Mashtaka kutekeleza wajibu wake wa kikatiba kwa uhuru kamili na bila woga au upendeleo, Mkurugenzi wa Mashtaka amewekewa kinga ya ajira yake. Kwa mujibu wa kifungu cha 19(1) na (2) cha Sheria ya Utumishi wa Mashtaka ya Taifa, sifa, masharti na mafao ya ajira ya Mkurugenzi wa Mashtaka yatakuwa sawa na yale ya ajira ya Jaji wa Mahakama Kuu. Aidha, kwa mujibu wa kifungu cha 19(3), Mkurugenzi wa Mashtaka hawezi kuondolewa kwenye madaraka yake isipokuwa kwa kushindwa kutimiza wajibu wake kwa sababu ya ugonjwa au kwa kukiuka Kanuni za Maadili ya Kitaaluma ya Maafisa wa Sheria, Mawakili wa Serikali na Wanasheria Walioko kwenye Utumishi wa Umma chini ya Sheria ya Utekelezaji wa Mamlaka ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Sura ya 268 ya Sheria za Tanzania. Hii ndio kusema kwamba, kwa mujibu wa Sheria, utaratibu wa kumwondoa Mkurugenzi wa Mashtaka kwenye ajira yake hauna tofauti na utaratibu wa kumwondoa Jaji wa Mahakama Kuu kwenye ajira yake. Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaamini kwamba utaratibu huu wa kikatiba na kisheria umempa Mkurugenzi wa Mashtaka nyenzo za kutosha kisheria za kupambana na uhalifu mkubwa hapa nchini na vile vile kuzuia matumizi mabaya ya mfumo wa uendeshaji na utoaji haki na hasa hasa ya mfumo wa mashtaka ya jinai. Licha ya kuwa na mamlaka na kinga hizi za kisheria, Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka imeshindwa kutekeleza wajibu wake ipasavyo. Hii inathibitishwa na kitendo cha Serikali kurudia takwimu zilizotolewa mwaka jana ndani ya Bunge hili juu ya kesi kubwa za rushwa zilizofunguliwa na Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Jinai zikiwamo kesi za wizi wa fedha za Benki Kuu ya Tanzania (EPA), uhujumu uchumi, kuisababishia serikali hasara, kusafisha fedha haramu na wizi wa kutumia silaha. Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inashangazwa na kusikitishwa na kushindwa kwa Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka kufungua na/au kuendesha mashtaka yanayohusu matukio makubwa ya ufisadi ambayo yametikisa taifa letu Serikali ya Awamu ya Nne ilipoingia madarakani miaka saba iliyopita. Hii ni kwa sababu tangu mwaka 2007, kumekuwapo kwa ushahidi wa kutosha unaowaunganisha viongozi na maafisa waandamizi wa Serikali ya Awamu ya Tatu na wa Awamu ya Nne na maswahiba wao wa kibiashara katika kashfa kubwa za Meremeta Ltd., Tangold Ltd., Deep Green Finance Ltd., Kagoda Agricultural Co. Ltd., Kiwira Coal Mine, Radar ya BAE Systems, Richmond, Dowans na nyinginezo nyingi. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali itoe kauli rasmi mbele ya Bunge hili tukufu juu ya kushindwa kwake kuwachukulia hatua stahiki wahusika wa kashfa hizi.
UBAMBIKIZAJI RAIA KESI ZA UONGO
Mheshimiwa Spika, Kwenye maoni yetu ya mwaka jana tulilalamikia kushindwa kwa Mkurugenzi wa Mashtaka ya Jinai kutimizima wajibu wake kikatiba na kisheria kuzuia matumizi mabaya ya utaratibu wa utoaji haki. Kwa kutumia mfano wa yaliyomkuta Diwani wa Kata ya Bumera katika Halmashauri ya Wilaya ya Tarime Mheshimiwa Tengera Marwa, tulionyesha jinsi ambavyo Jeshi la Polisi limekithiri vitendo vya kukamata na kufungulia wananchi kesi za uongo zinazohusu tuhuma za makosa makubwa ya jinai ambayo hayana dhamana kisheria. Aidha, tulionyesha jinsi ambavyo msongamano wa mahabusu katika magereza yetu kulingana na idadi ya wafungwa ni ishara ya kushindwa kwa mfumo wa dhamana chini ya Sheria ya Mwenendo wa Jinai, Sura ya 20 ya Sheria. Mheshimiwa Spika, Katika maelezo yake mbele ya Kamati, Waziri wa Katiba na Sheria amesema kwamba Wizara yake imeunda Jukwaa la Taifa la Haki Jinai (The National Criminal Justice Forum) ili “... kutoa fursa kwa wadau wa Haki-Jinai kutafuta ufumbuzi wa changamoto zilizopo katika mfumo wa utoaji haki-jinai....” Mheshimiwa Waziri aliiambia Kamati kwamba katika miezi Februari na Mei ya mwaka huu, ‘Kamati Maalum’ ya Jukwaa hilo “... iliunda timu ndogo iliyotembelea baadhi ya magereza nchini kutatua baadhi ya kero zinazowasibu wafungwa na mahabusu.”
DHARAU KWA MAHAKAMA KUU
Huku, Mheshimiwa Spika, ni kupoteza muda na fedha na rasilmali kidogo tulizo nazo. Ufumbuzi wa matatizo ya kufurika kwa mahabusu katika magereza ya nchi yetu utapatikana kwa kufumua na kubadilisha kabisa mfumo wetu wa dhamana chini ya Sheria ya Mwenendo wa Jinai ambao unakataza dhamana kwa idadi kubwa ya watuhumiwa wa makosa yaliyotajwa katika kifungu cha 148(5)(a) na (e) ya Sheria hiyo. Vifungu hivi viwili ndio chanzo kikubwa cha polisi kubambikiza wananchi wasio na hatia kesi za uongo kwa lengo la kuwakamua, na ndio chanzo kikubwa cha msongamano katika mahabusu na magereza yetu. Kama ilivyosema Mahakama Kuu katika kesi ya Jackson s/o ole Nemeteni @ ole Saibul @ Mdosi @ Mjomba na wenzake 19 dhidi ya Mwanasheria Mkuu, Shauri la Madai Na. 117 la 2004, bila kuwepo utaratibu uliowekwa na sheria kama inavyoelekezwa na ibara ya 15(2)(a) ya Katiba, “utekelezaji wa masharti ya kifungu cha 148(5)(a) umetumiwa vibaya.” Kwa sababu hiyo, Mheshimiwa Spika, Mahakama Kuu ilitamka kwamba kifungu hicho kinachokataza dhamana kwa watuhumiwa wa makosa ya wizi wa kutumia silaha ni kinyume cha ibara ya 15(2)(a) ya Katiba. Mheshimiwa Spika, Kuhusiana na kifungu cha 148(5)(e) cha Sheria ya Mwenendo wa Jinai kinachoweka masharti ya dhamana ‘yasiyotekelezeka’ kwa watuhumiwa wa makosa ya uhujumu uchumi, Mahakama Kuu – katika kesi ya Prof. Dr. Costa Ricky Mahalu & Mwenzake dhidi ya Mwanasheria Mkuu, Shauri la Maombi Na. 35 la 2007 – ilitamka kwamba kifungu hicho ni cha kibaguzi kwa watuhumiwa maskini na kinakiuka matakwa ya ibara ya 13(2) ya Katiba inayokataza ubaguzi ‘ama wa dhahiri au kwa taathira....’ Kwa kutumia mamlaka yake chini ya ibara ya 30(5) ya Katiba, badala ya kukifuta kifungu hicho, Mahakama Kuu katika kesi zote mbili iliielekeza Serikali ifanye marekebisho katika kifungu cha 148(5)(a) na (e) ya Sheria ya Mwenendo wa Jinai ili kuweka utaratibu bora zaidi wa kushughulikia dhamana za watuhumiwa wa makosa ya wizi wa kutumia silaha na wa uhujumu uchumi. Katika Kesi ya Jackson s/o ole Nemeteni, Mahakama Kuu ilitoa muda wa miezi kumi na nane – kuanzia tarehe 13 Julai, 2007. Na katika Kesi ya Prof. Dr. Costa Ricky Mahalu, Mahakama Kuu ilitoa muda wa mwaka mmoja kuanzia tarehe 4 Oktoba, 2010. Hii ina maana kwamba Serikali ilitakiwa iwe imetekeleza maelekezo ya Mahakama Kuu juu ya kifungu cha 148(5)(a) kufikia tarehe 12 Desemba, 2008. Aidha, Serikali ilitakiwa kutekeleza maelekezo ya Mahakama Kuu kuhusu kifungu cha 148(5)(e) kufikia tarehe 3 Oktoba, 2011. Huu ni mwaka wa nne na nusu tangu kwisha kwa muda uliowekwa katika Kesi ya Jackson s/o ole Nemeteni lakini Serikali haijafanya marekebisho tajwa ya Sheria ya Mwenendo wa Jinai. Aidha, miezi sita imekwishapita tangu muda uliowekwa katika Kesi ya Prof. Dr. Costa Ricky Mahalu lakini Serikali haijatekeleza maelekezo hayo. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali itoe kauli rasmi mbele ya Bunge hili tukufu ni kwa nini imepuuza maelekezo ya kikatiba ya Mahakama Kuu kuhusu marekebisho ya sheria ambazo Mahakama ya Tanzania imetamka kwamba zinakiuka Katiba. Aidha, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali itoe kauli rasmi kama, na lini, inatarajia kutekeleza maelekezo hayo ya Mahakama Kuu.
TUME YA MABADILIKO YA KATIBA
Mheshimiwa Spika, Tume ya Mabadiliko ya Katiba ilianza kazi Mei Mosi 2012 baada ya Rais Kikwete kufanya uteuzi wa wajumbe na Makatibu wa Tume. Katika mwaka wa fedha 2011/2012, Tume ilitengewa jumla ya shilingi bilioni 6. 575 kwa ajili ya utekelezaji wa majukumu yake kwa kipindi cha Mei hadi Juni, 2012. Kati ya fedha zilizoidhinishwa, Wizara imekiri kupokea shilingi bilioni 3.625 au asilimia 55 ya fedha iliyoidhinishwa. Katika randama ya Fungu 08 la Tume ya Mabadiliko ya Katiba iliyowasilishwa kwa Kamati mwezi uliopita, Serikali ilipendekeza matumizi ya shilingi bilioni 39.95 kwa ajili ya matumizi mengineyo ya Tume kwa mwaka wa fedha 2012/2013. Hata hivyo, baada ya Kamati kuhoji busara ya makadirio haya makubwa, Wizara ilipunguza jumla ya shilingi bilioni 6.005 katika makadirio ya bajeti ya Tume, na hivyo kubakiwa na makadirio ya shilingi bilioni 33.944. Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inatambua umuhimu wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba kupatiwa rasilimali zote zinazohitajika ili kuiwezesha kutekeleza vyema majukumu yake mengi na makubwa. Hata hivyo, Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaamini kwamba umuhimu wa Tume sio leseni ya matumizi yasiyoelezeka na yasiyokubalika ya fedha za umma hasa hasa katika mazingira ambayo wananchi wanahubiriwa na watawala kwamba miradi ya maendeleo yao ya kiuchumi na kijamii haitekelezeki kwa sababu ya ufinyu wa bajeti ya Serikali. Aidha, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaamini kwamba kuteuliwa kuwa mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba ni fursa adimu na ya heshima kubwa ya kulitumikia taifa inayokuja mara chache sana katika maisha ya taifa. Ni fursa wanayopata watu wachache sana katika historia ya taifa lolote. Mheshimiwa Spika, Mapendekezo ya makadirio ya bajeti ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba yanatishia kuigeuza heshima ya kutumikia waliyopewa wajumbe wa Tume kuwa hongo ya Serikali. Hii ni kwa sababu, katika bajeti ya shilingi bilioni 33.944, Serikali inapendekeza kuwalipa wajumbe na watendaji wa Tume posho mbali mbali za jumla ya shilingi bilioni 14.633 au asilimia 43 ya bajeti nzima ya Tume kwa mwaka huu wa fedha peke yake. Hivyo, kwa mfano, kila mjumbe wa Tume atalipwa posho ya kikao (sitting allowance) ya shilingi laki mbili kila siku kwa mwaka mzima, kikao kiwepo au kisiwepo! Posho hizi za vikao peke yake zitagharimu jumla ya shilingi bilioni 9.594 kwa mwaka huu wa fedha 2012/2013. Aidha, Mheshimiwa Spika, kila mjumbe wa Tume atalipwa jumla ya shilingi elfu hamsini kila siku kwa mwaka mzima kama posho ya majukumu (responsibility allowance), awepo kazini au asiwepo kazini! Posho hii nayo itawagharimu walipa kodi wa Tanzania shilingi milioni 630 kwa mwaka huu wa fedha peke yake. Vile vile kuna shilingi milioni kumi ya posho ya matibabu “... kwa wajumbe ambao hawamo kwenye utaratibu wa Serikali wa kugharamia matibabu na madawa.” Zaidi ya hayo, wajumbe wa Tume na Sekretarieti yake watalipwa posho ya kujikimu wanaposafiri ndani ya nchi kikazi ya jumla ya shilingi bilioni 4.399 kwa mwaka huu wa fedha pekee. Mheshimiwa Spika, Sio malipo ya posho hizi tu ndio yenye mgogoro. Kwa mujibu wa randama ya Tume, shilingi bilioni 2.032 “... zitatumika kulipia gharama za nyumba za wajumbe na Sekretarieti ya Tume.” Kwa mujibu wa majukumu yake chini ya Sheria ya Mabadiliko ya Sheria, Sura ya 83 ya Sheria za Tanzania, Tume inatakiwa kukusanya maoni ya wananchi nchi nzima na, kwa sababu hiyo, wajumbe wanatazamiwa kuwa safarini katika sehemu mbali mbali za nchi yetu. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali kutoa kauli mbele ya Bunge hili tukufu kwa nini wajumbe na Sekretarieti wanapangishiwa nyumba Dar es Salaam wakati wanatakiwa kutembelea maeneo mbali mbali nchini wakikusanya maoni ya wananchi. Aidha, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali ieleze Bunge hili tukufu gharama zote za kila Mjumbe wa Tume, Sekretarieti na watumishi wengine wote wa Tume ili Wabunge na wananchi wa Tanzania wafahamu kodi wanazolipa zinavyotumika katika mchakato wa Katiba Mpya. Mheshimiwa Spika, Matumizi ya aina hii ndio yanayoifanya Serikali isiaminike kwa wananchi pale inapodai kwamba matatizo makubwa ya malipo ya mishahara na marupurupu yanayowakabili watumishi wa sekta ya afya, elimu, n.k. yanatokana na upungufu au ukosefu wa fedha. Serikali hii haiwezi kuaminika inapowaambia madaktari wetu kwamba haiwezi kuwalipa stahili zao kwa sababu ya ufinyu wa bajeti, au inapowahubiria wanafunzi wetu wa elimu ya juu juu ya ‘sungura mdogo.’ Kwa sababu hizi, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaishauri Serikali iwalipe wajumbe wa Tume mshahara wa kila mwezi – hata kama ni kwa viwango vya juu kabisa vya mishahara ya watumishi wa umma - kwa muda wote watakapokuwa wanatekeleza majukumu ya Tume. Aidha, kwa vile Sekretarieti ya Tume inaundwa na watu ambao tayari wapo katika utumishi wa umma, watu hawa waendelee kulipwa mishahara waliyonayo kwa kazi zao za sasa ila wahesabike kwamba wako Tume kwa secondment. Vile vile, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni haioni mantiki yoyote ya kutumia mabilioni ya fedha za wananchi kuwapangishia nyumba wajumbe wa Tume na Sekretarieti juu ya malipo mengine makubwa yanayopendekezwa. Lazima, kama taifa, tushone koti letu kulingana na ukubwa wa kitambaa tulicho nacho!
MWISHO
Mheshimiwa Spika, Napenda kuchukua fursa hii kuwashukuru wajumbe wote wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni chini ya uongozi wa Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni Mheshimiwa Freeman A. Mbowe kwa ushauri na ushirikiano uliowezesha maandalizi ya maoni haya. Aidha, niwashukuru familia yangu – mke wangu mpenzi Alicia Bosensera na mapacha wetu Agostino Lissu na Edward Bulali – kwa kuendelea kuvumilia upweke unaotokana na ‘Daddy’ kuwa mbali muda mwingi kwa sababu ya majukumu mazito ya kibunge. Aidha, niwashukuru wapiga kura wangu wa Jimbo la Singida Mashariki kwa imani na nguvu wanayonipa kila siku kwa kuendeleza msimamo wetu thabiti wa kukataa kunyanyaswa, kunyonywa na kupuuzwa na ‘Ndaa ya Njou’! Mwisho naomba nichukue fursa hii kuwashukuru viongozi, wanachama na wapenzi Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) na wananchi wote wa Tanzania ambao wameendelea kutuunga mkono na kututia nguvu katika kipindi hiki muhimu katika historia ya nchi yetu. Ninawaomba waendelee kutuunga mkono na kututia nguvu katika siku ngumu na za majaribu makubwa zinazokuja! Mheshimiwa Spika, Baada ya maelezo haya marefu, naomba kukushukuru na wewe binafsi na naomba kuwasilisha.
---------------------------------------------------------------
Tundu Antiphas Mughwai Lissu
MSEMAJI & WAZIRI KIVULI, SHERIA, KATIBA NA UTAWALA
KAMBI RASMI YA UPINZANI BUNGENI

No comments:

Post a Comment